December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ndoa za utotoni chanzo cha ugonjwa wa fistula

Judith Ferdinand,TimesMajira online

Ndoa za utotoni zinatajwa kusababisha athari kwa watoto wa kike kisaikolojia,kiafya,kiuchumi na mengineyo.

Athari za afya tunaona kwa namna gani ndoa hizo za utotoni zinavyoweza kusababisha binti kupata ugonjwa wa fistula ya uzazi ambao ni jeraha kubwa linalopatikana wakati wa kujifungua.

Jeraha hilo humpokonya mwanamke au msichana afya yake, haki na utu,ni shimo linalotokea kati ya njia ya uzazi na kibofu na kusababisha kutodhibitiwa kwa haja ndogo.

Pia shimo hilo lililo kati ya njia ya uzazi na njia ya haja kubwa husababisha kinyesi kupita bila kizuizi.

Sababu au chanzo cha mtu kupata fistula ni mama kupata uchungu kwa muda mrefu kabla ya kujifungua pamoja na kutokuwa na uwiano kati ya njia ya uzazi na ukubwa wa kichwa cha mtoto.

Shinikizo la muda mrefu linalotokana na kichwa cha mtoto kwenye njia ya uzazi ya mama kushindwa kusambaza damu na kusababisha mishipa kufa na kuanguka na baada ya kuanguka shimo linalojitokeza linaitwa fistula.

Fistula ya uzazi inachangia asilimia 8 ya vifo vya uzazi, na asilimia 90 ya visa vya kujifungua watoto wafu huku wataalamu wakieleza kuwa watoto wa kike waliopo kwenye ndoa za utotoni wapo hatarini zaidi kupata ugonjwa huo.

Waathirika wa ndoa za utotoni na changamoto ya fistula

Majira lilipata fursa ya kutembelea Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando na kuzungumza na waathirika wa ugonjwa wa fistula miongoni mwao ni waathirika wa ndoa za utotoni.

Kokuteta Shukuru (18)siyo jina lake halisi mkazi wa Meatu mkoani Simiyu,aliolewa akiwa na umri wa miaka 17 kasoro huku mumewe akiwa na umri wa miaka 21.

Akizungumza na Majira akiwa katika wodi ya wagonjwa wa fistula kwenye hospitali hiyo ya Rufaa ya Kanda akipatiwa matibabu ya ugonjwa huo, anaeleza kuwa alisoma hadi darasa la saba na baada ya kuhitimu elimu hiyo ya msingi hakubahatika kuchaguliwa kuendelea na elimu ya sekondari na kuamua kuolewa.

Baada ya miezi mitatu ya ndoa alipata ujauzito na kuendelea kuhudhuria kliniki lakini ilivyofika siku ya kujifungua uchungu ulianza saa moja asubuhi hadi saa moja jioni.

“Ilipofika saa 5 usiku nikaanza kusukuma lakini mtoto akawa hatoki,wakanipeleka chumba cha upasuaji na kufanyiwa upasuaji, wahudumu wa afya walifanikiwa kuokoa maisha yangu lakini mtoto alifariki,”anaeleza Kokuteta na kuongeza; 

“Nilikaa hospitalini kwa wiki tatu baada ya hapo nikatolewa mpira wa kupitisha haja ndogo lakini ilianza kutoka mfululizo hivyo wakaniwekea tena mpira,haja ndogo ikawa inapita pembeni ya mpira siyo ndani ya mpira,”.

“Kutokana na hali hiyo nilipewa rufaa ya kuja Bugando kutoka Simiyu ambapo nilikaa wiki moja ndio wakanifanyia upasuaji baada ya kugundua nasumbuliwa na ugonjwa wa fistula,” 

Anaeleza sababu za kutoendelea na elimu ya sekondari

Kokuteta anaeleza kutofaulu katika mitihani yake kulichangia yeye kushindwa kuendelea na masomo ya sekondari hivyo kuamua kuolewa.

Ananasema anachohitaji kwa sasa ni kupata mtoto mwingine baada ya mtoto wake wa kwanza kuzaliwa akiwa amefariki hali inayomuumiza kama mama.

Nini ilikuwa ndoto yake

Anaeleza kuwa ndoto yake alikuwa anatamani akimaliza masomo awe muuguzi ingawa kwa sasa baada ya kuingia kwenye ndoa hatamani tena kusoma.

Naye Agnes Lucas (18)siyo jina lake halisi ,mkazi wa Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera, anaeleza kuwa aliingia kwenye ndoa za utotoni akiwa na umri wa miaka 16 baada ya kuacha shule akiwa darasa la sita.

Nini kilisababisha kuingia kwenye ndoa za utotoni

Agnes anaeleza kuwa siku moja akiwa anatoka shule alikutana na mwanaume ambaye alimtongoza naye akubali na kuamua kwenda kuishi naye.

“Mimi mwenyewe ndio niliamua kutoroka kwenda kuishi na mwanaume na kuacha shule bila ridhaa ya wazazi wangu,” anaeleza.

Baada ya miezi mitano alibeba mimba, muda wa kujifungua ulipofika,uchungu ulianza asubuhi na ilipofika majira ya mchana ndipo akaenda hospitalini, kila alipojaribu kusukuma mtoto alikuwa hatoki na baada ya vipimo mtoto alionekana amekaa vibaya.

“Walinipeleka chumba cha upasuaji na walifanikiwa kumtoa mtoto akiwa hai,niliendelea kukaa hospitalini kwa muda wa wiki moja kisha wakanitolea mpira wa haja ndogo na kurudi nyumbani,”anaeleza Agnes.

Baada ya siku nne tangu atoke hospitali alianza kuona haja ndogo inatiririka bila mpangilio hivyo alirudi hospitalini ambapo alielezwa kuwa anapaswa kwenda Mwanza Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando.

“Nilivyofika hapa Bugando wakanifanyia upasuaji kwani nilibainika kuwa na fistula,kwa mujibu wa daktari ilitokana na mimi kuwa na umri mdogo na nikabeba mimba,”.

Alitoa wito kwa mabinti wenzake wahakikishe wanasoma ili kutimiza ndoto zao na kuepuka kuingia kwenye ndoa za utotoni ambazo zinasababisha kupata madhara mbalimbali ukiwemo ugonjwa wa fistula.

Kwa upande wake mama mzazi wa Agnes Lucas, anaeleza kuwa binti yake baada ya kujifungua na kukaa siku chache alianza kutokwa na haja ndogo mfululizo,alimpeleka zahanati mbalimbali huko kijijini kwao na kupewa vidonge pamoja na kudungwa sindano bado hakupata nafuu.

“Nikawa najiuliza huyu mtoto amekuwaje, nikaamua kumpeleka hospitali ya Kayanga,wakampima na kumuwekea mpira wa haja ndogo kisha tukarudi nyumbani kutafuta fedha na baada ya wiki mbili nikampeleka hospitali ya Nyakahanga,baada ya kufika hapo waliniambia nimpeleke Bugando,” anasema mama huyo.

Alipewa barua ya kumleta Bugando na alipofika katika hospitali hiyo aliambiwa binti yake amepata fistula na hivyo matibabu yake ni kufanyiwa upasuaji.

Changamoto baada ya binti yake kupata fistula

Mama wa Ages anaeleza changamoto ni pamoja na uchumi wa familia kuyumba kwani alitumia muda mrefu kumhudumia mwanaye na mjukuu wake,isitoshe mumeke alifariki baada ya binti yao kufikisha miezi miwili na nusu tangu kujifungua ambapo mjukuu wake amefikisha miezi nane tangu azaliwe.

Akizungumzia hali ya binti yake kukimbilia kuolewa na kukatisha masomo anaeleza kuwa, kama mzazi hakujisikia vizuri na ni jambo la kusikitisha kwa sababu matarajio ya familia ni kuwa aje kuwa msaada kwa wenzake.

“Nilikuwa nategemea mwanangu atakuja kunisaidia badala yake amegeuka kuwa mzigo maana kapata fistula ingawa amepatiwa matibabu, hivyo mzigo wote wa kumlea yeye pamoja na mtoto wake upo juu yangu na isitoshe kuna wadogo zake nao wananitegemea huku kipato changu kikiwa duni,na huko alikoolewa ni kama wamemtelekeza,”anaeleza.

