December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NIT yaingia mkataba na wakandarasi kujenga majengo ya chuo.

Na Penina Malundo,Timesmajira,Online

CHUO cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kimeingia mkataba na wakandarasi kujenga majengo  matano ya Chuo hicho ambao ni sehemu ya mradi wenye thamani ya Bilioni 49 na unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo iliyofanyika Jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (Elimu) Prof. Carolyne Nombo amesema Serikali itasimamia mradi huo mpaka kuhakikisha malengo yanafikiwa.
“Kwa wakandarasi ninawaomba mfanye kazi kwa bidii na uweledi ili kuhakikisha kuwa mradi unakamilika kwa muda uliopangwa yaani miezi 12.” Amesema

Amesema wakandarasi hao wataweza kujenga majengo bora kulingana na thamani yake pia kukabidhi majengo hayo kwa muda wa makubaliano kwenye mkataba.
Amesema majengo hayo ni muhimu kwa ustawi wa mafunzo yanayotolewa na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji na kuomba ujenzi uanze kwa kasi huku wakizingatia taratibu zote za kisheria na za kiufundi ili kukamilisha kazi hiyo kwa ubora na kwa muda mfupi inavyotarajiwa”
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Zacharia Mganilwa amesema mkataba wa ujenzi uliosainiwa unathamani ya shilingi Bilioni 21 ambapo ujenzi huo huo utafanywa kwa mwaka mmoja.
Amesema chuo hicho kimeanzisha kituo cha umahiri katika taaluma ya anga na masuala yote ya usafirishaji ambapo tayari NIT imefika asilimia 75 ya utekelezaji.