Na Hamisi Miraji, Timesmajira Online
UNAPOZUNGUMZIA afya ni neno lenye maana ya ukamilifu wa binadamu kimwili, kiakili na kijamii kwa kutokuwepo kwa maradhi.
Huduma ya afya inaweza kushughulikia mahitaji mengi ya afya ya mtu katika maisha yake yote.
Miongoni mwa mahitaji hayo ni pamoja na kuzuia, kutibu, matibabu ya kurekebisha na kutunza.
Nusu ya watu bilioni 7.3 ulimwenguni bado hawapati huduma kamili na muhimu za afya. Kuna nchi takribani 30 ambazo maelezo yake yanapatikana, ni nane pekee ambazo hutumia angalau dola za Kimarekani 40 kwa kila mtu kwa huduma za msingi za afya kwa mwaka.
Uwepo Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya nchini (NHIF), umesaidia kwa kiasi kikubwa uimarishaji wa huduma za matibabu kupitia mpango wake wa mikopo ya vifaa tiba.
Taarifa za mfuko huo hadi kufikia Juni 2023, zinaonesha kuwa jumla ya vituo vya kutolea huduma za matibabu 401, vimenufaika na sh. Bilioni 46.3 ambazo zimetolewa kupitia mpango huo ili kuviwezesha kuboresha huduma zake.
Mpango huo umewezesha vituo kuongeza mapato kutokana na uwepo wa huduma bora.
Mei, 2023 wakati wa kusomwa na kujadiliwa kwa makadirio ya Bajeti ya Wizara ya Afya Bungeni, hoja kubwa ilizungumzwa na wabunge juu ya umuhimu wa bima ya afya kwa wananchi.
Kupitia hoja zile kila Mtanzania kwa sasa anatakiwa kuwa na Bima ya Afya ili aweze kupata huduma za matibabu wakati wowote na bila ya kuwepo kikwazo chochote cha fedha.
Wabunge walielezea adha mbalimbali wanazopata wananchi wakati wanapohitaji huduma za matibabu, lakini kubwa zaidi ni gharama kubwa za matibabu ambazo wengi wanashindwa kuzimudu
Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga amesema Serikal ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya afya hapa nchini.
Konga amesema, wamefanya maboresho ya huduma za NHIF kwa wadau wake nchini ili kila mmoja aweze kumudu gharama za matibabu.
“Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia imefanya mambo makubwa sana katika sekta ya afya, nasi kama taasisi za umma hatuna budi kufanya maboresho ambayo yatawezesha wananchi kupata huduma bora na haraka,” amesema Konga.
Amesema, NHIF imefanya maboresho kitita cha mafao, lengo la kwanza ni kuboresha upatikanaji wa huduma bora na za uhakika kwa wanachama.
La pili kufanya maboresho ya huduma na gharama zake kwa kuzingatia maendeleo ya teknolojia ya tiba na hali ya bei katika soko.
Aidha, amesema lengo lingine ni kuwianisha kitita cha mafao na orodha ya dawa muhimu (NEMLIT) pamoja na Mwongozo wa Tiba wa Taifa (STG).
Hata hivyo licha ya kuanisha malengo ya kitita cha mafao yalioboreshwa lakini walipita kwa wadau mbalimbali ili kupata maoni yao kuhusu maboresho ya kitita hicho.
Yapo malengo mbalimbali aliyoainisha ikiwemo kujenga uwezo wa vituo vya afya ngazi zote kuanzia afya ya msingi, kuboresha huduma kwa wananchi na kuimarisha udhibiti ili kuzuia mianya ya udanganyifu.
Amesema, yapo mambo muhimu yaliyozingatiwa wakati wa maboresho ya kitita hicho, hasa kufanya tafiti ya gharama halisi za matibabu katika soko husika.
Kushirikisha taasisi chini ya Wizara ya Afya ikiwemo Bohari ya Dawa (MSD) na TMDA, lengo ni kuwianisha kitita cha mafao na orodha ya dawa zolizosajiliwa.
Kupitia maboresho yaliofanyika kuna ongezeko la jumla ya dawa 124 katika kitita cha mafao cha mfuko kutoka Orodha ya dawa muhimu ya Taifa (NEMLIT) na kuweka mbadala wa dawa 309 katika kitita cha mafao ili kuwianisha na NEMLIT.
Konga amesema, Kitita hicho kinatarajiwa kuanza utekelezaji wake rasmi mwaka huu baada ya mchakato wa zoezi la utoaji elimu kukamilika kwa wadau wote wa mfuko ikiwemo watoa huduma.
Katika kubainisha hilo, hivi karibuni Waziri wa Afya Ummy Mwalimu alitoa taarifa ya hali ya utoaji huduma za afya nchini kwa mwaka 2023.
