Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
BENKI ya NMB imeingia makubaliano rasmi (MoU) na Chama cha Wanawake Wamiliki wa Shule na Vyuo Tanzania (TAWOSCO), yaliyosainiwa sambamba na uzinduzi wa ‘NMB School Proposition, lengo likiwa ni kuwawezesha kupata mikopo yenye riba nafuu kwa maendeleo ya taasisi zao.
MoU hiyo imesainiwa na Afisa Mkuu wa Fedha wa NMB, Bw. Juma Kimori na Katibu Mkuu wa TAWOSCO, Bi. Aisha Mzee, mbele ya Katibu Mkuu wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng’i Issa, wakishuhudiwa pia na Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi.
Makubaliano hayo yanaleta sokoni Akaunti Maalum isiyo na Makato ya Mwezi kwa ajili ya kukusanya ada na michango mingine, Huduma ya Flex Malipo kuwezesha kukusanya malipo kupitia ‘Control Number’ na AdaBima ya kumwezesha mzazi anapopata ulemavu wa kudumu au kifo.
Akizungumza wakati wa kusaini makubaliano hayo, Bw. Kimori alisema MoU hiyo itawezesha upatikanajiwa Huduma za Wakala, Lipa Mkononi (Lipa Namba na QR), pamoja na Mashine za POS mashuleni, ambako kutakuwa na Bima za Magari, Maisha na Majengo ya Shule na mikopo mbalimbali.
Bw. Kimori alibainisha kuwa kwa kutambua kuwa Elimu Msingi Bora wa Maisha kwa Mtanzania na kwa kuthamini kazi kubwa inayofanywa na wanawake wanaomiliki shule na vyuo nchini, dhamira ya kusapoti jitihada hizo imewasukuma kusaini makubaliano hayo muhimu kwa afya ya elimu nchini.
“Mwenyekiti (wa TAWOSCO) ametuambia kaulimbiu yenu kama chama ni ‘Mwanamke Muumbaji wa Maadili,’ hili ni jambo kubwa sana, kwa sababu maadili ni jambo la lazima na tutambua kuwa shule ama chuo kikimilikwa na mwanamama, maadili mema yatakuwa kipaumbele kikuu.
“Leo hii tunasaini MoU hii tukitambua kazi kubwa iliyofanyika baina ya pande mbili hizi yaani NMB na TAWOSCO, huu mkataba unakuja na masuluhiso tele, ambayo yamejikita katika utatuzi wa changamoto na matatizo ya Sekta ya Elimu hasa shule na vyuo vya wanachama.
“Ni makubaliano yaliyobeba utatuzi wa matatizo mnayopitia wamiliki, wazazi, wanafunzi wa shule na vyo vyenu, na wadau wote, changamoto za kifedha, za mikopo, bima, ada na kadhalika, kwa hiyo mkataba huu ‘package’ iliyokamilika
“Tutatambua katika maisha, mzazi anaweza kupata ulemavu ama kifo, AdaBima iko ndani ya masuluhisho haya, lakini pia tunatambua kuwa TAWOSCO inazo taratibu za makusanyo ya michango ya wanachama, NMB imekuja na masuluhisho ya michango hiyo ya vikundi,” alibainisha Bw. Kimori.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu NEEC, Beng’i Issa ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo alizipongeza NMB na TAWOSCO kwa kusaini makubaliano hayo aliyoyataja kama mkombozi wa sekta ya elimu na wamiliki wa shule na vyuo, ambao wanakabiliwa na changamoto nyingi za kifedha.
“Kuendesha taasisi za elimu kunahitaji nguvu kubwa ya kiuchumi kuweza kupata majengo, vifaa vya kuanzia biashara bila faida kwa muda mrefu, hadi kuanza kupata faida. Nawapongeza kwa sababu taasisi nyingi za kifedha zilikuwa zinakwepa kukopesha wamiliki wa shule na vyuo.
“Tatizo la fedha limekuwa kubwa sana kwenye sekta ya elimu, hasa katika shule binafsi, hawana mahali pa kupata mitaji ya kutosha kukidhi mahitaji yao, lakini naamini TAWOSCO ni taasisi nzuri kufanya nayo kazi, kwani inahusisha wanawake ambao ni kundi adilifu katika masuala ya fedha, hukopa kwa malengo na hurejesha kwa wakati.
“Leo mnaingia makubaliano na NMB, benki kwa kawaida na nadhani imeelezwa hapa kwamba watakuja kuangalia usajili wa taasisi zenu, wataangalia uzoefu wako umefanya kazi kwa miaka mingapi, wataangalia rekodi za mapato na matumizi na masuala mengine kama hayo.
“Hiyo ndio itaiwezesha benki kujua mzunguko wako wa fedha ambao ndio msingi wa ukopeshwaji, watajua uwezo wako wa kukopa na faida wanayoweza kupata kwako, kwahiyo kumbukumbu, kuweka sawa mahesabu na kukaguliwa na wakaguzi wanaotambulika ni muhimu sana,” alisisitiza Beng’i Issa.
Naye Bi. Aisha Mzee ambaye ni Katibu Mkuu wa TAWOSCO, aliishukuru NMB kwa kukubali kufanya kazi na taasisi yake, aliyosema ni moja tu kati ya taasisi nyingi ambazo NMB ingeweza kuzichagua kufanya nazo kazi, na kuwa uamuzi wa kuwachagua wao, umetuheshimisha sana.
“Kwa niaba ya wanachama wa TAWOSCO, nichukue nafasi hii kuwahakikishia NMB kwamba wanapokuwepo wanawake walio chini ya mwamvuli huu, haangushwi mtu, hapa hakitaharibika kitu.
“Tumepokea heshima zote alizotupa Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, uwingi wetu huu unaojumuisha wanawake kutoka mikoa mbalimbali nchini, unathibitisha namna wanavyothamini heshima waliyopewa na NMB.
“Tunawashukuru Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenri na wafanyakazi wa NMB kwa hili, Mungu awabariki sana wote, tunaamini huko tuendako mtatupa kipaumbele wanawake ambao ndio kitovu cha maadili.
“Wito wangu kwa wanachama TAWOSCO ni kuheshimu masharti ya mikopo, raha ya mkopo ni kukopa kwa malengo na kurejesha kwa wakati. Nami nachukua dhamana kwa niaba ya wanachama hawa, nawahakikishia NMB kwamba tutasimamia uchukuaji na urejeshaji wa mikopo,” alisisitiza Bi. Aisha.
More Stories
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best
Waziri Mavunde:Benki Kuu yanunua tani 2.6 za Dhahabu nchini
Kampeni msaada wa kisheria ya mama Samia kutatua kero za kisheria Katavi