May 6, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ndoa za utotoni kikwazo kufikiwa usawa wa kijinsia

Judith Ferdinand  

Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa yanatoa wito wa usawa wa jinsia, huku lengo namba 5.3, likitoa wito mahususi kukomeshwa kwa mila potofu ifikapo mwaka 2030, zikiwemo ndoa za utotoni na za kulazimishwa.

Hata hivyo, malengo hayo yanaweza yasifikiwe endapo wito huo hautafanyiwa kazi ya kukomeshwa kwa ndoa za utotoni. Kauli hii inajidhihirisha kupitia wanafunzi wa shule ya sekondari Bugogwa na Kayenze, zilizopo wilayani Ilemela mkoani Mwanza, wakieleza namna ndoa hizo zinavyoweza kukwamisha jitihada za kufikia usawa wa kijinsia. 

Ninawasili kwenye shule ya sekondari Bugogwa, ninapokewa na ujumbe unaosomeka, “Ukiacha nisome, itapendeza.” Safari yangu inaishia kwenye ofisi ya Mkuu wa shule ya sekondari Bugogwa, napokewa na Mwalimu wa Taaluma, tunafanya mazungumzo kisha ananipa ruhusa ya kuzungumza na wanafunzi wa kike, baada ya kujitambulisha, mazungumzo yetu yaanza.

Huyu ni Nenetwa Ngedele, anaeleza ndoa za utotoni zinavyokwamisha kufikia malengo ya usawa wa kijinsia na kusababisha kuwa na taifa lenye wanawake ambao kiwango chao cha elimu kipo chini au ambao hawajasoma, hivyo kuishia kufanya shughuli ambazo hazihitaji elimu.

Mfano halisi wa hali hii ni simulizi ya Kokusima Mukama siyo jina lake halisi mwenye umri wa miaka 22, mkazi wa Kayenze wilayani Ilemela, mama wa watoto wawili. Binti huyu aliyekuwa na ndoto za kuwa mwalimu.

Ndoto hiyo haikuweza kufikiwa na kulazimika kukatisha masomo akiwa darasa la pili baada ya baba yake kuitelekeza familia na mama kushindwa kukidhi mahitaji. Kutokana na hali ngumu ya maisha, katika harakati za kujikwamua kutoka kwenye hali hiyo alikutana na mwanaume ambaye ana umri wa miaka 32 kwa sasa anajishughulisha na uvuvi, aliyemrubuni na kujikuta akiingia naye kwenye ndoa akiwa na umri wa miaka 15.

Kokusima anasimulia kwamba analazimika kuuza karaga kwa ajili ya kusaidia kipato cha familia pamoja na kueleza kuwa hawezi kufanya shughuli zaidi za kitaalamu isipokuwa ambazo hazihitaji elimu ambazo kwa asilimia kubwa hufanya uchumi wake kuwa wa chini.

Kisa cha Kokusima kinaonesha picha halisi pamoja na kuunga mkono hoja ya tafiti mbalimbali zilizofanyika duniani, zikieleza kuwa moja ya athari za ndoa za utotoni ni pamoja na kukosekana kwa haki ya mtoto kupata elimu. Utafiti huo unaeleza, msichana akibaki shuleni kwa muda mrefu, anapunguza uwezekano wa kuolewa akiwa chini ya umri wa miaka 18 na kuzaa watoto katika miaka ya utotoni. Zaidi ya asilimia 60 ya mabibi harusi katika nchi zinazoendelea hawana elimu rasmi.

Tafiti hizo zinaeleza kuwa wanawake walioolewa utotoni, kuna uwezekano mdogo wa kupata kazi ya kitaalam au inayohitaji ujuzi. Hali hiyo inamfanya kuwa na uwezekano mkubwa wa kufanya kazi za kilimo ambazo aghalab huhitaji ujuzi mkubwa. Utafiti huo pia unaonesha kuwa wanawake sita kati ya 10, sawa na asilimia 60, walioolewa wakiwa na umri wa chini ya miaka 18, walijishughulisha zaidi na kazi za kilimo ikilinganishwa na wanawake wa wanne kati ya 10 sawa na asilimia 39 ambao waliolewa wakiwa na umri wa miaka 20 au zaidi. Hawa walifanya kazi za kitaalam zaidi na walikuwa na elimu kubwa zaidi.

Fibi Ilelema mwanafunzi wa shule ya sekondari Bugogwa, katika kusisitiza umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike anahoji kuwa kama Rais Samia Suluhu Hassan, angeliolewa akiwa na umri mdogo, taifa lingempata Rais mwanamke? Aidha, anahoji kama Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt. Angeline Mabula, angeliingia kwenye ndoa za utotoni taifa lingempata wapi na kumtumia katika nafasi ya ubunge, unaibu waziri na waziri?

Kauli ya binti huyo inaungwa mkono na Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dkt. Alex Malasusa, wakati akifungua mafunzo kwa waandishi wa habari 31 kuhusu ndoa za utotoni, chini ya mradi wa ‘Hapana Marefu Yasiyokuwa na Mwisho’ unaotekelezwa na kanisa hilo wenye kauli mbiu isemayo, ‘Ndoa za utotoni, sasa mwisho.’

Askofu Malasusa anasema ndoa za utotoni zinapoteza uelekeo wa mtoto wa kike huku akitolea mfano mtoto aliyeokolewa kwenye ndoa za utotoni wilayani Kwimba mkoani Mwanza, ambaye ameendelea na masomo ya uhandisi wa meli ‘Marine Engineering’, kama binti huyo asingeokolewa kwenye janga la ndoa ya utotoni asingelifikia hatua ya kusoma masomo ya kuwa mhandisi.

Majira pia ilibisha hodi shule ya sekondari Kayenze baada ya kutoka shule ya sekondari Bugogwa, hapa ninapokewa na Kaimu Mkuu wa shule hiyo, ninajitambulisha na kuanza mazungumzo kisha anawaita wanafunzi wa kike. Katika mazungumzo nao wanaeleza ndoa za utotoni kuwa ni kikwazo cha kutoa fursa sawa kwa mabinti kama wanavyonufaika wavulana.

Mmoja wa wanafunzi wa shule ya sekondari Kayenze, Belina Anthon, anasema wasichana wanaoolewa wakiwa wadogo mara nyingi hulazimika kuacha shule. Anaeleza kuwa bila elimu, wasichana wanakosa maarifa, stadi na fursa za kiuchumi ambazo zingeliwasaidia kushindana kwa usawa na wanaume katika soko la ajira au uongozi.

Belina anasema wanawake waliokatiza ndoto zao wakiwa watoto kutokana na ndoa za utotoni, mara nyingi hukwama katika utegemezi wa kifamilia. Hali hii huzuia ushiriki wao kwenye uchumi wa taifa, hivyo kudhoofisha juhudi za kufikia uwakilishi sawa wa kijinsia.

Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa za Benki ya Dunia, ndoa za utotoni hupunguza kipato cha mwanamke katika maisha yake kwa asilimia tisa pale wanapoolewa mapema na kuacha shule.

Naye Neema Mwita mwanafunzi wa shule ya sekondari Kayenze, anasema wasichana waliolazimishwa kuolewa mapema hupoteza fursa ya kuwa viongozi, hali inayozidi kuwapa unyonge hivyo kushindwa kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za kisiasa.

Kauli ya Neema inaungwa mkono na mmoja wa wananchi wa Kayenze Mashaka Masanja, anayesema wanawake ambao walikosa fursa ya kupata elimu kutokana na ndoa za utotoni, watajikuta wakitegemea zaidi nafasi za upendeleo katika uongozi mbalimbali hususani za kisiasa kama viti maalum.

“Kwa kawaida vigezo vya kuwania nafasi mbalimbali za uongozi za kisiasa nchini zinataka mtu awe anajua kusoma na kuandika, hivyo kama mwanamke alikatisha masomo au alimaliza kidato cha nne, lakini hakupata fursa ya kuendelea zaidi, ataishia kupata nafasi za Ubunge na Udiwani, lakini hataweza kupata fursa zaidi ya kuwa waziri mkuu, waziri au naibu waziri, mkuu wa mkoa au wilaya na nafasi nyingine nyingi zinazohitaji mtu ambaye amepata fursa ya elimu ya juu zaidi,” anasema na kuongeza:

“Hali hiyo itafanya baraza la mawaziri kukosa usawa wa kijinsia, kwani litakuwa na wanaume wengi, hivyo kufanya wanawake kukosa sauti katika ngazi za juu zaidi za maamuzi na uongozi, hivyo moja kwa moja malengo ya usawa wa kijinsia hayatofikiwa.”

Pia Neema anasema ndoa za utotoni husababisha mimba za mapema ambazo ni hatari kiafya, huzidisha msongo wa mawazo, na afya duni huathiri uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kijamii, kisiasa na uchumi hivyo kuchochea umaskini katika familia.

Mtaalam wa mafunzo mradi Hapana Marefu Yasio na Mwisho, Mchungaji wa KKKT Dayosisi Mashariki ya Ziwa Victoria, Julia Gabriel, anaelezea kisa cha binti ambaye aliozeshwa akiwa na umri mdogo, kisha akapata mimba ambayo kwake ilikuwa ni shida. Baada ya kuzaa alizira kumnyonyesha mtoto, kwani akili zake zilikuwa bado ni za kitoto, kunyonyesha kwake ilikuwa ni kero na vurugu. Kiakili hajakaa sawa, mwisho wa siku mwanaume kamrudisha kwao kwani aliona hafai kuwa mke tena.

“Binti kakosa fursa ya elimu, akili imevurugika, karudishwa kwao akiwa na mtoto na familia yake ina hali duni, hivyo kaenda kuongeza mzigo kwa familia na kuchochea umaskini zaidi, familia kile ilichokipata haijakifaidi, wamemuingiza mtoto kwenye maumivu ya kisaikolojia, pengine ingemuacha akasoma angekuwa msaada kwenye familia,” anasema Mchungaji Julia.

Akizungumza na Majira, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Afya ya Uzazi, Mratibu wa Huduma ya Fistula kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, Dkt Elieza Chibwe, anasema mbali na athari za kiafya pia ndoa za utotoni zinatengeneza jamii maskini kwa aslimia 100, kwa sababu anakuwa hajapata fursa ya kuendelezwa kiuchumi ili kuweza kushindana kwenye soko la ajira. 

“Kutakuwa na taifa lenye wanawake tegemezi wasioweza kuchangia uchumi wa taifa, kutokana na madhara atakayoyapata baada ya kuozeshwa kati umri mdogo. Binti akipata ugonjwa wa fistula umaskini unaongezeka. Akitolea mfano, labda alikuwa na biashara ya kupika vitumbua ni nani atakayekwenda kununua kitumbua au bidhaa kwa mtu anayetokwa na haja ndogo au kubwa mfukulizo hali hiyo hufanya uchumi kushuka,” anasema na kuongeza:

“Ataathirika kisaikolojia kwani atashindwa kushiriki shughuli mbalimbali ikiwemo ibada, misiba, mikutano ya kujadili maendeleo ya taifa au kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.” 

 Kaimu Mkuu wa shule ya sekondari Kayenze, Noel Zaidi, anasema malengo ya usawa wa kijinsia yanaweza yasifikiwe kwa sababu binti akiishaingia kwenye ndoa katika umri mdogo anakuwa amezingirwa na majukumu ya kifamilia. Anafafanua kuwa ukitazama uhusiano ulivyo na mfumo dume kwa Kanda ya Ziwa, binti huyo hataweza kupata fursa ya kushiriki katika ngazi za maamuzi kuanzia ndani ya familia.

“Hali hiyo itamfanya mwanamke hata akiwa mkubwa kukosa ujasiri wa kukabiliana na wanaume kutokana na kutokuwa na elimu ambayo kwa kiasi kikubwa ingempa nguvu ya kuweza kukabiliana na vikwazo hivyo kuwa na uwezo wa kushindana katika fursa mbalimbali ikiwemo za ajira na uongozi.”

Naye Mwalimu wa Taaluma wa shule ya sekondari Bugogwa,Tumaini Kabila, anasema ndoa za utotoni zinarudisha nyuma jitihada za kufikia usawa wa kijinsia kwani zinasababisha taifa kupoteza nguvu kazi ya jinsi ya kike licha ya uzoefu kuonesha kuwa wana mchango mkubwa katika maendeleo akitoa mfano wa Rais Samia ambaye anaongoza nchi ijapokuwa ni mwanamke.

Diwani wa Kata ya Kayenze, Issa Mwalukila, anaeleza kuwa ndoa za utotoni zinakwamisha malengo ya usawa wa kijinsia kwa sababu zinafifisha ndoto za mabinti walio wengi, hivyo kushindwa kufikia zile fursa anazoweza kupata mwanaume ikiwemo za kielimu, ajira hata uwakilishi ndani na nje ya nchi. 

Anasema suala hilo lina athari kwa walengwa na taifa kwani mzigo wa utegemezi utakuwa mkubwa kutokana na kuzalisha wanawake ambao hawana uwezo wa kuzalisha mali kitaalam.

Taarifa ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) zinaonesha kwamba asilimia 21 ya wanawake vijana huolewa kabla ya kufikia umri wa miaka 18. Hii inamaanisha kuwa wanawake milioni 650 wameolewa chini ya umri unaotakiwa, sawa na wanawake milioni 12 kila mwaka duniani, idadi hii kubwa ya ndoa za utotoni takribani asilimia 37 zinatokea barani Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara.

Taarifa hizi ni kilelezo cha ukubwa wa tatizo jinsi idadi kubwa ya wanawake wanapoteza fursa za kupata elimu kutokana na ndoa za utotoni, hivyo kuwa kikwazo cha kufikia malengo ya usawa wa kijinsia kwani elimu ndio msingi wa kuwakwamua wanawake ili wafikie fursa mbalimbali kama ajira bora, uchumi, siasa na maendeleo kama ilivyo kwa wanaume.