March 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NHIF yaeleza inavyotumia TEHAMA kudhibiti udanganyifu

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya(NHIF)umesema umefanikiwa kuimarisha mifumo ya TEHAMA katika shughuli za mfuko ili kuimarisha utendaji na tija.

Ambapo kutokana na kuimarisha kwa mifumo hiyo wamefanikiwa kuokoa bil.22  kutokana na usimamizi madhubuti wa mfuko wa NHIF, fedha ambayo ilikuwa inapotea kutokana na udanganyifu wa baadhi ya wanachama.

Hayo yamesemwa jijini hapa leo Machi 10,2025 na Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Dkt.Irene Isaka wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na muelekeo wa mfuko huo katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita ambapo amesema watumishi 36 wa vituo vya kutolea huduma wamechukuliwa hatua kwa kufanya udanganyifu kwenye mfuko.

Dkt.Isaka amesema kuwa kupitia mfumo huo mwananchi anaweza kujisajili ili kujiunga na mfuko wa Taifa ya Bima ya Afya.

Vilevile amesema mwanachama anaweza kupata huduma za afya kupitia namba yake ya NIDA na si lazima awe na kitambulisho cha NHIF.

“Pia NHIF ina mfumo wa kutambua utendaji wa watumishi wake kutumia TEHAMA.
Tumeunganisha mifumo yetu na Taasisi nyingine za Serikali ikiwemo NIDA, RITA, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), TIRA,TRA na Wizara ya Afya,”amesema Dkt.Isaka.

Aidha ameeleza kuwa mfumo huo unachakata madai yote ya watoa huduma wao na unauwezo wa kufanya uchambuzi wa taarifa zilizowasilishwa za madai na kuondoa udanganyifu.

Hivyo kurahisisha malipo ya watoa huduma yanafanyika kwa wakati kwa sababu ya uwepo wa mifumo ya TEHAMA.

“Ambapo Madai ya watoa huduma za afya yanafanyika ndani ya siku 60 ikilinganishwa na siku 120 za awali kabla ya uwepo wa mifumo,”amesema.

Pamoja na hayo amesema katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita wamefanikiwa  kumesajili wanachama milioni 2.2.

Huku ukusanyaji wa michango ukifikia trilioni 2.3 kwa sasa kutokana na maboresho yaliyofanyika katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita.

“Shilingi trilioni 2.29  zimelipwa kwa watoa huduma waliohudumia wanachama wa NHIF.Ulipaji malipo ya watoa huduma unafanyika kwa wakati kwa kuzingatia huduma mpya za afya zinazotolewa.

“Vilevile bil.91 zimelipwa kwa watoa huduma waliohudumia wanachama wa NHIF ambao ni wastaafu.

Akizungumzia muelekeo wa NHIF Dkt.Isaka amesema kuwa ni kutumia TEHAMA kuendelea kuimarisha huduma zake kwa wananchi ili kurahisisha utoaji wa huduma bora na kwa wakati kwa wananchi.

Ambapo amesema NHIF inakwenda kusajili makundi maalumu kama wakulima, wajasiriamali na mengine.

“Tunawasihi wananchi kuendelea kujitokeza kwa ajili ya kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, msisubiri hadi mnapokuwa wagonjwa ndipo mshughulikie kupata Bima ya Afya,”amesema Dkt.Isaka.