Daktari Bingwa wa magonjwa ya wanawake na afya uzazi anena juu ya fistula

Akizungumza na Majira ofisini kwake,Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Afya ya Uzazi,Mratibu wa Huduma ya Fistula wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando,Dkt Elieza Chibwe anaeleza kuwa fistula ya uzazi ni tundu ambalo halitakiwi kuwepo,linalotokea kati ya kibofu cha mkojo na uke pia njia ya haja kubwa.

Tundu hilo husababisha mgonjwa wa fistula kutokwa na haja ndogo au kubwa mfululizo kupitia tundu hilo kwa sababu anashindwa kuuzuia.

Dkt Chibwe anaeleza kuwa,asilimia 85 ya wagonjwa wote wa fistula wanapata shida ya kutokwa haja ndogo muda wote kwa sababu wanashindwa kuuzuia.

Nini kinachosababisha ugonjwa wa fistula

Dkt.Chibwe anaeleza sababu kubwa ya fistula ni uchungu pingamizi anaokutana nao mama mjamzito ambaye amefikia muda wa kujifungua lakini kutokana na sababu nyingi ikiwemo tamaduni, umbali mrefu kutoka sehemu alipo hadi kwenye huduma za afya na kuchelewa kupata huduma.

“Tamaduni kwa maana kwamba kule kijijini kuna akina mama wazee ambao ni wakunga na kazi yao ni kuzalisha lakini hawana ujuzi,ikitokea shida hawezi kufanya jambo jingine hivyo kukaa na mjamzito muda mrefu na wakati mwingine kutokuwa na uwiano kati ya kichwa cha mtoto na nyonga ya mama,”anasema mtaalamu huyo wa magonjwa ya wanawake na kuongeza

“Hivyo inafika mahali mtoto anakwama na kwenye nyonga kuna mifupa pia kichwa cha mtoto kina mfupa kinakwenda kukandamiza uke na kibofu cha mkojo kwa muda mrefu.”

Anasema hali hiyo usababisha sehemu iliyokandamizwa kukosa damu,hivyo pana kufa na kutengeneza kidonda na zile nyama nyama zinaachia na kufanya tundu ambalo litasababisha haja ndogo au kinyesi kuendelea kutoka bila kujizuia.

Ndoa za utotoni,mimba za utotoni zinavyochangia fistula

Dkt.Chibwe anaeleza kuwa,wagonjwa wengi wa fistula ni wasichana wenye umri chini ya miaka 20,sababu nyingi za kupata ugonjwa huo kwanza ni ya kibaiolojia, maumbile yao yanakuwa bado hayajakomaa.

Kwa hiyo kumpata binti mjamzito mwenyewe umri wa miaka 15,16 na 17,uwezo wake wa kujifungua ni mdogo kwa sababu nyonga zake zinakuwa bado ndogo na hazijakomaa.

Dkt. Chibwe anasema watoto hao wa kike wakipata uchungu pingamizi bila msaada asilimia kubwa wanapata fistula pia njia na ukubwa wa kichwa cha mtoto kunakuwa hakuna uwiano kwani wasichana hao wadogo maumbo yao yanakuwa madogo mfano ukiwa na binti wa miaka 17 na wa miaka 25 wote ni wajawazito na wanatazamia kujifungua watoto wenye kilo tatu.

“Mwenyewe miaka 25 ana uwezekano mkubwa wa kujifungua mtoto akiwa salama kuliko mwenye umri wa miaka 17,kwa sababu yule ameisha kuwa mkubwa na viungo vipo tayari na kati ya hao mwenye uwezekano mkubwa wa kupata fistula ni huyo wa miaka 17,”anafafanua.

Sababu ya pili ni watoto hao kutokuwa uamuzi kwani bado wanategemea uamuzi kutoka kwa waume zao,familia,wazazi na jamii wakati wa kujifungua.

“Mtoto wa miaka 15 hana maamuzi akienda ukweni mama mkwe anamwambia yeye watoto aliwazalia nyumbani na yeye binti anaweza kujifungulia nyumbani kwa sababu hana uamuzi wowote na kutokana na umri wake mdogo hupata shida, pia wagonjwa wa fistula tunaowaona huko wodini tunawaita mashujaa maana wengi wao wanakufa kwa sababu ya hiyo vita ya uzazi,”anaeleza Dkt.Chibwe.

