Na Penina Malundo, Timesmajira
ILI mwanafunzi aweze kufaulu vizuri mitihani yake na kukuza taaluma yake ipasavyo, anapaswa kutengenezewa mazingira mazuri ya kusomea ikiwemo miundombinu ya uhakika ambayo itauwezesha kusoma bila kupata changamoto yoyote.
Miongoni mwa miundombinu muhimu inayopaswa kuwepo shuleni ni pamoja na nishati ya umeme ya uhakika, madarasa, jengo la utawala pamoja na mabweni ambayo inasaidia kwa kiasi kikubwa kusaidia ufaulu kuongezeka kwa wingi kutokana na uwepo wa mazingira mazuri ya kusomea .
Kwa kuona hilo Miradi ya Maendeleo ya Kijamii (LADP),chini ya Mradi Mkubwa wa Kufua Umeme wa Rusumo uliopo katika Mpango wa Bonde la Mto Nile (Nile Basin Initiative NELSAP )ambao unafadhiliwa na Benki ya Dunia (World Bank),iliamua kutoa msaada wa vitu mbalimbali katika Shule ya Ngara High School kwa lengo la kuboresha mazingira ya shule hiyo.
Uamuzi huo umefikiwa baada ya mradi wa LADP kwa kushirikiana na wananchi kutambua vipaumbele vyao ambavyo vinaonyesha sehemu gani zinachangamoto na kuweza kuzitatua kwa kusaidiwa kuwezeshwa na NELSAP ikiwemo eneo hilo la Shule ya sekondari Ngara.
Wananchi walichagua eneo hilo baada ya kuona Ngara High School kuwa na mazingira magumu ya kusomea wanafunzi kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo umeme, mabweni, bwalo la chakula pamoja na jengo la utawala kwa ajili ya ofisi za walimu na watendaji wengine wa shule.
Changamoto ya miundombinu ya shule hiyo imetokana na shule hiyo kurithi majengo ya wakimbizi mwaka 2019 baada ya kufungwa kwa kambi iliyokuwa inajulikana kwa jina la Lumasi ambayo ilikuwa na changamoto nyingi ya kimazingira ikiwemo ukosefu wa umeme pamoja na majengo kuwa ya kizamani.
Nelson Rwamtamo Makamu Mkuu wa Shule ya Ngara anasema shule hiyo ilianza na wanafunzi 115, ikiwa na miundombinu hafifu ambayo iliachwa na wakimbizi waliokuwa wanaishi hapo kabla ya kufungwa kwa kambi hiyo.
Anasema baada ya kuanzisha shule hiyo walikuwa wanatumia umeme wa jua(solar)ambao ilikuwa inawatesa wanafunzi hususan nyakati za masika ambapo jua lilikuwa haliwaki hivyo kufanya mwanga kutotoka katika taa.
Rwamtamo anasema hali hiyo ilikuwa mbaya kwao kitaaluma kwani wanafunzi walikuwa wanashindwa kujisomea nyakati za usiku na kuishia kukaa mabwenini pindi umeme ukiwa hauwaki au mvua zikiwa zinanyesha.
Anasema hali ya ufaulu ilikuwa inashuka kwa wanafunzi wao na kufanya kushika nafasi za mwisho kutokana na miundombinu ya shule kutokuwa rafiki kwa wanafunzi wao.
”Walimu tulishindwa kabisa kufundisha hadi usiku hali iliyotufanya kuwa tunahakikisha tunafundisha mchana tu,ikifika usiku kama umeme wa solar ukiwepo wanafunzi watajisomea kama hamna wanafunzi watalala hivyo ilitufanya kushindwa hata kuandaa masomo nyakati za usiku hali iliyofanya kuzidi kurudi nyuma kitaaluma,”anasimulia na kuongeza
”Mwaka 2023 tulibahatika kupata umeme mkubwa wa maji,umeme huu ulikuja kwa msaada wa LADP ,chini ya Mradi Mkubwa wa Kufua Umeme wa Rusumo uliopo katika Mpango wa Bonde la Mto nile (Nile Basin Initiative NELSAP )na kufadhiliwa na Benki ya Dunia(World Bank),ambao ulitusaidia kwa kiasi kikubwa sana kuendesha shughuli zetu za Kitaaluma,na kubadilisha kabisa maisha yetu katika shule yetu,”anasema.
