January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NMB yang’ara maonesho ya OSHA

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Katika maadhimisho ya siku ya afya na usalama mahali pa kazi duniani yanayoratibiwa kitaifa na Wakala wa Afya na Usalama Mahali pa kazi (OSHA), Benki ya NMB imetangazwa kuwa benki yenye sera bora ya usalama na afya mahali pa kazi katika sekta ya kibenki.

Benki ya NMB katika kilele cha maonesho hayo yaliyofanyika kwenye Viwanja vya Tumbaku mkoani Morogoro, ilinyakua tuzo tatu na kuendelea kuwa benki bora katika sekta ya fedha.

Katika kilele cha maadhimisho hayo yaliyofanyika Aprili 28 mwaka huu, NMB ilinyakua tuzo zifuatazo;

  • Mshindi wa jumla wa kwanza katika sekta ya fedha.
  • Sera bora ya afya na usalama mahali pa kazi kwa sekta za fedha
  • Banda bora katika sekta ya fedha

Kauli mbiu katika maadhimisho hayo ya mwaka huu ambayo yamefanyika kwa mara ya 19 nchini Tanzania ni, “Mazingira Salama na Afya ni Kanuni na Haki ya Msingi Mahali pa Kazi.”

Aidha, awali Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kilele cha maonesho hayo aliwataka waajiri wote nchini kuchukua hatua ya kuhakikisha wanalinda usalama na afya za wafanyakazi wao kama yalivyomatakwa ya Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi Namba 5 ya mwaka 2003.

Pia aliwaagiza kushirikiana na Wakala wa Afya na Usalama mahali pa kazi (OSHA) kuwapatia wafanyakazi elimu ya namna ya kutumia mifumo itakayostawisha mazingira ya afya na usalama mahali pa kazi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (wa pili kulia) akimkabithi Afisa Mwandamizi wa Afya na Usalama Mahali pa Kazi, Caroline Baraza moja ya tuzo kati ya tatu walizopokea Benki ya NMB.