Pia kutokuwa na uwezo wa kiuchumi huchangia kutokwenda kliniki au kuwa na mahudhurio machache,ikumbukwe kuhudhuria kliniki kunamsaidia kupata vitu vingi,kwa hiyo anakuwa hajaandaliwa,hajapimwa na wala hawajui maendeleo ya mtoto tumboni au afya yake mama au kama mtoto huyo anaweza kujifungua kawaida.

“Mtu yoyote anaweza asijifungue kawaida lakini binti mdogo uwezo wa kwenda kutafuta huduma za afya hana,kwanza kiuchumi bado hapati msaada hivyo wengi wao wanaishia kupata fistula,na fistula inayowapata watoto ni mbaya kuliko ya watu wazima kwa sababu inasababisha washindwe kutembea,” anasema.

Mabinti wa miaka 16 hadi 18 wanaopata fistula wengi watoto wao wanakufa,ni ugonjwa unaomfanya aaibike pia ni kujenga taifa la wanawake tegemezi wasioweza kuchangia uchumi wa taifa kutokana na madhara watakayoyapata baada ya kuozeshwa katika umri mdogo.

“Alikuwa na ndoto zake akihitimu shule angefanya vitu vingi lakini unamuozesha mapema na mtu ambaye hampendi,kabeba mimba,kateseka miezi tisa, kapata uchungu pingamizi,kakosa mtoto na kapata fistula ugonjwa wa kumuaibisha,na ukienda ndani zaidi kwenye jamii kwa binti aliyepata ugonjwa wa fistula wanaona kama ni laana hivyo anaweza kuachika,” anaeleza Dkt.Chibwe.

Anaeleza kuwa mbali na athari za kiafya,kuna athari nyingine ambapo ukiwa na binti wa miaka chini ya miaka 18 na hajaendelea kielimu unakwenda kutengeneza jamii maskini kwa asilimia 100.

Pia baada ya mama au binti kupata fistula umaskini unaongezeka,mfano labda alikuwa na biashara ya kupika vitumbua, ni nani atakaye kwenda kununua kitumbua au bidhaa kwa mtu anayetokwa na haja ndogo au kubwa mfululizo, hali hiyo hufanya uchumi wake kushuka.

Aidha wana athirika kisaikolojia na watashindwa kushiriki shughuli mbalimbali ikiwemo ibada,misiba,wanaume zao wana waacha na watoto wanateseka kwa wale ambao wamefanikiwa kujifungua watoto wakiwa hai.

Idadi ya wagonjwa wa fistula kwa mwezi

Dkt.Chibwe anaeleza katika Hospitali hiyo ya Rufaa ya Kanda Bugando,kwa mwezi wanapokea wagonjwa zaidi ya 20 wa fistula na kila wiki wanawafanyia upasuaji wagonjwa 8 ikiwemo wasichana wenye umri chini ya miaka 18 waliopata ugonjwa huo kutokana na kubeba mimba katika umri mdogo.

Nini kifanyike kuzuia fistula kwa watoto wa kike

Dkt.Chibwe, anaeleza suluhisho la kutokomeza fistula kwa mabinti wadogo ni kutokomeza ndoa za utotoni ambazo mara nyingi zinachangia mtoto wa kike kubeba mimba katika umri mdogo wakati ambao viungo vyake vya uzazi vinakuwa havijakomaa.

Watoto wapitie hatua zote za ukuaji ili baadaye wawe msaada kwa familia,jamii na taifa,wahudumu wa afya waongezwe katika vituo vya kutolea huduma na elimu sahihi ya afya ya uzazi itolewe.

Watoto hao wa kike wakipitia hatua zote za ukuaji zinazotakiwa ikiwemo kwenda shule itasaidia kupunguza tatizo hilo la fistula kwa binti wa miaka chini ya 18 kuolewa na kupata ujauzito wakati wenzake wapo sekondari.

“Tutengeneze taifa ambalo wanawake wanaweza kujitegemea kiuchumi na kimaamuzi,hicho ni kitu cha msingi na watoto wetu waende shule,” anashauri Dkt. Chibwe.

Pia wajawazito wahudhurie kliniki kwani kuna uwezekano mkubwa wa kutopata ugonjwa wa fistula,ikitokea mtu kaupata ugonjwa huo aende hospitali kwa matibabu bila malipo (hutolewa bure).