January 7, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NMB yazindua kampeni ya Onja Unogewe, Lipa Mkononi

Na Yusuph Mussa,Timesmajira Online, Mbeya

MKUU wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera amezindua kampeni ya Onja Unogewe ya Benki ya NMB, huku akiwahamasisha wananchi kutumia huduma hiyo ambayo ataweza kutoa fedha mahali popote kwenye simu za mkononi na matawi ya benki hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera akizungumza na wananchi (hawapo pichani) kwenye hafla ya uzinduzi wa Kampeni ya Onja Unogewe ya Benki ya NMB.

Akizindua kampeni hiyo Agosti 6, 2023 kwenye Stendi ya Mabasi ya Daladala (Nane Nane) jijini Mbeya, Homera ameema wananchi wengi hasa wafanyabiashara, wanaweka maisha yao rehani kwa kutembea na fedha nyingi mifukoni hasa wanapokwenda kununua bidhaa nje ya Wilaya ama mikoa yao ama nchi za Zambia na Malawi.

“Niwapongeze NMB kwa kuja na wazo zuri ambalo linakwenda kuweka wepesi wa ufanyaji malipo ya huduma na bidhaa mbalimbali kwani itakuwa ni msaada mkubwa sana. Natambua changamoto kubwa ambayo watu wengi wamekuwa wakiipata hasa ya kutembea na kiasi kikubwa sana cha fedha wanapo taka kufanya manunuzi mbalimbali, sasa hili tunalo kwenda kuzindua leo linakwenda kutatua changamoto hizo na kufanya urahisi wa malipo ya huduma na bidhaa,”.

“Kwa hapa Mbeya mjini, naamini wengi tunafahamu kuwa kumekuwa na uhalifu na wizi katika maeneo ya biashara, lakini pia tunatambua wafanya biashara wengi kutoka wilaya zingine na mikoa ya jirani wanakuja hapa kwa ajili ya kununua bidhaa za kwenda kufanyia biashara zao huko watokako hawa ni watu ambao wanasafiri na kiasi kikubwa cha fedha lakini pia huwaweka wafanyabiashara wa hapa Mbeya hatarini, kwani wanawaachia pesa nyingi sana madukani mwao,”amesema Homera.

Mkuu wa Idara ya Mtandao wa Matawi na Mauzo wa Benki ya NMB Donatus Richard akizungumza na wananchi (hawapo pichani) kwenye hafla ya uzinduzi wa Kampeni ya Onja Unogewe ya Benki ya NMB.

Homera amesema sasa NMB imekuja na suluhisho la kuweka pesa za wananchi kwenye akaunti na kutumia simu tu kufanya manunuzi au malipo ya huduma mbalimbali.

Hii ni nzuri kwa wanafamilia wa benki ya NMB inastahili pongezi zaidi katika hili kwani mbali na kumsaidia mwananchi kufanya malipo salama kabisa kwa pande zote mbili za muuzaji na mnunuaji bado mnunuaji anazawadiwa rejesho la mpaka asilimia 10 ya kiasi alicholipa.

“Kazi imebaki kwetu wateja kuendelea kujiunga na huduma hii ya NMB Mkononi na tuanze kuskani QR zao kwenye sehemu za huduma tupate rejesho hili,rai yangu kwa watu wa Mbeya ni kwamba muda ndio huu wa kuvuna mazuri kutoka benki hii tusilaze damu kabisa, tuchangamkie fursa,”.

Wananchi wakiwa kwenye hafla ya uzinduzi wa Kampeni ya Onja Unogewe ya Benki ya NMB.

Amesema ipo haja ya watanzania wengi kuendelea kuwa na akaunti za benki kwa maslahi makubwa ya uchumi wa nchi yetu, hivyo amewasisitiza wakazi wa Mbeya na Watanzania kwa ujumla kuwa wasisite kufungua akaunti za benki na wala wasiwe na hofu kuwa benki ni kwa ajili ya wenye kipato kikubwa, kwani benki ni kwa ajili ya watu wote.

Awali, Mkuu wa Idara ya Mtandao wa Matawi na Mauzo wa Benki ya NMB Donatus Richard amesema benki hiyo inawathamini na inatoa motisha kuendelea kutoa huduma na masuluhisho yaliyo bora yenye kukidhi mahitaji ya wananchi kama wateja, na zaidi kuendelea kuwaalika hata wasio wateja wao kwenda kujiunga nao na kufurahia huduma bora na salama zaidi.

“Tunajivunia kurahisisha upatikanaji wa huduma nafuu na salama za kibenki, kupitia mifumo na masuluhisho ya kidijitali ikiwemo, NMB mkononi, NMB pesa wakala, matumizi ya kadi, na huduma za intaneti,masuluhisho ya kutoa huduma kidijitali ikiwemo mikopo ya mshiko fasta, ambayo ni huduma ya mikopo ya kidijitali, isiyokuwa na dhamana, kupitia simu ya mkonon

Akizungumzia kampeni hiyo amesema imelenga kuwapatia huduma nzuri na fursa ya kuzijaribu ambapo tunasema ‘mnazionja’ na kwa kufanya hivyo zipo faida kubwa ambazo mtakuwa mkizipata wanaamini kuwa wengi watazipenda na kuendelea kuzitumia.

Richard amesema kwa namna ya kipekee, wanaileta huduma ya Lipa Mkononi ya Benki ya NMB ambapo kwa kutumia simu ya Mkononi ambayo tayari umeshajiunga na NMB Mkononi, utakwenda kufanya malipo ya bidhaa na huduma katika sehemu mbalimbali.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wafanyakazi wa NMB katika hafla ya uzinduzi wa kampeni ya Onja Unogewe ya benki hiyo

Vile vile kwa wateja ambao hawana akaunti na NMB, iwapo simu yako imeunganishwa na huduma za malipo kutoka Visa, MasterCard na Union Pay, unaweza kufanya malipo katika huduma zao za Lipa Mkononi (QR) zaidi ya laki moja (100,000) ambazo zimesambaa nchini kote.

“Watoa huduma na wafanyabiashara mbalimbali watapatiwa kitu kinaitwa QR Code, pamoja na namba ya malipo (yaani Lipa Namba) ambapo kama mteja wa benki hii hutakuwa na ulazima wa kubeba pesa bali kwa kutumia simu yako ya mkononi utafanya malipo kwa kuskani ile QR kwa wale wenye simu janja na kwa wale wenye hizi za kawaida (kitochi / kiswaswadu) basi utalipa kwa kutumia namba ya malipo.. Pindi mteja afanyapo malipo kwa njia hii, fedha inakwenda moja kwa moja kwenye akaunti ya mfanyabiashara, yaani instant payment, hivyo basi kumpa urahisi mfanyabiashara kutoa huduma bila wasiwasi.

“Sisi kama benki ya NMB hatutaishia kukurahisishia malipo lakini tutakurejeshea asilimia kumi ya fedha uliolipa kwenye akaunti yako Hii maana yake ni kwamba, ukifanya malipo ya 100,000 kwa kuskani QR ya NMB, baada ya malipo hayo, utarejeshewa sh. 10,000 kwenye akaunti yako” amesema Richard.