January 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NHIF yaboresha Kitita cha Mafao mwaka 2023

Na Hamisi Miraji, Timesmajira Online

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya(NHIF), umeboresha kitita cha mafao cha mwaka 2023, kwa wananchi katika upande wa ushauri na huduma mbalimbali ikiwemo utoaji wa huduma za Dawa pamoja na uchujaji wa damu (Dialysis).

Kitita hicho kinatarajiwa kuanza utekelezaji wake rasmi Januari mosi,2024 baada ya mchakato wa zoezi la utoaji elimu kukamilika kwa wadau wote wa mfuko ikiwemo watoa huduma.

Hayo yamesema leo jijini Dar es Salaam, na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa Bima ya Afya (NHIF), Bernard Konga alipokutana na wahariri wa vyombo vya Habari nchini.

Konga amesema, kutumia kitita hicho fedha wanazolipa kwa watoa huduma upande wa dawa zitakuwa juu, ili waweze kupata faida kupitia kitita hicho huku upande wa uchujaji wa damu gharama yake ishuka kutoka 240,000 hadi 200,000.

Amesema kifungu Na 16(4), cha sheria ya Mfuko wa NHIF kimempa mamlaka Waziri kuridhia Kitita cha mafao kinachotolewa kwa wanufaika wa Mfuko.

“Kitita hicho cha Mafao kinaainisha orodha na bei za huduma zitolewazo kwa wanufaika ambazo hutumika wakati wa malipo kwa watoa huduma za matibabu.

“Kifungu Na 39A, cha Sheria ya Mfuko sura 395, kinataka kufanyika kwa tathimini ya uhai na uendelevu wa mfuko, ambapo tangu kuanza utekelezaji wa majukumu ya mfuko mwaka 2001, tathimin zipatazo saba zimefanyika (mwaka 2003,2006,2009,2012,2013,2016 na 2021),” amesema Konga.

Konga amesema, mapendekezo ya tathmini ya mfuko ni muhimu kuzingatiwa ili kuhakikisha kuna uendelevu katika upatikanaji wa huduma bora kwa wanufaika bila kuathiri uhai na uendelevu wake.

“Kitita cha mafao kinachotumika hivi sasa kilifanyiwa maboresho kwa mara ya mwisho mwaka 2016.

“Katika kutekeleza takwa hilo la Mkataba wa Agosti 1,2022 mfuko kupitia barua yenye Kumb Na EA35/269/01-A/32 ulitoa Notisi ya miezi mitatu ya kusudio la kufanya maboresho ya Kitita chake cha Mafao,” amesema.

Aidha, amesema tangu kutolewa kwa notisi hiyo Mfuko uliendelea kukusanya na kupokea maoni, ushauri na mapendekezo kutoka kwa wadau wake kwa lengo la kuboresha kitita chake cha mafao.

Akitaja miongoni mwa malengo ya maboresho hayo ni pamoja na kuboresha upatikanaji wa huduma bora kwa wanachama, kufanya maboresho ya huduma na gharama zake kwa kuzingatia maendeleo ya Teknolojia ya tiba na hali ya bei katika soko, Kuwianisha Kitita cha Mafo na Orodha ya Dawa muhimu (NEMLIT) pamoja na mwongozo wa Tiba wa Taifa (STG).

“Licha ya kuanisha malengo ya kitita cha mafao yalioboreshwa lakini walipita kwa wadau mbalimbali ili kupata maoni yao kuhusu maboresho ya kitita hicho.

“Yapo malengo mbalimbali ikiwemo kujenga uwezo wa vituo vya afya ngazi zote kuanzia afya ya msingi, kuboresha huduma kwa wananchi na kuimarisha udhibiti ili kuzuia mianya ya udanganyifu,” amesema.

Aliwataja wadau walioshirikishwa katika kuboresha kitita hicho ni pamoja na umoja wa Wamiliki Vituo binafsi vya Huduma za
Afya APHFTA, Tume ya Huduma za Kijamii za Kikristo (CSSC) na BAKWATA.

Wengine ni vyama mbalimbali vya kitaaluma, Cha cha Madktari Tanganyikia (MAT), vituo vya huduma vinavyomilikiwa na serikali ikijumuisha Hosptali za Rufaa za Mikoa na wanganga wafawidhi wa hospitali za halmashauri.

Akizungumzia mambo muhimu yaliozingatiwa wakati wa maboresho ya kitita hicho, Konga amesema kufanya tafiti ya gharama halisi za matibabu katika soko husika.

Amesema, Kushirikisha taasisi chini ya Wizara ya Afya ikiwemo Bohari ya Dawa (MSD) na TMDA, lengo ni kuwianisha kitita cha mafao na orodha ya dawa zolizosajiliwa.

Katika hatua nyingine, Konga amesema kupitia maboresho yaliofanyika kuna ongezeko la jumla ya dawa 124 katika kitita cha mafao cha mfuko kutoka orodha ya dawa muhimu ya Taifa (NEMLIT) na kuweka mbadala wa dawa 309 katika kitita cha mafao ili kuwianisha na NEMLIT.

Kwa upande wake Afisa Idara ya Habari, Maelezo Lilian Lundo amesema, utaratibu wa NHIF kushirikisha vyombo vya habari katika masuala mbalimbali unatoa nafasi kwa umma kupata taarifa sahihi kuhusu huduma za bima.

Naye Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Jukwaa la Wahariri, Jane Mihanji akitoa salamu kwa niaba ya Mwenyekiti wa (TEF), aliushukuru Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa kuendelea kuonesha ushirikiano na vyombo vya habari nchini.

“Niwashukuru kwa niaba ya TEF, kuona umuhimu wa sisi kuwa hapa, wakati wote mkiwa na jambo msisite kuwasiliana nasi, vivyo hivyo nasi linapotokea jambo msisite kupokea simu zetu ili kupata ufafanuzi mbalimbali juu ya umma kupata taarifa kuhusu bima ya afya” amesema.