Ummy amesema, Tanzania inafanya vizuri upande wa Utalii Tiba ambapo Kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanyika katika kuboresha huduma za kibigwa na bobezi, Tanzania imeweza kuvutia wagonjwa kutoka nje ya nchi na kwa takwimu za mwaka 2023 Wagonjwa 1,937 waliotoka nje kuja kutibiwa nchini.
“Kwa mwaka 2022 idadi ya wa wagonjwa kutoka nje ya nchi wa Tiba Utalii waliokuja kutibiwa nchini ilikuwa 1,699 na takwimu za mwaka 2023 zinaonesha kuwa jumla ya Wagonjwa 1,937 waliotoka nje ya Nchi walikuja kutibiwa nchini”
“Wagonjwa hawa wanatoka katika nchi za Comoro, Malawi, Burundi, Zambia, Congo DRC, Uganda, Zimbabwe na Kenye, walihudumiwa katika Hospitali sita ikiwemo Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Taasisi ya Mifupa MOI, Aga khan na Saifee”
“Tanzania imekuwa kimbilio la wagonjwa kutoka nje ya nchi, na wagonjwa hawa wanaleta fedha za kigeni na hivyo kuchangia pato la Taifa.
“Asilimia 74 ya Watanzania wanapata huduma za afya katika ngazi ya msingi yaani zahanati, vituo vya afya na hospitali za Wilaya/Halmashauri,”anasema.
Hata hivyo amesema, Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais TAMISEMI itaendelea kuongeza nguvu ya kuimarisha usimamizi na uendeshaji wa utoaji wa huduma za afya ngazi ya msingi.
Mbali na hivyo, katika kuhakikisha sekta ya afya inakua, NHIF imewezesha ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamini Mkapa iliyoko Dodoma, ambayo inatoa huduma za kibingwa bobezi, ambapo awali wanachi walilazimika kwenda nje ya nchi kupata matibabu.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka NHIF, jumla ya shilingi Bilioni 129.2 zilitumika katika ujenzi wa hospitali hiyo pamoja na ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa vya uchunguzi wa magonjwa.
Mbali na uwekezaji huo mkubwa, mfuko kupitia mpango huo umewezesha ujenzi wa majengo pacha ya Hospitali ya Mifupa (MOI), kwa gharama ya sh. Bilioni 17.97. Majengo hayo yameboreshwa zaidi huduma hospitalini hapo na kuwezesha huduma mbalimbali za kitaalam kufanyika bila kikwazo cha ukosefu wa vifaa, dawa au majengo.
Mfuko huo pia, umefanya maboresho makubwa ikiwemo matumizi ya alama za vidole na sura kwa kuwatambua wanachama wake wakati wanapohitaji kupata huduma za matibabu katika vituo vya matibabu.
Matumizi ya alama za vidole na sura ni moja ya maboresho makubwa yanayofanywa na mfuko huo ili kuimarisha na kurahisisha zaidi huduma za upatikanaji wa huduma za matibabu kwa wanachama, lakini pia kulinda uhai endelevu wa mfuko.
Hata hivyo, pamoja na jitihada za kusimamia upatikanaji na huduma bora kwa wanufaika wake, bado kumekuwa na changamoto mbalimbali katika utoaji wa huduma ikiwemo kutozingatiwa kwa masharti ya mkataba baina ya mfuko na wadau wake ikiwemo watoa huduma na wanachama.
Hadi kufikia Juni 2023, Mfuko umechukua hatua kwa wote waliobainika kufanya udanganyifu ikiwa ni pamoja na kusitisha mikatana 18 baina yake na watoa huduma. Kuwaripoti watumishi 139 wa sekta ya afya katika mamlaka zao za ajira yakiwemo mabaraza yao ya kitaaluma kwa wanufaika (1,197).
Kwa mfuko zimechukuliwa ikiwemo kusitisha matumizi ya kadi (697), kuamuriwa kulipa gharama za matibabu zilitumika (325), kuwafungulia mashtaka (67) na kuwaripoti katika mamlaka za uchunguzi (108).
Katika kuimarisha usimamizi wa huduma za Bima ya Afya kwa wanachama wake, na pia kupata suluhisho la changamoto zinazojitokeza na kuhakikisha kuwa wanachama wanapata huduma bora, kuanzia mwezi Juni 2023, mfuko uliamua kuweka watumishi wake katika baadhi ya mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Kilimanjaro na Dodoma.
More Stories
Ubunifu wa Rais Samia kupitia Royal Tour unavyozindi kunufaisha Tanzania
Rais Samia anavyojenga taasisi imara za haki jinai kukabilina na rushwa nchini
Rais Dk. Samia alivyowezesha Tanzania kuwa kinara usambazaji umeme Afrika