Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
BENKI ya NMB imezindua huduma ya kimkakati kwa ustawi wa sekta ya Fedha na Uchumi wa Taifa ‘NMB Worldwide Pesa, inayowapa fursa Watanzania ya kutuma na kupokea pesa kutoka nchi 22 za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kupitia simu za mkononi.
Uzinduzi wa NMB Worldwide Pesa ‘Dhumuni Halina Mipaka,’ umefanyika jijini Dar es Salaam,Novemba 28,2024 ikizinduliwa na Mkurugenzi wa Biashara ya Kimataifa na Diplomasia ya Uchumi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi John Ulanga.
NMB Worldwide Pesa inayoletwa kwa ushirikiano wa NMB, Mastercard, Thunes, TerraPay na Nala, ni zao la maboresho maalum ya huduma ya Worldwide Pesa iliyozinduliwa mwaka jana, ikilenga kuwawezesha Watanzania waishio nje ya nchi ‘Diaspora,’ kutuma fedha nchini kutokea kote duniani.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Ofisa Mkuu wa Wateja Wakubwa na Serikali wa NMB, Alfred Shao,amesema dhamira ya huduma hiyo ni kusapoti lengo la Serikali la kuongeza kiwango cha fedha kinachopokelewa kutoka kwa Diaspora wa Tanzania hadi kufikia kiasi cha Trilioni 3.75 kwa mwaka ifikapo mwaka 2028.
“Kwa kulitambua lengo hilo, nasi kuunga mkono, NMB tuko hapa kuleta suluhisho muhimu la kuendana na adhma hiyo ya Serikali na taifa letu kwa ujumla, na Worldwide Pesa itakuwa na mchango sio tu wa kufanikisha lengo hilo,pia kutanua wigo wa huduma zetu na kuzifanya kuwa za kisasa zaidi,”amesema Shao na kuongeza:
“Kwetu sisi NMB, ni heshima kwetu kupata imani kutoka kwa washirika wetu ambao ni taasisi za fedha kama Mastercard, Thunes, TerraPay na Nala, ambazo zina mtandao mpana na uhusiano na benki kubwa za nchi nyingi za ndani na nje ya Afrika,”.
Aliongeza ya kuwa, ushirikiano wa taasisi hizo utaiwezesha NMB kuongeza tija ya huduma za kifedha (kutuma na kupokea), huku akitambia uwekezaji mkubwa ambao wameufanya kwenye Teknolojia ya Kidijitali hasa kwenye Kulinda Usalama wa Mifumo na Taarifa za Benki na Wateja ‘Cybersecurity Technologies.’
Kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mohamed Thabit Kombo, Balozi Ulanga aliipongeza NMB kwa mapinduzi chanya na uwekezaji wa kiteknolojia katika kufanikisha huduma rahisi, rafiki, nafuu na salama kwa ukuaji wa haraka wa uchumi wa wateja na Watanzania.
“Sisi kama Serikali tuna furaha kuona huduma yenu hii mpya imeanza na nchi 22 wanachama wa Jumuiya mbili kubwa Afrika yaani Afrika Mashariki (EAC) na Kusini mwa Afrika (SADC), kwani itakuwa chachu ya mzunguko wa fedha katika ukanda huu, ambao sisi ni wanachama wa jumuiya zote mbili,” amesisitiza.
Balozi Ulanga aliitaka NMB kuunda mfumo utakaowezesha matumizi ya huduma hiyo kutoka benki zote na kwamba hilo litaharakisha na kuongeza kasi ya ukuaji wa taasisi hiyo, ambayo kwa ilipofikia inapaswa kuvuka mipaka ya nchi na Bara la Afrika kutokana na ukubwa na ubora wake kihuduma
Kwa upande wake, Meneja wa Akaunti – Afrika Mashariki wa Thunes, Jack Ngari, aliishukuru NMB kwa kujenga msingi imara wa ushirikiano kihuduma na kwamba imani waliyopata kutoka kwenye benki, inawapa nguvu ya kushiriki ukuzaji uchumi wa Tanzania, jambo ambalo ni fahari kwao.
Naye Doreen Ngalo, ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa TerraPay,amesema wanajivunia miaka mitano ya ushirikiano wa kibiashara na NMB, wenye wastani wa miamala ya kimataifa yenye thamani ya zaidi ya Dola Mil. 1.2 na kwamba uzinduzi wa NMB Worldwide Pesa unawapa uhakika wa kuongezeka kwa miamala hiyo.
More Stories
DC Korogwe awataka viongozi wa vijiji kuwatumikia wananchi kwa uadilifu
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam