Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
KIKOSI cha timu ya Taifa ya Vijana ya Tanzania chini ya umri wa miaka 20, ‘Ngorongoro Heroes’ leo kitashuka dimbani kuwakabili Somalia katika mchezaji wake pili wa Kundi A wa mashindano ya CECAFA utakaochezwa kwenye Uwanja wa Black Rhino, Karatu.
Vinara hao wa Kundi A watakutana na Somalia ambao wana hasira za kujeruhiwa na Djibouti ambao waliibuka na ushindi wa goli 2-1 katika mchezo wao wa juzi lakini pia wakitaka kuendeleza ushindi baada ya kupata ushindi mnono wa goli 6-1 katika mchezo wao wa kwanza dhidi ya Djibouti.
Katika mchezo huo Djibouti walikuwa wa kwanza kuliona lango la Ngorongoro baada ya msambuliaji Abdorahman Kamil kuipatia bao dakika ya 14 lakini Tanzania walisawazisha dakika ya dakika ya 52 mshambuliaji Teps Theonasy.
Pia waliongeza magoli yaliyofungwa na Abdul Hamis dakika ya 65, 71 na 90 na mengine yakiwekwa kimiani na Khelfin Hamdoum dakika ya 82 na Kassim Haruna dakika ya 88.
Akizungumza kuelekea katika mchezo huo wa leo, kocha mkuu wa Ngorongoro Heroes, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ amesema kuwa, watahakikisha wanaendelea kutoa kichapo katika mchezo huo ili kujihakikishia nafasi ya kucheza nusu fainali katika mashindano hayo na hatimaye kutinga fainali ambayo itawahakikishia nafasi ya kuiwakilisha nchi katika Fainali za U-20 za Afrika zitakazofanyia nchini Mauritania.
Amesema, jambo zuri ni kuwa wanaelewa wanakwenda kukutana na timu ya aina gani baada ya kusoma mbinu zao katika mechi yao ya juzi ambazo pia watazitumia kama silaha ya kuwawezesha kupata ushindi.
Julio amesema kuwa, watahakikisha wanacheza mchezo huo kama watu wazima na watapambana kwelikweli, kuingia na nidhamu ya hali ya juu pamoja na kutuliza mipira ili kuweza kufikia malengo yao.
“Tutaingia katika mchezo wetu wa leo huku tukisaka alama tatu muhimu ambazo zitatuwezesha kutinga nusu fainali. Tumefanikiwa kuanza vizuri mashindano haya na tutahakikisha tunaendeleza matokeo mazuri tuliyoanza nayo hivyo leo tutatumia madhaifu ya wapinzani wetu kwani tumeshajua sehemu ambazo tutakazowadhibiti na wapi tutatumia kuawamaliza,” amesema Julio.
Hata hivyo kocha huyo amesema kuwa, tayari ameshawajenga kisaikolojia wachezaji wake na hawatarudia makosa waliyoyafanya katika mchezo wao wa kwanza katika mashindano hayo dhidi ya Djibouti.
Katika mashindano hayo, mshindi wa kila kundi ataingia moja kwa moja nusu fainali na timu zitakazoshiriki nafasi ya pili kwa kundi B na C zitacheza bechi kusaka ‘best looser’ ambapo timu hiyo itakutana na mshindi wa kundi A huku mshindi wa Kundi B akichuana na mshindi ya kundi C.
Mechi hizo za nusu fainali zitachezwa Vovemba 30 huku mechi ya kumsaka mshindi wa tatu pamoja na mshindi wa mashindano hayo ikichezwa Desemba 2.
More Stories
Naibu Waziri wa Fedha abariki ujio mpya wa Bahati Nasibu
Zanzibar kuzalisha wachezaji wenye vipaji
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes