Na Mwandishi Wetu, timesmajira,online Dar
BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limepata mafanikio katika kutekeleza majukumu yake katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa Rais Dkt. John Magufuli.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Samwel Gwamaka, amesema katika miaka mitano iliyopita, NEMC imeweza kujipambanua kama taasisi muhimu katika kufanikisha azma ya Serikali ya ujenzi wa viwanda na kuimarisha msingi wa uchumi wa kati.
“Katika kipindi cha miaka mitano Serikali ya Rais Magufuli NEMC imekewa mazingira rafiki na kuondoa baadhi ya vikwazo ambavyo vilifanya NEMC kushindwa kusimamia utekelezaji wa majukumu yake,’’ amesema Dkt. Gwamaka na kutaja sehemu ya mafanikio hayo kuwa ni pamoja na kuzuia matumizi ya mifuko ya plastiki.
NEMC pia huratibu na kutoa ushauri juu ya kulinda maeneo makubwa kama hifadhi za taifa na namna nzuri ya kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Dkt. Gwama amesema NEMC imejenga utaratibu wa kukutana na wawekezaji na wafanyabiashara na kwamba kwa pamoja wamekubaliana juu ya umuhimu na faida ya kutunza mazingira kwa manufaa ya ustawi wa jamii ya watanzania na dunia kwa ujmla.
“Katika kipindi cha miaka mitano tumekutana na wawekezaji pamoja na wafanyabiashara ili kujadiliana mambo muhimu ya mazingira ambayo yalionekana kuwa ni changamoto kubwa na kuyapatia ufumbuzi na pia waliweza kutambua NEMC kama chombo wezeshi na kinachosimamia watu wafuate sheria na taratibu za mazingira,’’ ameeleza. NEMC imepunguza siku za utoaji vibali vya Athari ya Tathmini kwa Mazingira (TAM).
Amesema katika kipindi hicho NEMC imeweza kushirikiana na vyombo vingine kuhakikisha malengo ya serikali yanatimia kwa kuondoa vikwazo visivyo na lazima na kuongeza kwamba NEMC imewahimiza wawekezaji na wafanyabiashara kutunza na kulinda mazingira kwa manufaa ya vizazi vya leo na vijavyo.
“Mbali ya kutoa elimu kwa wawekezaji na wafanyabiashara, Baraza limeondoa vikwazo kadhaa ambavyo vilikuwa vinachelewesha mchakato wa kupata vibali hali ambayo ilikuwa inawakatisha tamaa wawekezaji kuwekeza hapa nchini,’’ amesema na kuongeza kuwa baraza litaendelea kusimamia kanuni, sheria na taratibu za mazingira.
Dkt. Gwamaka amesema kuwa elimu kwa wananchi pamoja na mafunzo kwa maofisa mazingira yataendelea kutolewa ili kufikia malengo ambayo Serikali ya imejiwekea.
“Licha ya mafanikio yaliyopatikana, NEMC tutaendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya utunzaji wa mazingira lakini pia kwa maofisa wetu wa mazingira ili kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali,” amesema.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
27 kulipwa kifuta jasho Nkasi
Mwakilishi Mkazi wa UN nchini awasilisha hati