Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online, Dar
SERIKALI ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais John Magufuli, imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya uchukuzi na usafirishaji na hakuna aliyeamini kama haya yanayoonekana machoni mwa Watanzania, yangeweza kufanyika ndani ya miaka mitano.
Mfano, miongoni mwa mageuzi makubwa ambayo Serikali hiyo imefanya ni pamoja na kupokea ndege mpya nane kati ya 11 zilizonunuliwa. Mageuzi mengine ni ujenzi na upanuzi wa viwanja mbalimbali vya ndege nchi nzima.
Pamoja na ununuzi wa ndege, upanuzi wa viwanja vya ndege,ujenzi wa viwanja vipya kama vile Uwanja wa Chato, upanuzi wa majengo ya abiria kwenye viwanja vya ndege, Serikali ina mikakati ya ujenzi wa viwanja vingine vya ndege kikiwemo cha Msarato mkoani Dodoma.
Kasi hiyo ya Serikali imekifanya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kuanzisha mitaala mbalimba ili pamoja na mambo mengine kukidhi malengo ya Serikali kwa kuzalisha wataalam wa sekta ya anga watakaokuwa tegemeo ndani na nje ya nchi.
Mfano, juzi NIT imezindua mafunzo ya kozi fupi ya madereva mahiri watakaohudumia katika viwanja vya ndege.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo jijini Dar es Salaam juzi, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) Meneja wa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Paulo Rwegasha alisema kuwa mafunzo hayo ni muhimu sana katika kuboresha utoaji wa huduma za usafiri wa anga hapa nchini.
Ametoa wito kwa washiriki wa mafunzo hayo na Watanzania wote watakaopata fursa ya kushiriki kuwa mabalozi wazuri na kutumia ujuzi wao kwa uaminifu na uadilifu katika kulinda rasilimali ikiwemo ya miundombinu ya usafiri wa anga ambapo Watanzania kupitia kodi zao wamewekeza ili kuchangia maendeleo yaTaifa.
Amesema kuwa katika kuhakikisha mafunzo yanakuwa endelevu na kutolewa kwa viwango stahiki, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege itashirikiana na Chuo kuhakikisha mafunzo hayo yanaleta tija kwa jamii na taifa nzima.
Ameupongeza uongozi wa chuo hicho kwa kuanzisha mafunzo hayo ambayo yanaendena na mipango ya Serikali ya awamu ya tano.
“Ni matumaini yangu kuwa wadau wa usafirishaji hasa kwenye maeneo ya viwanja vya ndege watatumia fursa hii kupata mafunzo hapa chuoni,”anasema.
Anasema kuwa amefurahi sana kuona Chuo kimeanzisha Kituo cha Umahiri cha Mafunzo ya Taaluma za Usafiri wa Anga na Operseheni za Usafirishaji (Centre of Excellence in Aviation and Transport Operation) ambacho kitasaidia na kuimarisha utoaji wa mafunzo mbalimbali kwenye sekta ya usafirshaji.
Kwa mujibu wa Meneja huyo, mafunzo hayo ni muhimu sana hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali ya Awamu ya Tano imewekeza sana kwenye sekta ya uchukuzi ikiwa ni pamoja na sekta ndogo ya usafiri wa anga.
00000000000000000
Akitoa mfano anasema hadi sasa tayari Serikali imeshapokea ndege mpya nane kati ya 11 zilizonunuliwa, ujenzi na upanuzi wa viwanja mbalimbali vya ndege nchi nzima.
Viwanja hivi ni pamoja na Ujenzi wa jengo jipya la abiria (Terminal III) katika kiwanja cha ndege cha Kimataifa Julius Nyerere, ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa Kilimanjaro na Msalato, ujenzi wa kiwanja cha ndege Mwanza, Songwe, Kigoma, Tabora, Shinyanga, Chato (Geita), Sumbawanga pamoja na Mtwara.
Anadokeza kuwa kukamilika kwa ujenzi wa miundombinu hii kutaongeza idadi na miruko ya ndege na huduma nyingine nyingi.
“Mafunzo haya ni muhimu sana katika kulinda miundombinu, kuimarisha na kuboresha utoaji wa huduma za usafiri wa anga hapa nchini,”anasema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa chuo hicho, Mhandisi Prof Blasius Nyichomba anasema kuwa ufunguzi wa mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mipango ya Chuo, sera mbalimbali za nchi pamoja na ushiriki wa Chuo katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi kama inavyoelekezwa kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025.