Rwamtamo anasema maisha yao yaliweza kubadilika kwa kiasi kikubwa,hali ya kujisomea kwa wanafunzi ilianza kuonekana na hata walimu kuanza kufundisha masomo ya ziada ambapo hali ya ufaulu ikaanza kupanda.
Anasema kwa sasa shule yao inatakribani wanafunzi 650 ambapo waliongezeka baada ya kupata msaada kutoka NELSAP ya uimarishaji ya miundombinu hiyo.
Anasema maboresho makubwa yamefanywa na LADP ambayo ni awamu ya kwanza na kufanya shule yao sasa kuwa na ufaulu mzuri katika Mkoa huo na kuonesha ni namna gani mazingira ya shule yanapoboreshwa yanaweza kubadilisha hali ya ufaulu kwa wanafunzi.
”Tunashukuru sana kwa hatua hii tumekuwa na umeme wa uhakika ambao haukatiki mara kwa mara ambapo ratiba zetu na kalenda ya shule inaenda kwa mujibu wa kanuni na taratibu za kitaaluma zilivyopangwa,”anasema .
*** Akizungumzia hali ya ufaulu baada ya ujio wa umeme.
Rwamtamo anasema baada ya kupata nishati hiyo ya umeme wameweza kujikuta katika mazingira yenye miundombinu mizuri na kujikuta wameweza kupandisha ufaulu wa kitaaluma kwa mwaka 2023.
Anasema kwa mwaka huo,Divisheni One ilikuwa na wanafunzi 99, Divisheni Two ilikuwa wanafunzi 100 ,Divisheni Three ilikuwa wanafunzi watano, huku kwa upande wa Divisheni four hawakuwa nayo wala sifuri
”Nawashukuru NELSAP kwa ujio wa miradi waliyotuletea hii ni hatua kubwa kwetu kujivunia na kuona namna tulivyotoka mwanzo na hadi sasa tulipo hali inayotia moyo ya kuhakikisha tunazidi kupanda kitaalum huku tukiendelea kushika nafasi za juu kimkoa hadi kitaifa,”anasema.
Akizungumzia miradi mingine iliyosaidiwa na NELSAP, anasema awali walikuwa na shida ya mabweni ambapo baada ya NELSAP na LADP awamu ya pili waliweza kupata bweni kubwa wenye uwezo wa kuhifadhi wanafunzi 80 pamoja na bwalo la chakula lenye uwezo wa kubeba wanafunzi 400 pamoja na kuwapatia Jengo la utawala la Ofisi ya shule hiyo.
”Niwashukuru NELSAP kwa kuweka shule yetu katika miundombinu mizuri, na kuifanya shule yetu kuzidi kukuwa kitaaluma na wanafunzi kuibua vipaji mbalimbali ikiwemo waimbaji,watangazaji pamoja na wanasheria,”anasema.
Aidha anawaomba wadau mbalimbali wa elimu kitaifa au kimataifa kuedelea kuishika mkono shule hiyo katika kutatua changamoto zao mbalimbali ikiwemo uhaba wa maabara ya Geographfia ,Kemistri,Fizikia na maabara nyingine.”Pia tunauhaba wa nyumba ya walimu ambapo hadi sasa tuna nyumba moja ya walimu ambayo inakaliwa na familia tatu hivyo bado tunauhitaji wa nyumba za walimu nyingine kwani shule yetu inawalimu wengi,”anasema na kusisitiza
”Pia tunaomba kusaidiwa Maktaba kwaajili ya wanafunzi kujisomea kwani bado hawana mahali pa kujisomea kwa kufanya hivyo tutakuwa tumesaidia eneo kubwa la Shule ya Ngara High School kitaaluma na kuzidi kuongeza hali ya ufaulu kwa wanafunzi wao kusoma katika mazingira mazuri.
Kwa Upande wake Mratibu wa Miradi ya Maendeleo ya Kijamiiupande wa Tanzania (LADP),Irene Chalamila anasema katika shule hiyo ya Ngara high School,LADP awamu ya kwanza imeweza kusaidia baadhi ya vitu mbalimbali ambapo tayari vimekamilika na vingine vinatarajia kukamilika katika LADP awamu ya pili.
