November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Nkasi kuchanja zaidi ya mabinti 30,000 chanjo ya HPV

Na Israel Mwaisaka, Timesmajira Online,Rukwa

WILAYA ya Nkasi mkoani Rukwa inatarajia kuwachanja watoto wa kike wapatao 32,168 chanjo ya kuwakinga wasichana dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi ili kukabiliana ugonjwa huo.

Akizindua chanjo hiyo katika shule ya msingi ya Isunta Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Nkasi na ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Razaro Komba amewataka wanananchi kuhamasika na kuhakikisha watoto wao wote waliofikisha umri wa miaka 9 hadi 14 wanapata chanjo hiyo.

Amedai kuwa zoezi hilo ambalo litadumu kwa muda wa siku 5 litakua na maana kama walengwa wote wataipata chanjo hiyo ili kuweza kukabiliana na ugonjwa huo wa saratani ya mlango wa kizazi ambao kwa sasa umekuwa ni tatizo na umeleta athari katika jamii.

Mkuu huyo wa wilaya amefafanua kuwa chanjo hiyo imeanza kutolewa toka mwaka 2014 mkoani Kilimanjaro na mpaka sasa imedumu kwa muda wa miaka 8 na serikali imeendelea kuitoa kutokana na changamoto wanayoipata wanawake hasa pale wanapokumbwa na ugonjwa huo.

Hivyo amewataka viongozi kuanzia ngazi ya kitongoji kuhakikisha kuwanatoa hamasa ya kutosha kwa watu wanaowaongoza kuhakikisha watoto wao wote wanapata chanjo hiyo.

Awali Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hiyo Ladislaus Mzelela amesema kuwa licha ya chanjo hiyo kutolewa katika shule zote lakini pia vituo 59 vimeandaliwa kwa ajili ya kutolea chanjo hiyo ya HPV katika Wilaya Nkasi.

Amedai kuwa ana uhakika kuwa watu wengi watajitokeza kupeleka watoto wao ili kuweza kupata chanjo hiyo kutokana na hamasa kubwa ambayo imeendelea kutolewa katika maeneo mbalimbali wilayani Nkasi.

Diwani wa Kata ya Isunta Aizeck Chambula amesema kuwa ugonjwa wa saratani ya shingo ya uzazi unajulikana katika jamii na wengi wamewapoteza ndugu zao kutokana na ugonjwa huo na kuwa atashangaa kama watu hao watashindwa kuwapeleka watoto wao kwenye chanjo hiyo.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Isunta Chrispini Wikula alimuhakikishia Mkuu wa Wilaya kuwa wao kama viongozi watahakikisha watu wote katika maeneo yao wanawapeleka watoto wao wote kupata chanjo ili kuweza kuwaweka katika mazingira salama.

Baadhi ya wananchi waliohudhuria hafla hiyo ya uzinduzi wa chanjo hiyo ya HPV wamesema kwamba wao wanatambua umuhimu wa chanjo hiyo na madhara yatokanayo na ugonjwa huo hivyo hawaoni sababu ya kutowapeleka watoto wao kwenda kupata chanjo hiyo.