January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NFRA yagawa chakula cha bei nafuu kwenye Halmashauri zenye mfumuko wa bei

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

SERIKALI kupitia Wakala wa Taifa wa hifadhi ya Chakula(NFRA)umesema umeanza kugawa Chakula Cha bei nafuu kwa Mikoa ambayo imekuwa na mfumuko mkubwa wa bei ya Chakula huku ikiimarisha hifadhi ya chakula nchini kwakuongeza akiba ya chakula toka Tani 58000 hadi kufikia Tani 110,000 kwa Mwaka 2021/2022 na ununuzi wa Chakula kwa Mwaka 2022/2023 unaendelea.

Hayo yamesemwa jijini hapa leo na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), CPA. Milton  Lupa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu shughuli za Wakala hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa Mwaka wa Fedha 2022/23.

Amesema kuwa ununuzi wa nafaka kwa msimu wa huo unaendelea kupitia kanda za Sumbawanga,(mikoa ya Rukwa na Katavi),Songea(mkoa wa Ruvuma),Arusha(mkoa wa Manyara)Shinyanga(mkoa wa Kigoma),Makambako(mikoa ya Iringa na Njombe),Songwe(mikoa ya songwe na Mbeya)na Dodoma.

Lupa amesema kuwa Wakala wa uhifadhi wa Chakula umejipanga kuhudumia maeneo mengine yatakayothibitika kuwa na mahitaji ya dharura na upungufu wa Chakula huku akitoa wito kwa wanachi ili kuwa na usalama wa Chakula ni muhimu kujihifadhia chakula ili kuwa na akiba ya kutosha.

“Wakala unawajibu wa kutoa chakula kwa walioathirika na upungufu wa chakula kutokana na majanga mbalimbali kwa kufuata maelekezo yanayotolewa na serikali,

“Chakula hicho hutolewa kwakuzingatia matokeo ya tathmini ya hali ya chakula nchini inayofanywa na serikali kupitia wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na wadau wengine,”amesema Lupa.

Pamoja na hayo Lupa amesema kuwa NFRA imefanikiwa kukamilisha sehemu ya Mradi na kuongeza uwezo wa kuhifadhi nafaka hadi tani 90,000 katika kanda za Arusha (Halmashauri ya Babati) na Sumbawanga na Mpanda.

Lupa amesema kuwa utekelezaji wa  mradi huo kwajili ya kuongeza uwezo wa kuhifadhi nafaka,ambapo ukikamilika utaongeza uwezo wa kuhifadhi kutoka tani 251,000 hadi tani 501,000.

“Kukamilika kwa Mradi huo kumeongeza uwezo wa kuhifadhi nafaka kutoka tani 251,000 hadi tani 341,000 na utekelezaji wa Mradi katika maeneo mengine Dodoma, Songea,Shinyanga,Songwe na makambako umefikia asilimia 85,”amesema.

Pia Lupa amezungumzia suala la ajira ambapo amesema NFRA imefanikiwa kutoa ajira za muda mfupi kwa wananchi zaidi ya 3,000 zinazochangia kipato kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

“Ajira hizo zinatokana na kazi mbalimbali zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa zoezi la ununuzi wa nafaka,uhifadhi na kipindi cha uzungushaji wa nafaka na utekelezaji wa Mradi wa kuongeza uwezo wa kuhifadhi nafaka,”Ameeleza Lupa

Lupa amesema ili kukabiliana na makali ya mfumuko wa bei za nafaka Wakala kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo imeongeza upatikanaji wa nafaka katika masoko ili kuleta unafuu wa maisha kwa wananchi.

“Kwa kuanzia,Wakala unahudumia Halmashauri za Bunda,Sengerema,Geita, Nzega,Liwale,Nachingwea,Longido,Loliondo na Monduli ambapo takriban tani 3,000 zimepelekwa katika maeneo hayo,”Amesema Lupa

Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ni Taasisi ya Serikali chini ya Wizara ya Kilimo iliyoanzishwa kwa Sheria ya Wakala za Serikali Na.30 ya mwaka 1997 na ulianza kazi rasmi julai 1,2008 ikiwa na jukumu la kuhakikishia nchi usalama wa chakula kwa kununua na kuhifadhi akiba ya chakula na kutoa chakula cha msaada kwa waathirika waliokumbwa na majanga mbalimbali ya kitaifa.