Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya
BENKI ya NMB kupitia Kanda ya Nyanda za Juu imetoa msaada wa shilingi milioni 30 kusaidia maandalizi ya Wiki ya Vijana Kitaifa na kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru, kinachotarajiwa kufanyika jijini Mbeya.
Akikabidhi hundi hiyo Oktoba 6,2025 kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa, Meneja wa Kanda ya Nyanda za Juu wa NMB, Wogofya Mfaramagoha amesema benki hiyo ni mdau mkubwa wa maendeleo na imekuwa ikishirikiana na serikali katika shughuli mbalimbali muhimu za kijamii.
“Kwa miaka mitano iliyopita, NMB tumetoa udhamini wa zaidi ya shilingi milioni 439 kwa shughuli mbalimbali. Mwaka huu tumejitolea milioni 30 kusaidia kuratibu kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru,” amesema Mfaramagoha.
Ameongeza kuwa Mbio za Mwenge wa Uhuru zina umuhimu wa kihistoria nchini, hasa mwaka huu ambao unaadhimisha miaka 61, tangu kuanzishwa kwake na miaka 29 tangu kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Pia amesisitiza kuwa vijana wana jukumu kubwa kuenzi falsafa za Mwalimu kwa kudumisha mshikamano na kuchochea maendeleo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa aliipongeza NMB kwa kuwa mdau wa kweli wa maendeleo, akiitaka benki hiyo kuendeleza juhudi zake za kutoa elimu ya kifedha kwa jamii ili kuondoa imani potofu kuhusu usalama wa fedha.
“Tunawashukuru kwa mchango huu muhimu. NMB imekuwa mfano wa kuigwa kwa mashirika binafsi yanayosaidia juhudi za serikali,” amesema Malisa.
Kilele cha mbio hizo na wiki ya Vijana Kitaifa kinatarajiwa kuwa tukio kubwa lenye kuunganisha vijana kutoka mikoa mbalimbali nchini.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi