March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NIC yaimarisha uhusiano na wateja Maonesho ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini Geita 2025

Na Mwandishi wetu,Geita

 MKURUGENZI  wa Masoko na Mawasiliano wa Shirika la Bima la Taifa (NIC) Karimu Meshack amefanya ziara ya kutembelea  mabanda ya wateja na washirika wake kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kibiashara, kusikiliza changamoto zao ili kutoa usuluhishi kwa wakati.

Wadau na washirika wa NIC waliofikiwa na Mkurugenzi huyo ni pamoja na Benki ya NMB, Benki ya Equity , Kampuni ya  Madini Bluecoast, Mfuko wa Pensheni (PSSSF), Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF),Mfuko wa Bima ya Afya wa Taifa ( NHIF), Kampuni ya Madini ya FEMA, na HEXAD Insurance Agency. 

Karimu amefanya ziara hiyo kwenye maonesho ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita katika viwanja vya Samia Suluhu Hassan Bombambili ambapo lengo ni   kuhakikisha huduma za NIC  zinawafikia wateja kwa karibu zaidi na kujibu mahitaji halisi ya wadau wa sekta ya madini.

 Aidha NIC ni miongoni mwa wadau wanaoshiriki kikamilifu maonyesho hayo ambayo yameanza Septemba 18,2025 na  kufunguliwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa yanatarajiwa kuhitimishwa kesho septemba 28,2025.

Akizungumza katika ziara yake hiyo Karimu amewashukuru  wateja wake  kwa kuendelea kutumia huduma za NIC, sambamba na kuendeleza uhusiano wa karibu unaojengwa katika msingi wa kuaminiana na kutatua changamoto kwa haraka.

Aidha amesema,ushiriki wa NIC katika maonyesho hayo ni nafasi ya kujifunza, kuelimisha na kushirikiana moja kwa moja na wateja na wadau wa kimkakati katika kuhakikisha kuwa huduma za bima zinawafikia wananchi wote kwa ufanisi na uwazi.

Amewakaribisha wadau na wananchi wote kwa ujumla  kutembelea banda la NIC, ili kupata elimu juu ya huduma mbalimbali za bima, kupata ushauri wa kitaalamu na kujiunga na huduma bora za bima kwa ajili ya maisha na biashara endelevu.