March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Njama amshukuru Rais Samia fedha za ukarabati Hospitali ya Magunga

Na Yusuph Mussa, TimesmajiraOnline,Korogwe

MBUNGE wa Jimbo la Korogwe Mjini mkoani Tanga CPA Charles Njama amemshukuru Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan baada ya kutoa sh. bilioni moja kwa ajili ya ukarabati wa majengo ya Hospitali ya Wilaya ya Korogwe, Magunga pamoja na kujenga Maternity Complex.

Hata hivyo, ameomba badala ya kufanyia ukarabati hospitali hiyo ambayo ilianzishwa mwaka 1952 huku kwa sasa ikiwa na umri wa miaka 73, majengo yake mengi ni chakavu, hivyo Serikali iwape fedha ili waweze kujenga majengo mapya kabisa kwenye kila idara.

Ameyasema hayo Februari 14, 2026 mbele ya Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba alipofika Korogwe kukagua Mradi wa Maji wa Miji 28 mkoani Tanga kwenye Kata ya Mswaha- Darajani.

“Tunamshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, kwani ametupatia sh. bilioni 1.06 kwa ajili ya ukarabati wa hospitali yetu ya Magunga. Naomba kidogo nitoe historia ya Hospitali ya Magunga. Hospitali yetu ya Magunga imejengwa mwaka 1952, hivyo ina umri wa miaka 73 kwa sasa, ile hospitali ni kongwe mno, na ukienda miundombinu ilivyo, haiendani kabisa na mji wetu wa Korogwe kwa sasa.

“Tumepata sh. bilioni 1.06, na tumeambiwa tukajenge Maternity Complex. Tunashukuru sana sababu huduma za akina mama hususani kwenye uzazi zote zitakuwa coverd (zitapatikana). Maombi yetu kwako, gharama ya ukarabati wa majengo yale ni kubwa mno, na hatuwezi kupata tija kubwa kwa kupitia ukarabati. Tunakuomba Waziri Mkuu, badala ya kufanya ukarabati tuendelee kujenga majengo mapya kwa awamu hata kidogo kidogo ili baada ya muda tuwe na hospitali mpya iliyokamilika ya kisasa ambayo wananchi wetu watapata huduma bora, na tutaondokana na gharama ya ukarabati wa mara kwa mara” alisema CPA Njama.

CPA Njama pia aliiomba Serikali kuendelea na mchakato wa Bandari Kavu inayokusudia kujengwa hapa mjini Korogwe, kwani bandari hiyo itahuisha uchumi wa wananchi wa Korogwe kwa shughuli nyingi na fursa mbalimbali kufanyika.

“Waziri Mkuu, tuna ombi letu wananchi wa Jimbo la Korogwe, na hili hata Mkuu wa Mkoa wetu (Balozi Dkt. Batilda Burian) amelizungumzia. Wananchi wanataka kuona Bandari Kavu inajengwa. Na Bandari Kavu hii ina maana kubwa sana katika uchumi, katika ajira, na maendeleo ya jimbo letu la Korogwe Mjini. Lakini sio hivyo tu, bali inakwenda kupunguza msongamano wa malori katika barabara yetu ya Tanga kuja Segera.

“Lakini pia itakwenda ku-stimulate (kuchechemua) uchumi kwa maana ya wafanyabiashara wadogo wadogo, mamalishe na babalishe, wasafirishaji wa bodaboda, bajaj na wasafirishaji wengine watakwenda kunufaika na Bandari Kavu hiyo. Tunakuomba sana Waziri Mkuu, ikikupendeza, na hili nalo, twende tukalitekeleze kwani litakwenda kuleta historia kubwa kwa uchumi wa Korogwe” alisema CPA Njama.