Na Iddy Lugendo, Timesmajira Online
SHIRIKA la nyumba la Taifa (NHC) limetoa msaada wa vitu mbalimbali ikiwemo vyakula na mavazi vyenye thamani zaidi ya milioni 2 katika kituo cha kulelea watoto yatima chenye jumla ya watoto 32 wakiwamo wa shule ya sekondari, msingi, chekechea na wengine ni wachanga ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Machi 08, 2024 Mpanda Mkoani Katavi Afisa Habari wa Shirika la Nyumba la Taifa Domina Rwemanyila amesema jukumu la kutoa zawadi au msaada kwa watoto hao ni jukumu la jamii nzima kwani katika watoto hao watapatikana akina mama na akina baba wa badae.
Aidha, Afisa Habari wa Shirika la Nyumba la Taifa Domina Rwemanyila amesema jambo hilo ni muendelezo wa shirika la Nyumba la Taifa katika kuendelea kutoa misaada kwenye sehemu mbalimbali zenye mahitaji, hivyo kupitia kwa Mkurugenzi wa NHC Hamad Abdalah, wataendelea kutoa misaada hiyo ili kuendelea kupeleka faraja na furaha kwa watu wote wenye uhitaji.
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) pia limepokea hati ya shukrani kutoka kwa Kituo cha Watoto Yatima Nsemulwa, cha Masista wa Maria Mtakatifu Malkia wa Afrika Kanisa Katoliki Jimbo la Mpanda, Hati hiyo ya shukrani imekabidhiwa leo kwa NHC na Mratibu wa Kituo hicho Rose Sungura, kufuatia msaada wa vitu mbalimbali vilivyotolewa kwa ajili ya Watoto hao.
Kwa upande wake, Mkuu wa kituo cha kulelea watoto Yatima Rose Sungura amesema kuwa Taasisi inayowakumbuka yatima ni mfano wa kuigwa kwani wangeweza kupeleka misaada yao sehemu zenye kuwaletea faida lakini NHC imeamua kutuletea sisi bila kupata faida yoyote huu ni upendo wa ajabu sana na ni mfano wa kuigwa.
“Fedha iliyotumika kununua vitu ingeweza kutengeneza faida kwenu lakini mkaona ni bora kuisaidia jamii ambayo inauhitaji mkubwa sana ili iweze kusonga mbele, ni jana tu nimehangaika kutafuta mabegi ya shule ya watoto, lakini leo Mungu amewaongoza mmetuletea mabegi mengi ya kutosha huu ni muujiza kwani ambacho nimehangaika na kukifikiria jana nakipataje leo mmekileta Mungu awabariki sana” amesema Sungura
Pia Mkuu wa kituo cha kulelewa watoto yatima Rose Sungura amesema jumla ya idadi watoto walio katika kituo hicho ni 32 ambapo lengo la kituo hicho ni kutoa malezi ya makuzi pamoja na elimu.
Naye Frank Malambo ni moja ya mzazi mwenye mtoto katika kituo cha kulelea watoto yatima amesema wanaume wengi hawashiriki ipasavyo kutembelea vituo hivyo hasa pale wanapopeleka watoto wao mara baada ya kufiwa na wenza wao
Hivyo, Wanaume wanaopeleka watoto katika vituo vya kulelea watoto yatima na wale watoto wanaotokea katika mazingira magumu wameombwa kutembelea watoto hao ili kujenga ukaribu na watoto wao wakiwa katika vituo hivyo.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa