Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.
Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (NEC) imepokea na kujadili kwa kina taarifa ya makubaliano ya uwekezaji na uendeshaji wa bandari baina ya Serikali ya Tanzania na ya Dubai na kubariki mchakato huo.
Taarifa iliyosomwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi,Sophia Mjema,mbele ya waandishi wa habari imesema kuwa NEC Katika kikao chake kilichoketi makao makuu ya CCM, jijini Dodoma leo Jumapili Julai 9, 2023 chini ya Mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan, kikao hicho kimesema uwekezaji na uendeshaji wa bandari ni kwa manufaa ya uchumi wa nchi.
Imesema kuwa uwekezaji huo ni utekelezaji wa vitendo wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020/25, Ibara ya 59, ukurasa wa 92.
Hivyo Mjema amesema kuwa kikao hicho kimekubaliana kuwa, Serikali iendelee kutoa elimu kwa wananchi katika jambo hilo.
“Serikali iongeze kasi ya kutoa elimu kwa wananchi juu ya uhalisia uliomo katika makubaliano ya uwekezaji na uendeshaji huo wa bandari,”amesema Mjema.
Pamoja na hayo Mjema amesema kuwa NEC imezipongeza Serikali zote mbili za Chama Cha Mapinduzi, Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kuendelea kutafsiri kwa vitendo Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025 kwa maslahi na ustawi wa watanzania wote.
More Stories
Wassira:Waliopora ardhi za vijiji warudishe kwa wananchi
Rais Samia apongezwa kwa miongozo madhubuti ya ukusanyaji wa kodi
Mwenda:Siku ya shukrani kwa mlipakodi ni maalum kwaajili ya kuwatambua,kuwashukuru