Na Angela Mazula,TimesMajira. Online
JUMLA ya sh. milioni 550 zitatolewa na Benki ya NMB kwa njia ya zawadi baada ya leo, kuzindua kampeni ya ‘Bonge la Mpango’ ambayo itawawezesha wateja wa benki hiyo, kujishindia fedha taslimu na zawadi nyingine lukuki.
Akitaja baadhi ya zawadi hizo Ofisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi jijini Dar es Salaam leo amesema zawadi hizo ni pikipiki ya miguu mitatu, gari aina ya Tata la kubebea mizigo maarufu na gari la kifahari aina ya Toyota Fortuner lenye thamani ya sh. milioni 169 ambalo litatolewa siku ya fainali.
“Tumeamua kuanzisha kampeni hii itakayodumu kwa miezi mitatu kama sehemu ya shukurani kwa wateja wetu baada ya mwaka jana kupata faida ya zaidi ya sh. bilioni 200 na kutangazwa na Jarida la Global Finance kuwa sisi ndiyo benki salama zaidi katika ardhi ya Tanzania kuweka fedha,” amesema.
Amesema wateja wote wa benki hiyo, wanaofikia milioni tatu wana nafasi ya kushinda zawadi hizo kwa kwa kuwa ni sehemu ya utaratibu wa NMB, kurudisha sehemu ya faida kwa wateja wake nchi nzima.
“Katika kipindi chote cha kampeni hii, wateja wote wanaoweka akiba walau sh. 100,000 wataingia kwenye droo ya wanaostahili zawadi zilizopo ambazo ni fedha taslimu sh. 500,000 kwa washindi 10 kila wiki, pikipiki ya miguu mitatu aina ya LIFAN na zawadi nyingine,” amesema.
Katika ufafanuzi wake, Mponzi amesema kampeni hii inalenga pia kwa wasio na akaunti za NMB kufungua akaunti, ili wawe sehemu ya kampeni kwa ajili wapate zawadi kwa kuwa kila mmoja kwa sasa anaugulia maumivu ya msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka uliomaliza fedha.
“Ili kukidhi vigezo na sifa za kujishindia zawadi zitakazotolewa, mteja anatakiwa kuweka akiba kwenye akaunti yake. Tukiwa benki inayoongoza nchini, tunakusudia kuhamasisha utamaduni wa kujiweka akiba.
“Mteja atakayeweka akiba ya sh. 100,000 na zaidi iwe kwa fedha taslimu au kuhamishia kwenda akaunti yake ya benki ya NMB, anajiweka kwenye nafasi ya kushinda zawadi zitakazotolea kila wiki na atakuwa sehemu ya watakaoshindania zawadi ya mwezi itakayotoa washindi watatu wa gari ya mizigo na pikipiki aina ya LIFAN,” amesema.
Hata hivyo droo ya mwisho itawahusisha wateja ambao wana akiba ya zaidi ya sh. milioni 10 kwenye akaunti zao iliyodumu kwa zaidi ya siku 30. Wateja hao wataweza kujishindia Toyota Fortuner.
Naye Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Donatus Richard amesema kampeni hiyo inashirikisha matawi nchi nzima na kuhakikisha inafanywa kwa ufanisi na weledi wa hali ya juu, ili kila mshiriki aweze kunufaika.
More Stories
Elon Musk : Bill Gates atafilisika endapo…
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi
Lina PG Tour yafufua gofu Moshi