December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Eudia Simoni (40),mkazi wa Mtaa wa Kolimba Kata Hombolo Bwawani Mkoa wa Dodoma

‘Nitapoteza maisha kwa ukosefu wa sh.laki 6’

Na Stella Aron

“NINAPATA maumivu makali sana, usiku sipati usingizi, nalia usiku na mchana na hali inazidi kubwa mbaya kila kukicha kwa ukosefu wa sh.600,000 ili nifanyiwe upasuaji wa ziwa hivyo nitapoteza maisha kutokana na umaskini wangu, nawamba Watanzania wanisaidie”

Eudia Simoni (40),mkazi wa Mtaa wa Kolimba Kata Hombolo Bwawani Mkoa wa Dodoma

Hiyo ni kauli ya Eudia Simoni Mlewa (40),mkulima,mkazi wa Mtaa wa Kolimba Kata ya Hombolo bwawani Mkoa wa Dodoma ambaye alikuwa akizungumza na kwa shida na Majira.

Eudia anasema kuwa anakumbuka mwaka jana Desemba aliona kijipu kidogo kwenye ziwa la kushoto ambapo awali hakusikia maumivu hivyo hali hiyo aliendelea kusubiri ili kiive.

Anasema kuwa kutokana na hali hiyo haikuweza kumzuia kuendelea kufanyakazi zake zake za kilimo kutokana na kutosikia maumivu katika sehemu yoyote ya mwili.

Anasema kuwa kadri siku zinavyosonga mbele alishangaa jipu hilo likiendelea kukua kwa kasi na kusababisha kuanza kusikia maumivu.

“Mume wangu alianza kushangaa kutokana na jipu hilo kuendelea kuwa kubwa zaidi, niliingiwa na hofu ingawa niliendelea na kilimo ingawa maumivu hayakuwa makali,” anasema.

Eudia anasema kuwa ilipofika Januari mwaka huu alianza kupata maumivu makali yaliyopelekea jipu hilo kupasuka ambapo usaha mwingi ulitoka na kuonekana kuwepo kwa shimo kubwa ambapo alilazimika kwenda Kituo cha Afya Hombolo.

“Baada ya kufika hospitali na daktari kunichunguza alinishauri kwenda Hospitali ya Mkoa kwa ajili ya uchunguzi zaidi na hapo nilipewa dawa ya kutuliza maumivu tu kwani maumivu yaliendelea kwa kasi kubwa,’ anasema.

Anasema kuwa daktari alimuandikia barua ya kwenda kuonana na madaktari katika Hospitali ya Mkoa Dodoma ambako kulikuwa na vipomo vingi na pia madaktari wengi.

“Baada ya kuonana na madaktari katika hospitali hiyo nao pia walitushauri Kituo cha Dayososi Matei kwa ajili ya kupima saratani ambapo baada ya vipimo walitueleza kuwa majibu yangetoka baada ya wiki mbili baada ya vipimo kupeleka Hospitali ya Muhimbili,” anasema.

Anasema kuwa maumivu makali yalizidi kuwa makali huku akiendelea kumeza dawa za kutuliza maumivu huku kidonda kikiendelea kuongezeka.

“Maumivu ni makali sana kwani nashindwa hata kulala si mchana wala usiku na hali yangu inazidi kuwa mbaya na sielewi mwisho wake,’ anasema kwa uchungu.

Anasema kuwa walipokwenda kuchukua majibu Mei 5,mwaka huu,ndipo alipobainika kuwa ana dalili ya saratani ya titi hivyo anatakiwa kufanyiwa upasuaji ambapo gharama yake ni sh.600,000.

“Tangu nilipopewa majibu hadi sasa hatujaweza kupata kiasi hicho hivyo na maumivu ni makali sana nawaomba Watanzania wenzangu au wadau mbalimbali pamoja na Serikalai wanisaidie ili nifanyiwe upasuaji vinginevyo nitapoteza maisha kwa ukosefu wa kiasi hicho na familia yangu haina uwezo wa kupata fedha hizo,” anasema.

MUME AZUNGUMZA

Dickson Mganga Luaha ni mume wa mgonjwa huyo ambapo anasema kuwa anapata wakati mgumu sana namna ya kupata fedha hizo huku hali ya mkewe ikizidi kuwa mbaya.

“Ninamuonea huruma sana mke wangu lakini pia tumefanya jitihaza za kutafuta hizo pesa tangu Mei mwaka huu kwa kuuza chakula chetu cha akiba ndani kiasi kwamba hata akiba ya chakula hakuna lakini bado fedha hazijatimia na chakula hatuna tena,” anasema.

Anasema kuwa wamefanya kila wameomba msaada kwa familia na majirani lakini hawakuweza kufanikiwa na kulazimika kwenda kijijini kwa mama mkwe ambaye pia hakuwa na akiba hivyo walilazimika kurudi tena nyumbani kwao ili watafute njia nyingine ya kupata pesa.

“Nina watoto sita wa kwanza ana miaka 18 na mwisho ana miaka 4 wote wanatugemea cha kusikitisha akiba ya chakula tumeuza ili mama yao apate pesa ya kufanyiwa upasuaji sielewi mwisho wake utakuwa hata hivyo tunawashukuru majirani wamekuwa msaada kwetu,’ anasema.

DIWANI VITI MAALUM

Mgombea udiwani wa viti maalumu kupitia CCM Editha Luhamo anawaomba wadau, wananchi na Serikali kwa ujumla kumchangia mgonjwa huyo ili afanyiwe upasuaji kwani kidonda alichonacho ni kikubwa.

“Mimi nikwenda kumuona na nikatoa msaada lakini bado hautoshi anahitajika kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji kwani amebainika ana saratani ya ziwa na familia hiyo haina uwezo kama mwanamke mwenzangu kwa kweli nimesikitisa sana namna anavyougulia,” anasema.

Editha anasema kuwa familia hiyo inahitaji msaada kwani hata wakina ya chakula waliyoa nayo wameuza ili wafanikishe matibabu jambo ambalo halijafanikiwa na

Anasema kuwa taarifa za kuumwa kwa kwake alizikia kwenye spika za matangazo ya Kanisa la Anglikana wakiomba wananchi kumchangia mgonjwa huyo ili afanyiwe upasuaji kwani anahitaji msaada mkubwa,” anasema,

MJUMBE WA NYUMBA KUMI

Laulend Sangaya ni mjumbe wa nyumba kumi anasema kuwa mgonjwa huyo yupo katika mtaa wake wa Kolimba hata hivyo kumekuwa na jitihada za kumsaidia kutokana na michango inayoendelea.

“Huyu mgonjwa namfahamu na tayari wanajiji wameanza kumchangia kiasi chochote ambacho mtu anachotaka hata hivyo kiwango cha ukusanyaji si cha kuridhisha, tunaomba kwa wasamaria wema wamsaidie na familia hiyo haina uwezo wa kutafuta sh.600,000” anasema.

Anasema kuwa kumekuwa na kundi la vijana wanaopita kila nyumba kuomba msaada kwa wanavijiji ili kufanikisha gharama hiyo.

Kwa mujibu takwimu za kiulimwengu zinaonesha kuwa katika kila watu watano mmoja atapatikana na saratani kabla ya kufikia umri wa miaka 75, na ushamiri wa saratani unaongezeka kadri tunavyozidi kuishi umri mrefu na magonjwa yanabadili kawaida zake.

Saratani ya matiti imekuwa ugonjwa tishio kwa wanawake. Wataalamu wanaitaja kama saratani hatari zaidi ikiongoza kusababisha vifo kwa wanawake kuliko saratani nyingine zote.

MAJIRANI WANENA

Baadhi ya majirani waliozungumza na Majira wameelezea namna mwanamke huyo anavyopata shida kutokana na maumivu makali anayopata na kulazimika kuanza kuchangishana ili jirani mwenzano apate matibabu.

Mmoja wa majira aliyejitambulisha kwa jina la Mama Helena anasema kuwa wamemua kwa moyo mmoja kila mmoja kuchangia kiasi chochote kwani watoto wake wanapata shida sana na wanakosa huduma za mama.