January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ngalula azindua Kamati za Bodi ya TPSF

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online Dar

Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Sekta Binafsi Nchini(TPSF), Angelina Ngalula, amezindua kamati saba za bodi ya TPSF zitakazopendekeza uboreshaji wa mazingira ya kufanya biashara na kuvutia uwekezaji nchini.

Kamati zilizozinduliwa ni Kamati ya Programu na Maendeleo ya Biashara, Kamati ya Fedha na Utawala, Kamati ya Ukusanyaji Rasilimali endelevu, Kamati ya Uwekezaji, Kamati ya Huduma za Uanachama, Kamati ya Sera, Tafiti na Ushawishi na Kamati ya Ukaguzi na Tahadhari.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kamati hizo, Ngalula amezitaka kamati kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, na kuwataka wafanyabiashara kuwa wazalendo, wawajibikaji na wawazi katika ulipaji kodi ili kuiwezesha Serikali kufikia malengo yake.

“Serikali ya awamu ya Sita imejiwekea malengo ya kukusanya kiasi cha sh. trilioni mbili kila mwezi kutokana na kodi hivyo ni nafasi kwa sekta binafsi kuiwezesha Serikali kufikia malengo hayo kwa kulipa kodi stahiki na kwa wakati,” amesema Ngalula

Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Sekta Binafsi Nchini (TPSF), Angelina Ngalula (katikati waliokaa) akiwa kwenye picha ya pamoja na wenyekiti wa kamati mbalimbali mara baada ya hafla ya uzinduzi wa kamati mbalimbali sita ndani ya bodi ili kukusanya maoni na kuleta mapendekezo yatakayosaidia kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuvutia uwekezaji hapa nchini iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana.

Amesema ili kufanikiwa kupata masoko hasa ya nje ya nchi ni lazima kwa kamati hizo ziwe na mahusiano mazuri na kuwatumia wanadiaspora waliopo nje ya nchi.

“Kuna wenzetu wengi tu wapo nje ya nchi. Hawa endapo tutawatumia vyema itakuwa rahisi hata kwetu sisi kuweza kupata masoko ya nje,” ameeleza Ngalula.

Ngalula amezitaka kamati hizo kuhakikisha zinatafuta namna ya kuwajengea miradi na uwezo vijana ambao amesema ni taifa la kesho.

“Kuna idadi kubwa ya vijana ambao kwa namna moja wanakwama kufikia malengo yao kwa kuwa tu hawajajengewa uwezo wa kujua namna ambavyo wanaweza kunufaika na fursa mbali mbali zilizopo.” Amesema Ngalula.

Aidha ameitaka sekretarieti kubuni njia bora za mapato ili fedha itakayopatikana isaidie katika utendaji wa majukumu, hasa ya kuwafikia wadau wengi wa mikoani.

“Wote tunafahamu kuna changamoto ya kifedha, lakini hii inatakiwa iwe chachu ya sisi kufikiria zaidi njia za kupata fedha za kuendesha shuguli za kuwafikia wadau wengi zaidi,” amesema

Mwenyekiti wa Kamati ya Sera,Tafiti na Ushawishi ambaye pia ni Mbunge wa Kibaha, Sylvestry Koka, amesema kamati itahakikisha changamoto za kisera zinatatuliwa ikiwa ni pamoja na ushirikishwaji wa wafanyabiashara katika upangaji wa viwango vya kodi na kutoa ushauri utakaoleta manufaa katika maendeleo ya nchi.

“Mimi ninaahidi kwako, mwenyekiti, kuwa kamati yangu itatekeleza kwa ufasaha maelekezo na hasa kuhakikisha wafanyabiashara wanashiriki kikamilifu kwenye kujenga nchi yao pamoja na kutatua vikwazo wanavyokutana navyo,” amesema Koka.

Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Utawala. Mercy Sila, amesema ili kuwepo na maendeleo endelevu ya ndani na taasisi ni muhimu kuhakikisha suala la utawala, uwazi na usimamizi wa fedha linasimamiwa kwa umakini na uzalendo mkubwa ili kujenga imani kwa wananchama juu ya mapato na matumizi na hali ya utawala kwa ujumla.

Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Sekta Binafsi Nchini (TPSF),Angelina Ngalula (katikati) akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kamati mbalimbali sita ndani ya bodi ili kukusanya maoni na kuleta mapendekezo yatakayosaidia kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuvutia uwekezaji hapa nchini. Kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati ya Sera,Tafiti na Ushawishi ambaye pia ni Mbunge wa Kibaha, Sylvestry Koka na kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasis ya Sekta Binafsi nchini, Francis Nanai.

“Katika ofisi yeyote ile, iwe ya serikali au taasisi binafsi, suala la uwazi kwenye utawala na usimamizi mzuri wa wa fedha ni mambo muhimu kwa maendeleo na ustawi wake; hivyo kamati yangu inakuhakikishia Mwenyekiti kuwa itasimamia misingi hii madhubuti ya utawala bora.

Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Francis Nanai, amesema sekretarieti imejipanga vyema kuhakikisha mipango na malengo waliyojiwekea yanafanikiwa huku akikiri kuwa suala la kutengeneza uhusiano na wanadiaspora linatija kubwa kwa ustawi wa wafanyabiashara nchini.

“Kwa kweli tumekuwa na mkutano wenye manufaa makubwa na kwa kipekee niwashukuru wanakamati wa kamati zote kwa mapendekezo na ushauri mliotupatia hasa kuhusu hili la diaspora. Mapendekekzo na ushauri wenu vitakuwa na mchango mkubes kwa wafanyabiashara na hata taifa.