Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online.Morogoro
BENKI ya NMB imeendelea kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma zake kwa kufungua tawi jipya mkoani Morogoro, lililozinduliwa rasmi Jumatano katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).
Hatua hiyo ya kujizatiti kibiashara, pia inalenga kuimarisha uongozi wa benki hiyo katika utoaji wa huduma bora za kifedha nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduni huo mjini hapa leo Ofisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi amesema tawi hilo limeleta ahuweni kwa wanajumuiya wa SUA na wananchi, wanaoishi jirani na chuo hicho kwa kurahisisha upatikanaji wa huduma za benki hiyo.
“Kabla ya tawi hili la NMB SUA, wateja wetu hususan wafanyakazi wa hapa SUA na wanafunzi walilazimika kusafiri hadi Tawi la NMB Wami lililopo katikati ya mji wa Morogoro zaidi ya kilomita sita kupata huduma za kibenki. Sasa wakazi wa Magadu, Mzinga, Kididimo, Misufini, Vibandani, Kasanga, Lugala na Mafiga huduma za kibenki tumewasogezea karibu,” amesema.
Ameongeza; “Benki yetu imekuwa benki inayoongoza katika utoaji wa huduma za kifedha, kwa kigezo cha ukubwa wa faida pamoja na uwekezaji kwenye jamii inayotuzunguka na kwa kigezo cha mtandao wetu mpana wa matawi, ATM na NMB Wakala kutoa huduma kwa wateja”.
Mponzi amesema mtandao huo, sasa una matawi 227 ambayo yanaongezwa nguvu kihuduma na mashine za kutolea fedha (ATM) zaidi ya 800 na mawakala zaidi ya 9,000. Mkoa wa Morogoro sasa una matawi 14 na Kanda ya Mashariki 22.
“Leo hii (jana), tunafungua tawi letu la NMB SUA ambapo sasa wakazi wa Wilaya ya Morogoro watakua wamepata mahala pa kupata mahitaji yao yote ya kibenki,” amefafanua na kuhamasisha matumizi endelevu ya tawi hilo.
Naye mgeni rasmi Makamu Mkuu wa SUA, Prof Raphael Chibunda amewachagiza wanafunzi, wananchi wanaoishi jirani na chuo hicho pamoja na wakazi wote wa Morogoro kuchangamkia fursa hiyo mpya kwa ajili ya maendeleo yao binafsi na taifa kwa ujumla.
Amesema huduma za kibenki ni kati ya huduma muhimu kwa ustawi wa jamii na maendeleo ya kiuchumi na kuipongeza NMB kwa kuwa mdau mkubwa wa maendeleo ya kiuchumi nchini.
Pia amesema, sekta ya fedha ina umuhimu wa kipekee kimaendeleo kwani ndiyo inayowezesha shughuli zote za uchumi kama kuwekeza, malipo ya kibiashara na ya binafsi, uwekaji wa amana na kupatikana kwa mikopo ya aina zote.
Sambamba na uzinduzi huo, benki hiyo imetoa msaada wenye thamani ya sh. milioni 16.2 wa vifaa vya hospitali, madawati kwa ajili ya shule ya sekondari ya chuo hicho na fedha kwa ajili ya mradi wa miti.
Kwa upande wake Meneja wa NMB Kanda ya Mashariki, Dismas Prosper amesema thamani ya mashine ya kufulia nguo za wagonjwa ni sh. milioni 6.9 na viti vya kusukuma wagonjwa sh. milioni 1.8.
Amesema mradi wa miti umechangiwa sh. milioni 2.5 na madawati 55 yaliyotolewa yamegharimu sh. milioni tano.
More Stories
Elon Musk : Bill Gates atafilisika endapo…
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi
Lina PG Tour yafufua gofu Moshi