January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Nkasi yajipanga kukusanya mapato 

Na Israel Mwaisaka, Timesmajira Online,Nkasi

Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi,imefanikiwa kuvuka lengo kwa kukusanya asilimia 32, ya mapato ya ndani katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha wa 2024/2025.Huku ikijipanga kukusanya mapato kwa ukamilifu.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi,Afraha Hassan,kwenye kikao cha Baraza la Madiwani cha kujadili taarifa za robo ya kwanza Kwa mwaka wa fedha wa 2024/25,baada ya kupokea taarifa za kwenye Kata.Ambapo Madiwani katika taarifa zao walijikita kutoa taarifa za makusanyo katika kata zao  kipindi cha miezi mitatu iliyopita.

Amesema kuwa amekaa na Watendaji wote wa Kata na kuwekeana mikakati ya kuhakikisha mapato yanakusanywa.Hatakua na huruma kwa mtu yeyote atakayezembea katika eneo hilo na  katika kufanikisha hilo ofisi yake itahakikisha madai yao yote yanalipwa kwa wakati,na zoezi hilo limekwisha anza.

Hata hivyo,Madiwani wa Baraza hilo,walisisitiza suala la makusanyo ya ndani na kumtaka Mkurugenzi Mtendaji  awe mkali kwa Watendaji wake, katika suala zima la makusanyo na kuomba iwepo motisha kwa Watendaji wanaokusanya vizuri mapato.

Diwani wa Kata ya Chala,Michael Mwanalinze, amedai kuwa mipango yote ya maendeleo katika Wilaya hiyo,itekelezeke inahitaji fedha, ambapo aliwaomba Madiwani wenzie kuwa sambamba na Watendaji wao katika suala zima la ukusanyaji wa mapato.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo,Pankrasi Maliyatabu,amemtaka kila mmoja kuwajibika ipasavyo katika nafasi yake huku Watendaji wa Kata wakipewa jukumu la kuhakikisha mapato hayapotei.

Pia aliwataka Watendaji wa Kata,kuwasimamia viongozi wa vijiji katika maeneo yao,kwa  kuwasomea Wananchi mapato na matumizi
ili kuondoa manung’uniko.