Anasema miongoni mwa maeneo ambayo wamesaidia katika shule hiyo ni uwekaji wa umeme,mradi wa bwalo la kulia chakula,Ujenzi wa Bweni la kulala wanafunzi pamoja na Ujenzi wa jengo la utawala.
”Uamuzi wa kufikia hapa kuleta umeme umetokana na uchaguzi wa mradi wa LADP unafanyika kwa kushirikiana na wananchi kwa kutambua vipaumbele vyao sehemu gani ambazo zinachangamoto na namna ya kuzitatua,”anasema na kuongeza
”Hivyo kwa shule ya Ngara high school ilionekana wanafunzi wanamazingira magumu sana ya kusomea kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo Umeme ndio tukaona tulete umeme ambao umeunganishwa katika shule hii na grid ya taifa kwa LADP awamu ya kwanza,”anasema .
Anasema umeme walioweka umetoka Kilometa 3.4 kutoka barabarani hadi shuleni na waeweza kusambaza nyaya zenye urefu wa nusu kilomita ambazo zimepita katika shule na kuunganisha majengo mbalimbali ya shule ambapo gharama ya mradi huo ni zaidi ya milion 195,636,344.
Chalamila anasema pamoja na kuleta mabadiliko katika shule yao pia umeme umeweza kuimarisha hali ya Ulinzi na usalama katika mazingira ya shule,ufanyaji kazi na usomaji kwa wanafunzi ambapo imeweza kulea hali ya ufaulu kuwa juu tangu matokeo ya mwaka 2023.
Anasema baada ya kukamilisha LADP awamu ya kwanza pia bado kukaonekana bado kunachangamoto sehemu za kula chakula kwa wanafunzi na sehemu ya kulala hivyo katika Mradi wa LADP awamu ya pili NELSAP imeamua kuendelea kuboresha maeneo hayo ili kuhakikisha wanawatengenezea maeneo bora ya kulala na kula wanafunzi wa shule hiyo.
”Kuna mradi wa bwalo la chakula la wanafunzi ili wasiendelee kula katika miti pamoja na bweni ilikuondoa msangamano wa wanafunzi kulala sehemu moja na kuondoa mrundikano tumeamua awamu ya pili ya Miradi yetu ya Maendeleo kuwajengea majengo hayo ili kupata sehemu nzuri ya kulala na maeneo mazuri tulivu na kujisomea.
”Pia tuliona hakuna jengo zuri la walimu ambalo wangeweza kukaa vizuri na kufanya kazi kwa weledi na kutunza nyaraka zao vizuri nalo katika awamu ya pili ya LADP tumeona kuwajengea jengo la Utawala ili nao wapate eneo zuri la kukaa na kufanya kazi,”anasema.
Naye Mmoja wa wanafunzi wa Shule hiyo kidato cha Sita ,Daniel James anasema shule yao ilikuwa na changamoto sana kabla ya NELSAP kuwapatia misaada hiyo mbalimbali kwani ilikuw haina umeme wala mabweni ya kutosha hivyo kusoma kwa changamoto.
”Kabla hatujafika katika shule hii,tulikuwa tunapata changamoto nyingi ya kujisomea,kulala katika bweni moja wanafunzi wengi hali ilifanya wanafunzi wengine kulala chini na wengine kulala wawili wawili kwa kitanda kimoja,”anasema.
Geofrey Mbissa Mwanafuzi wa Shule hiyo Kidato cha Sita HGL anasema wakati umeme ulipokuwa haujafika usalama wao ulikuwa hafifu sana ambapo walikuwa wanakumbana na viumbe mbalimbali ambavyo vilikuwa hatarishi kwao.
Anasema kwasasa wanaishukuru NELSAP kwa kuwasaidia umeme ambao wanapata nyakati zote hata usiku na kuwa huru kutembea kwenda madarasani kujisomea tofauti na miaka ya nyuma umeme kusipowaka uwa wanalala mabwenini.
More Stories
Ubunifu wa Rais Samia kupitia Royal Tour unavyozindi kunufaisha Tanzania
Rais Samia anavyojenga taasisi imara za haki jinai kukabilina na rushwa nchini
Rais Dk. Samia alivyowezesha Tanzania kuwa kinara usambazaji umeme Afrika