October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NFRA yajivunia mafanikio miaka mitatu ya Samia

Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline, Dodoma

MKURUGENZI Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Dkt. Andrew Komba, amesema taasisi hiyo imepata mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.

Mafanikio hayo ni pamoja na kuwa maghala ya kutosha kwa ajili ya kuhifadhi nafaka zinachonunuliwa kutoka kwa wakulima.

“Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, uwezo wa NFRA ulikuwa kuuza wastani wa tani 50,000 tu za nafaka, lakini baada ya taasisi hiyo kujengewa uwezo tumeweza kufikisha hadi tani 1,750,000 kupitia mauzo ya nafaka yanayofanyika ndani na nje ya nchi,” alisema Dkt Komba.

Akiongea na waandishi wa habari Jijini hapa hivi karibuni Dkt Komba amesema kuwa mafanikio hayo yanatokana uungwaji mkono mkubwa kutoka serikalini kupitia Wizara ya Kilimo chini ya Waziri wake, Hussein Bashe.

“Hii imetokana na kasi ya ukuaji wa taasisi hiyo ambayo imepata mafanikio makubwa ndani ya kipindi cha miaka mitatu iliyopita. Pia katika kipindi hicho, NFRA kama taasisi ilikuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 50,000 tu za nafaka,” alisema.

Kwa mujibu wa Dkt Komba, baadaye uwezo huo uliongezeka hadi kufikia tani 351,000 baada ya utekelezaji wa mradi wa uhifadhi nafaka wa miaka mitatu ulioanza mwaka 2018 na kusimam iwa na Wizara ya Kilimo.

“Baada ya uwekezaji huo kufanyika ikiwemo wa miundombino mbalimbali, uwezo wa uhifadhi wa taasisi umeongezeka hadi kufikia tani 400,000 mpaka kufikia mwezi Juni mwaka huu. Matarajio ya NFRA ni kuwa na uwezo wa kuhifadhi kati ya tani 700,000 hadi 1,000,000 kufikia Juni mwakani yaani 2025,” alisisitiza.

Dkt Komba alisema NFRA kwa sasa imebadilisha mtazamo kutoka kuwa taasisi ya kuhifadhi nafaka pekee na kuwa taasisi ya kufanya biashara ya nafaka baada ya kutosheleza hifadhi ya chakula cha kutosha hapa nchini ili kuzidi kujiongezea uwezo.

“Tuna mipango ya kupanua biashara zaidi ya kuuza nafaka katika nchi za jirani kufikia matarajio tuliyonayo,” alisema na kuongeza kuwa

NFRA kama taasisi imewajengea uwezo watendaji wake na kuwapa mafunzo ndani na nje ya nchi ili kuzidi kuwajengea uwezo katika utendaji wao.