January 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NMB inakopesha hadi bil. 340

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Tanga

NMB imejinasibu kuwa ina uwezo wa kukopesha wawekezaji wakubwa na wa kati hadi bilioni 340, ikiwa ni kiwango cha juu kwa mkopaji mmoja na hiyo kuwa chachu kwa wawekezaji kufanya shughuli zao kwa tija nchini.

Hayo yamesemwa na Meneja wa NMB Kanda ya Kaskazini Baraka Ladislaus kwenye Kongamano la Uwekezaji, Biashara na Utalii sambamba na uzinduzi wa Mwongozo wa Uwekezaji Mkoa wa Tanga, huku kauli mbiu ikiwa ni ‘Wekeza Tanga kwa uwekezaji endelevu’ linalofanyika jijini humo kwa siku mbili Novemba 16- 17, 2023.

Meneja wa NMB Kanda ya Kaskazini Baraka Ladislaus akizungumza kwenye Kongamano la Uwekezaji

“NMB tunajivunia uwezo wetu wa kutoa suluhisho mbalimbali za kifedha kwa wawekezaji,moja ya nguvu zetu kuu ni uwezo wetu wa kutoa mikopo ya biashara ndogo na za kati (SMEs),tumekuwa na uzoefu mkubwa katika kuunga mkono biashara zao,kuwawezesha kukua na kufanikisha ndoto zao katika ujasiriamali,”ameeleza

Ameeleza kuwa imani yao ni kuwa SMEs ni nguzo muhimu katika uchumi wowote na kwa kuwapa msaada wa kifedha unaohitajika NMB inachangia ukuaji wa uchumi na kukuza mazingira mazuri ya uwekezaji.

“Kwa sasa NMB inaweza kukopesha mpaka bilioni 340 kwa mkopaji mmoja, uwezo ambao naamini kwa wawekezaji unaweza ukawa chachu kubwa sana ya kuona ni sababu gani uendelee kuwa mwekezaji katika Mkoa wetu wa Tanga” amesema Ladislaus.

Sehemu ya washiriki kwenye Kongamano la Uwekezaji Mkoa wa Tanga

Ladislaus amesema wakielewa umuhimu wa kuendesha mfumo wa ukopeshaji kwa uwajibikaji benki hiyo inazingatia kikamilifu mwongozo wa kiwango cha juu cha kukopesha mkopaji mmoja (SBL) uliowekwa na mamlaka za udhibiti.

Kiwango walichoweka kimezingatia taratibu na wanaamini kinakidhi na wakati huo huo wakiwapa wawekezaji ushirika salama na wa kuaminika.

Pia inatambua umuhimu wa ukaribu wa upatikanaji wa huduma kwa wawekezaji ambapo kwa Mkoa wa Tanga wana jumla ya matawi 12.

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga Mhandisi Mwanaisha Ulenge (katikati) ni mmoja wa washiriki kwenye Kongamano la Uwekezaji Mkoa wa Tanga

“Uwepo wetu wa matawi unaeneza usawa wa kifedha, unapunguza pengo la kijiografia na kuhakikisha kuwa hakuna mjasiriamali au fursa ya uwekezaji inapotezwa utayari wetu wa siku zote katika jukumu kubwa la kuchochea ukuaji wa kiuchumi kwa kushirikiana na watu wenye maono kama ninyi, tunaweza kuunda mfumo imara wa uwekezaji, ambapo ndoto zinabadilika kuwa ukweli na ustawi unakua kwa wote,” amesema Ladislaus.