December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NMB yakabidhi vitanda 40 Sekondari ya Kalambo

Na Israel Mwaisaka, TimesMajira Online, Rukwa

BENKI ya NMB kanda ya nyanda za juu jana imekabidhi msaada wa vitanda 40 vyenye thamani ya shilingi Milioni kumi na laki nne kwa shule ya sekondari ya wasichana kalambo kama sehemu ya utatuzi wa changamoto hiyo katika shule hiyo.

Akikabidhi vitanda hivyo 40 vitakavyokuwa na uwezo wa kutumiwa na Wanafunzi 80 kwa katibu tawala wa wilaya Kalambo Selivily Ndumbaro meneja wa NMB kanda ya nyanda za juu Straton Chilongola amesema msaada huo ni sehemu ya faida wanazozipata na kuweza kuirudisha kwa jamii.

Amesema kuwa Benki hiyo ilipata ombi kutoka kwa viongozi wa serikali wilayani Kalambo juu ya uhitaji wa vitanda kwa shule hiyo ya wasichana ambayo ni mpya na kuona umuhimu wa jambo hilo na wao kulipa uzito mkubwa na kuamua kutoa vitanda 40 vitakavyokwenda kutatua tatizo la ukosefu wa vitanda lililopelekea baadhi yao kulala chini.

Katibu tawala wa wilaya Selivil Ndumbalo kwa upande wake aliishukuru benki hiyo kwa msaada huo mkubwa na kuahidi kuvitunza vyema vitanda hivyo ili vidumu kwa muda mrefu na kuwa wao kama serikali wataendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa benki hiyo na kuwaomba kwamba wasichoke kuwasaidia kwani bado mahitaji ni makubwa

Mkuu wa shule hiyo ya Wasichana Kalambo Sister stela Kayobola aliishukuru benki hiyo ya NMB kwa msaada huo kwani ukosefu wa vitanda ulikua unapelekea baadhi ya wanafunzi wanaotoka katika mazingira magumu kushindwa kuripoti shule kwa wakati kwa sababu ya wazazi wao kushundwa kuwanunulia magodoro lakini sasa hari ni shwari

Awali mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya Kalambo Shafii Mpenda alidai kuwa NMB imekua ni moja ya Benki rafiki kwao na kuwa mahusiano haya yaliyopo watayalinda na kuwa wao watawahamasisha Wananchi kuhakikisha wanazitumia bidhaa za benki hiyo katika kujiletea maendeleo.

Na aliitaka benki hiyo kutochoka kushirikiana nao katika changamoto mbalimbali walizonazo kama hiyo ya vitanda na kuwa wataendelea kuwashikirikisha kila jambo wanaloliona kuwa linaweza kutatuliwa na NMB kulingana na wakati husika.
Mwisho