December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NMB yawakutanisha walimu zaidi 200 kuadhimisha siku yao

Na Israel Mwaisaka, Timesmajira Online,Nkasi


BENKI ya NMB imewakutanisha Walimu zaidi ya 200 wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi katika kuadhimisha siku ya yao ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo namna ya kuitumia mikopo wanayoipata katika kujiimarisha kiuchumi na kujipanga vyema namna ya kuishi baada ya kustaafu.

Akizungumza na walimu hao Kaimu Meneja wa NMB Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Daniel Zake amesema wameiandaa siku hiyi ya Mwalimu Spesho kama hatua ya kutambua mchango wa walimu kama Moja ya kundi linalopata huduma za benki hiyo.

Amesema kuwa wameamua kukutana nao Ili kuwajengea uwezo namna ya kuitumia mikopo wanayoipata Ili iweze kuwanufaisha na kujiandaa katika maisha ya baadae hasa baada ya kustaafu badala ya kuendelea kuwapatia mikopo bila ya elimu namna njema ya matumizi ya fedha hizo .

Amefafanua kuwa benki hiyo inatamani kuona maisha ya Walimu yanakua endelevu hata baada ya kustaafu bila ya kuwa na wasiwasi wa kimaisha au kuyumba kiuchumi na kuwa suluhisho pekee kwao ni kukopa na kuiendeleza mikopo hiyo kwa kuzifanyia kazi zenye tija hasa uzalishaji utakaowawezesha kujiwekea akiba wenyewe kama maandalizi ya kuelekea kustaafu katika program yao ya jiwekee.

Meneja wa NMB tawi la Nkasi Josephine Fute amesema benki hiyo ina programu maalumu iitwayo “Jiwekee” na katika siku hii muhimu ya Mwalimu Spesho watafundishwa namna njema ya kujiwekea akiba ambayo itakua na msaada mkubwa baada ya kustaafu badala ya kutegemea kiinua mgongo pekee kinachotolewa na serikali.

Pia watawafundisha namna ya kupata mikopo mingine ikiwemo Ile ya kilimo,uvuvi,biashara na mengineyo ambayo itawasaidia kuwa wajasiriamali kwa kuwa na shughuli nyingine za kiuchumi nje ajira zao za ualimu.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Vicent Magendela amesema watumishi wengi wakiwemo walimu wamekua waathirika wakubwa wa kukosa elimu ya matumizi ya fedha hasa pale wanapopata fedha Kwa wingi baada ya kustaafu.

“Elimu hiyo itawasaidia kuwa na uzoefu wa kumiliki fedha nyingi toka wakiwa kazini na hata wakistaafu hakuna kitakachowachang’anya,”.

Hata hivyo amewataka walimu hao kuendelea kujifunza namna ya kutumia huduma hizo za kibenki sanjari na kufanya shughuli katika muda wa ziada ili hata baada ya kustaafu wasiwe wageni katika maisha mapya watakayokwenda kuyaishi.

Kwa upande wao walimu wamekiri kuishi maisha magumu baada ya kustaafu hasa baada ya kushindwa kuzitumia fedha nyingi zinazopatikana kwa mpigo ikiwa ni pamoja na kuandamwa na madeni mengi hasa kutokana na kukopa katika maeneo mbalimbali.

Benki ya NMB imekuwa na Utaratibu wa kukutana na Walimu na kuwajengea uwezo namna njema ya kuishi na kuepukana na mikopo umiza kutoka Kwa wakopeshaji binafsi ambao ni matapeli.