Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online, Dodoma
MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Bernard Konga amesema kitita cha mafao ya huduma za afya cha mfuko huo kina jumla ya dawa 975 na siyo kama inayodaiwa kupunguzwa kwa kitita hicho.
Konga ametoa kauli hiyo leo jijini hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu taarifa zinazosambaa mitandaoni kwamba kitita hicho kimepunguzwa kwa zaidi ya dawa 100 taarifa alizosema siyo sahihi.
Aidha amesema mfuko huo unaendelea na mawasiliano kuona namna gani ambavyo unaendelea kujumuisha dawa na kuona namna bora ya kuweza kutambua magonjwa na kutibu.
“Hivi sasa kuna zoezi linaendelea Serikalini la kuboresha muongozo wa kutoa matibabu ,sisi kama mfuko muongozo huo ukitolewa na Serikali tutaangalia dawa ambazo zimejuishwa na sisi pia tutazijumuisha lengo tusimfanye mteja wetu ajutie huduma zetu lakini kimsingi kitita chetu bado ni kipana na kina dawa nyingi” amesisitiza.
Ametumia fursa hiyo kuwataka watoa huduma wazingatie mikataba yao ili kuondoa sintofahamu kwa wateja wa mfuko huo.
“Watoa huduma waangalie mikataba yao inasemaje, tumeona haya yaliyojitokeza ,mtu kwenye taasisi yake ameandika ‘memo’ akaanza kusambaza ,lakini mtoa huduma akumbuke yeye ana mkataba na sisi kwa hiyo azingatie kilichopo kwenye mkataba” amesisitiza huku akisena
“Na kama kuna changamoto yoyote baina ya sisi na mtoa huduma ni vyema mtoa huduma akarudi kwetu na siyo vinginevyo ili kuondoa changamoto na sintofahamu zinazosababisha wateja kuondoa imani kwa mfuko wetu.”
Hata hivyo amesema hivi sasa mfuko utaanza kukaa karibu na watoa huduma ili kutoa ufafanuzi kwao na kwa wanachama kuhusu huduma za mfuko was NHIF.
“Tumepata picha halisi kwamba tunahitaji kukaa karibu na watoa huduma wetu ili kuweza kutoa ufafanuzi kwao na kwa wanachama wetu ili wasipate changamoto yoyote maana hatupendi kuwa chanzo cha changamoto na sintofahamu bali kutoa huduma stahiki.” amesisitiza.
Hivi karibuni kumekuwa na taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii kwamba NHIF imeondoa dawa zaidi ya 100 kwenye mfuko huo zikiwemo dawa za ‘presha’ jambo ambalo siyo kweli.
More Stories
Balozi Nchimbi kuongoza waombolezaji mazishi ya Kibiti leo
Dkt.Tulia,apewa tano kuwezesha wananchi
Nkasi yajipanga kukusanya mapatoÂ