“Licha ya ukweli kwamba, Serikali imeendelea kufanya mapinduzi anuai katika sekta ya uchukuzi na safirishaji, ulimwengu wa biashara umekuwa na ushindani mkubwa sana,” anasema na kuongeza;
Mapinduzi haya na ushindani wa kibiashara vimeongeza uhitaji mkubwa wa rasilimali watu yenye weledi wa hali ya juu nchini na duniani kote.Ili kuendana na mapinduzi haya anuai, Chuo kimeweka mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuendelea kubuni kozi au mafunzo mbalimbali katika sekta ya uchukuzi na usafirishaji yenye maslahi mapana kwa Taifa.”
Mkuu wa NIT, Mhandisi Prof Zacharia Mganilwa anasema kuwa hayo ni mafunzo ya kihistoria kwani ni mara ya kwanza kuwa na mafunzo kama haya ya madereva wanaotoa huduma za usafiri kwenye viwanja vya ndege katika historia ya nchi.
Anasema hadi kuanza kwa mafunzo hayo ni matokeo ya juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia Chuo pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya usafirishaji na uchukuzi.
“Hivyo napenda kuwashukuru wadau wote kwa kazi nzuri walioifanya katika kuhakikisha mtaala wa mafunzo haya unakamilika kwa wakati na mafunzo yanaanza,” anasema .
Anabainisha kuwa chuo kina Idara ya Usalama katika Usafirishaji na Mafunzo ya Mazingira ambayo inasimamia utoaji wa mafunzo ya jumla ya kozi fupi 28 za usafiri na usafirishaji zikiwemo kozi za udereva mahiri, udereva wa mabasi, udereva wa magari makubwa ya mizigo pamoja na udereva wa kujihami.
Aidha,anasema kuzinduliwa kwa kozi hii kutafanya Chuo kuwa na jumla ya kozi fupi 29 chini ya Idara hiyo.
Anadokeza kuwa idadi ya washiriki wa mafunzo ya kozi fupi kwa ujumla imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka hivyo kupelekea ongezeko la madereva wenye weledi jambo ambalo linachangia kupunguza ajali barabarani.
“Hata hivyo, pamoja na ukweli huu, bado hapakuwa na mafunzo mahususi kwa watoa huduma maeneo ya viwanja vya ndege,”anasema Prof Mganilwa na kuongeza kwamba chuo kimeandaa mtaala utaotumika kufundishia madereva hao.
“Mafunzo haya ni muhmu sana kwani ili kuwa na usafiri wa anga endelevu na shindani tunahitaji mazingira salama ya kufanyiakazi pamoja na waendeshaji wenye weledi watakao toa huduma zenye viwango bora zaidi,” anasema.
Anasema kuwa Chuo kwa kutambua mchango mkubwa wa sekta ya usafirishaji katika kuchochea maendeleo ya nchi, kimeendelea kuimarisha na kusogeza huduma kwa jamii ili kurahisisha utoaji wa mafunzo.
“Chuo kimeanzisha Kituo Umahiri cha Mafunzo ya Taaluma za Anga na Operesheni za Usafirishaji (Center of Excellence in Aviation and Transport Operations – CEATO) kwa mkopo kutoka Benki ya Dunia,” anasema
Kwa mujibu wa Mkuu huyo, fedha hizo zitatumika kujenga madarasa, maabara, karakana pamoja na kununua vifaa vya mafunzo ikiwemo Cabin CrewMock Up, simulators na ndege kwa ajili ya mafunzo ya urubani.
Vilevile, anaongeza kwamba Chuo kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kina mpango wa kufungua Kituo mahiri cha Kikanda cha Mafunzo ya Usalama Barabarani (Regional Centre of Excellence in Road Safety) Jijini Dodoma.
“Kituo hiki kitasaidia kuimarisha miundombinu ya kujifunzia na kufundishia ambapo Chuo kitaweza kuwafikia wadau wengi zaidi na kwa urahisi,” anasema.
More Stories
Boost ilivyoboresha miundombinu ya elimu Ilemela
Samia apongeza walimu 5,000 kupatiwa mitungi ya gesi, majiko kutoka Oryx
Uwekezaji kwenye kilimo utatimiza ndoto ya Samia ya nchi kuwa ghala la chakula Afrika