Na Mwandishi wetu,Timesmajira
MAMLAKA ya Hifadhi ya Ngorongoro imeongoza kwa kukusanya mapato ya juu zaidi kupitia shughuli za utalii nchini, ambapo katika mwaka wa fedha 2024/2025 imeingiza jumla ya shilingi bilioni 269.9.
Mafanikio haya yanatokana na ongezeko la watalii wa ndani na nje ya nchi, sambamba na maboresho ya miundombinu ikiwemo reli ya kisasa (SGR), ambayo imerahisisha usafiri hadi kwenye vivutio vya utalii.
Akizungumza Siku ya Ngorongoro katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu kama Sabasaba, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Pindi Chana, amesema mwamko mkubwa wa Watanzania kutembelea hifadhi umechangia ongezeko la watalii, ambapo idadi ya wageni waliotembelea hifadhi mbalimbali imefikia zaidi ya milioni 5.
Waziri Chana amesema kuwa Maadhimisho ya Siku ya Ngorongoro katika maonesho hayo imelenga kutangaza utalii wa ndani na kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu thamani ya rasilimali za taifa zinazopatikana kwenye hifadhi.
Amesema kuwa uelewa ulioongezeka kupitia Kampeni kama The Royal Tour na Amazing Tanzania ambapo umechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la idadi ya watalii katika miaka ya hivi karibuni.

“Hili linajumuisha siyo tu watalii wa kimataifa, bali pia ongezeko la watalii wa ndani, hasa wakati wa likizo na mwishoni mwa wiki.
“Kwa miaka ya hivi karibuni tunaona mabadiliko familia, watu binafsi, ofisi, na hata kwaya za makanisa wanatembelea maeneo ya hifadhi kwa wingi. Ndiyo maana tuna imani kuwa tutafikia lengo la watalii milioni nane ifikapo mwaka 2030,” amesema.
Waziri Dkt. Chana amesisitiza kuwa utalii bado ni nguzo muhimu ya uchumi, ikichangia katika uundaji wa ajira na mnyororo mpana wa thamani nchini kote.
Ameongeza kuwa juhudi za serikali zinalenga kuhakikisha Watanzania wengi wananufaika na ukuaji wa sekta hiyo.”Kuna umuhimu wa kuadhimisha Siku ya Ngorongoro katika maonesho ya biashara,kwani itasaidia kukuza utalii wa ndani na kuonyesha vivutio vya kipekee.
“Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) tayari imekusanya Shilingi bilioni 269.9 katika mapato kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ikiwa ni ishara ya mafanikio ya mikakati ya masoko na ushirikishwaji wa umma,”amesema

Kwa Upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Latifa Khamis, amesema kuwa uhifadhi na utalii vinazidi kuwa vivutio vikuu katika maonesho hayo. Kufikia Julai 11, banda la Wizara tayari lilikuwa limevutia wageni 659,604, na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka hadi kufikia mwisho wa maonesho.
Amesema Ngorongoro kama eneo la kipekee kutokana na uwepo wa binadamu na wanyamapori wanaoishi kwa pamoja, jambo linaloongeza mvuto wake kimataifa.
Naye Kamishna Msaidizi Mwandamizi kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Mariam Kobelo, amrhakikishia umma kuwa mamlaka hiyo imejizatiti kulinda urithi wa kitamaduni na kihistoria wa eneo hilo chini ya mfumo wa sasa wa kisheria, kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
Mpango wa serikali unaakisi maono mapana ya kuufanya utalii kuwa nguvu kuu katika mabadiliko ya kijamii na kiuchumi nchini Tanzania.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi