Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online, Dar
CHUO cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kimezindua rasmi Kamati ya Ushauri ya wadau wa kisekta kitakachofanya kazi na Kituo cha Umahiri cha Mafunzo ya Taaluma za Usafiri wa Anga na Operesheni za Usafirishaji.
Kituo hicho ni cha kihistoria, kwani ni mara ya kwanza kuwa kituo cha Umahiri cha Mafunzo ya Taaluma za Anga na Operesheni za Usafirishaji kuanzishwa katika historia ya nchi yetu.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkuu wa Chuo hicho Mhandisi Profesa Zacharia Mganilwa amesema;
“Kwa namna ya pekee niwashukuru Benki ya Dunia kwa kufadhili Kituo chetu cha umahiri ambayo ni muhimu sana kwa ustawi wa sekta ya uchukuzi na sekta ndogo ya Usafiri wa Anga.”
Ameongezea kuwa ili kuimarisha mahusiano ya vyuo na wadau wa sekta pamoja na kuhakikisha kuwa mafunzo yatolewayo na kituo yanakidhi mahitaji ya soko, Benki ya Dunia ilielekeza vituo vyote vya umahiri kuwa na Kamati ya Ushauri wa Wadau wa Kisekta.
”Kamati hii imeundwa na wajumbe kutoka sektambali mbali waliobobea katika njia kuu za usafirishaji yaani usafiri wa anga, reli, maji na barabara. Hii itasaidia sana katika kukishauri Chuo namna bora ya kuendesha Kituo hiki cha Umahiri,” amesema.
Prof Mganilwa alisema kuwa kamati hiyo imezingatia mahitaji ya sekta binafsi ambapo asilimia 50 ya wajumbe wa kamati hii wanatoka kwenye sekta binafsi.
”Majukumu ya kamati hii ni pamoja na kutoa mapendekezo na ushauri utakaosaidia Kituo cha Umahiri kukidhi mahitaji ya elimu bora ya ufundi hapa nchini na nje ya nchi,” amesema.
Ameongezea, “Kamati itaweza vile vile kukisaidia Kituo kujua mwelekeo na mwenendo wa soko la ajira katika sekta ya Usafirishaji kwa kuzingatia mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia.”
Amesema kuwa Kamati hiyo itaweza kukishauri Kituo namna bora ya kuzalisha wahitimu wenye ustadi, weledi na ufanisi ili kuendana na hitaji la soko la ajira; na Kukisaidia Chuo kuwa mahusiano ya karibu na wadau wa kisekta ili wanafunzi na wakufunzi waweze kupata nafasi za kufanya mazoezi viwandani.
“Vile vile kamati itaweza kukisaidia Kituo cha Umahiri kuboresha mitaala kwa kutoa taarifa ya mahitaji halisi ya soko pamoja na Kuunganisha Chuo na sekta kwa ajili ya kufungua fursa za kuboresha mafunzo ya Kituo cha Umahiri kwa kubadilishana wakufunzi, ujuzi, na vifaa vya mafunzo,” amesema.
Kupitia mradi huu wa EASTRIP, Chuo cha Taifa cha Usafirishaji kitapatajumla fedha za Kimarekani dola milioni 21,250,000 sawa na sh. sh bilioni 49,053,500,000 kwa ajili ya kuanzisha kituo hiki cha Umahiri cha Mafunzo ya Taaluma za Anga na Operesheni za Usafirishaji.
Aidha kituo hicho cha umahiri cha mafunzo ya Taaluma za Anga na Operesheni za Usafirishaji ni cha kipekee katika mradi wa EASTRIP na katika nchi yetu ya Tanzania chenye malengo ya kupunguza uhaba wa wataalam katika sekta ya usafiri wa anga na operesheni za usafirishaji ndani na nje ya Tanzania.
”Chuo kupitia ufadhili huu kitafanikisha malengo ya Taifa ya kuzalisha wataalum wazawa kwenye fani za urubani, uhandisi wa ndege, operesheni na menejimenti katika njia kuu za usafirishaji na uchukuzi, jambo ambalo limekuwa kilio cha muda mrefu kwa Taifa letu. Aidha, miundombinu ya kujifunzia na kufundishia itakayoimarishwa itakisaidia Chuo kutoa mafunzo bora na kuwafikia wadau wengi kwa urahisi,” Mkuu wa Chuo ameongezea.
Mkuu huyo wa Chuo amesema kuwa fedha zitakazopokelewa na NIT kupitia mradi huu wa EASTRIP zimelenga kufanikisha malengo mbali mbali.
“Moja ya malengo yatakayofanikishwa na mradi huu wa ESTRIP ni pamoja na kuboresha utawala na menejimenti katika kutoa mafunzo kama Kituo cha Umahiri; kuimarisha mahusiano kati ya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji na wadau mbalimbali wa sekta ya anga na operesheni za usafirishaji,” amesema.
“Tutaweza vile vile Kutoa udhamini (scholarships) kwa wanafunzi wasichana ili kuwawezesha kusoma na kubobea katika taaluma za anga na logistiki; Kuboresha na kutengeneza mitaala inayokidhi mahitaji ya soko la ndani na la kimataifa.” amesema.
Ametabanaisha kuwa kituo kitaweza kutoa wahitimu wa mafunzo ya taaluma za anga na operesheni za usafirishaji zaidi ya 4,000 katika kipindi cha miaka mitano ya mradi pamoja na kuongezea uwezo wa waalimu kupitia mafunzo ya shahada za uzamili, mafunzo ya muda mfupi (professional training) na mafunzo ya vitendo (industrial attachments).
“Katika mradi huu tutaweza kuboresha miundombinu kwa kujenga majengo tisa ya Kituo chetu cha Umahiri ikiwemo jengo la Kituo cha Umahiri (Mabibo), jengo la mock up (Mabibo), jengo la mafunzo ya ufundi (Mabibo), hostel mbili zenye kubeba wanafunzi 2100 (Mabibo), hanga ya ndege (Dar es Salaam), hanga ya ndege (Kilimanjaro), makazi ya wafanyakazi (Kilimanjaro) na makazi ya wanafunzi (Kilimanjaro),” amesema.
“Pamoja na hayo tutaboresha vifaa vya mafunzo na vitendea kazi kwa kununua ndege tatu, simulator mbili za ndege, Cabin Crew Mock Ups, vifaa vya TEHAMA kwa ajili ya mafunzo, vifaa maalum ya mafunzo ya uhandisi wa ndege na magari manne ya mradi,” amesema.
Chuo kilipokea awamu ya kwanza ya fedha za mradi sawa na asilimia 30 ya fedha zote za mradi wa Kituo cha Umahiri hapa Chuo cha Taifa cha Usafrisihaji kwa ajili ya utekelzaji wa mradi mwishoni mwa Machi, 2020.
More Stories
CCM hakuna kulala, Nchimbi atua Tabora kwa ziara ya siku mbili
Kongamano la Uwekezaji na Biashara lafunguliwa Pwani
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi