Judith Ferdinand,Timesmajira Online,Mwanza
Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT),Askofu Dkt. Alex Malasusa,amesema ndoa za utotoni zinachangia uwepo wa talaka nyingi nchini,hivyo ametoa wito kwa jamii kuhakikisha suala la ndoa hizo linafikia mwisho kwa ajili ya ustawi wa taifa na watoto hususani wa kike ambao ndio waathirika zaidi.
Askofu Malasusa,ametoa kauli hiyo Januari 20,2025,wakati akifungua mafunzo kwa waandishi wa habari 31 kutoka mikoa na vyombo mbalimbali nchini,kuhusu ndoa za utotoni,yanayofanyika mkoani Mwanza kwa siku tatu,chini ya mradi wa hapana marefu yasiyokuwa na mwisho, unaotekelezwa na KKKT wenye kauli mbiu isemayo,”Ndoa za utotoni,sasa mwisho”.
“Wito wangu kwa jamii ya Watanzania,sasa suala la ndoa za utotoni lifike mwisho kwani zinaondoa upendo,ndio maana tuna tatizo kubwa la talaka nchini,kwa sababu mmoja wa wana ndoa,hawakua na uamuzi wa kuingia katika ndoa.Sisi viongozi wa dini lazima tuone kama Biblia inavyosema, ndoa na iheshimiwe,sasa watoto wengi wanasukumwa katika ndoa na hawana uhuru wa kuingia katika ndoa.,”amesema Askofu Malasusa na kuongeza:
“Sheria zipo lakini kila siku wazazi wanabuni mbinu mpya ikiwemo kuwataka watoto wao wajifelishe ili waende kuwaoza,waandishi wa habari ibueni hayo mambo na ikiwezekana tuleteeni viongozi wa dini,kwamba mzazi fulani amefanya hiki na hiki,na mimi nitakuwa mstari wa mbele,kusimama na kwenda kuwatoa watoto hao,kwani Tanzania tumefanikiwa mambo mengi na hili Waandishi wa habari mkilichukulia kwa nguvu tutafanikiwa,”.
Askofu Malasusa,amesema pia ndoa za utotoni zinapoteza uelekeo wa mtoto wa kike huku akitolea mfano mtoto aliyeokolewa kwenye ndoa za utotoni wilayani Kwimba mkoani Mwanza, ambaye ameendelea na masomo ya Uhandisi wa Meli “Marine Engineering”,ambapo kama kungekuwa hakuna watu wa kumuokoa taifa lingempoteza Mhandisi wa baadae.
“Watoto waendelee kufundishwa juu ya haki zao ili waweze kujitetea wenyewe na kujisimamia na kujua kuwa wanamaisha zaidi kuliko kukimbilia kwenye ndoa.Ni jambo la aibu mtoto kuolewa katika umri mdogo ambapo wazazi hasa wa kiume wanaona watoto wa kike kama rasirimali za kiuchumi na kupigia hesabu ana watoto wangapi ambao wataolewa ili pate mahari,”.
Msimamizi Mkuu,program ya maisha endelevu na uwezeshaji KKKT,Patricia Mwaikenda,amesema maisha ya ndoa za utotoni yamekuwa safari ndefu katika nchi nyingi ikiwemo Tanzania.Ambapo safari hiyo imeanzia tangu kwa mabibi,mama,dada,rika moja,watoto na wajukuu ambao wamekuwa wakiozeshwa.
Hivyo kanisa likaona sasa suala la ndoa za utotoni lifike mwisho linalochangiwa na mila na desturi kandamizi, kwa kuanzisha mradi ambao utafanya viongozi wa dini kuwa mstari wa mbele kukataa jambo hilo,kutoa elimu kwa watoto wa kike na kiume kuweza kukata na kupinga suala la ndoa za utotoni,watoto wa kike kuweza kujitete.
“Tangu mradi huo uanze mwaka juzi,kanisa limeisha okoa watoto watatu ambao walikuwa wanaozeshwa kwa nguvu,kutoka Wilaya ya Kwimba binti alikuwa amemaliza kidato cha nne matokeo yametoka akawa anaozeshwa,Mchungaji akapiga simu akashirikiana na Serikali ukawekwa mtego,muhusika akakamatwa sikuya kulipa mahari,huyu binti sasa anasoma marine engineering,fikiri kichwa kizuri hivyo kinapelekwa kupika ugali kwa kupelekwa kwenye ndoa hata hawezi,”.
Mkurugenzi Mtendaji wa Upendo Media, Neng’ida Johhannes,amesema,kama kanisa wananjivunia kuwa sehemu ya mapambano dhidi ya ndoa za utotoni,kwani wasichana wanaoolewa katika umri mdogo wanapoteza fursa ya kupata elimu huku afya zao zinakuwa hatarishi pamoja na kuingia kwenye ndoa ambazo hazina upendo wala heshima.
“Ndoa za utotoni ni tazizo ambalo linakabili pia nchi yetu,na nchi nyingi zinazoendelea,kwa mujibu wa tafiti mbalimbali zilizofanya hapa nchini na za kimataifa,zinaonesha Tanzania mikoa ambayo inaongoza kuwa na kiwango cha juu cha ndoa za utotoni ni Shinyanga,Tabora,Mara,Dodoma na Lindi, huku chanzo kikitajwa kuwa ni umasikini na mila kandamizi,”amesema Johhannes.
Hata hivyo,amewataka waandishi wa habari kuhakikisha inakuwa mstari wa mbele kuhimiza jamii,ili iweze kuachana na mila kandamizi na ukawaida unasababisha ndoa za utotoni.
Akiwasilisha mada katika mafunzo hayo,Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Mwanza,Baraka Makona,amesema,ndoa za utotoni zinafanyika zaidi katika maeneo ya vijijini katika jamii maskini na katika mikoa ya Magharibi,Kusini na Kaskazini-Magharibi mwa Tanzania.
Ambapo wanawake wanne kati ya kumi sawa na asilimia 37 wenye umri wa miaka 15-49 wanaoish vijijini waliolewa wakiwa watoto ikilinganishwa na wanawake wawili kati ya kumi sawa na asilimia 21 wanaoishi mijini.
Kwa mujibu wa taarifa za UNICEF,zinaonesha asilimia 21 ya wanawake vijana huolewa kabla ya kufikia umri wa miaka 18,hii inamaana kuwa wanawake milioni 650 wanaolewa chini ya umri unaotakiwa sawa na wanawake milioni 12 kila mwaka.Huku idadi kubwa ya ndoa za utotoni asilimia 37 zinatokea Kusini mwa Jangwa la Sahara ambapo na Tanzania ikiwemo.
More Stories
Samia aja na mkakati wa kukabiliana na ajali
Rais Samia, Mwinyi wapongezwa kupitishwa kuwani Urais CCM
Rais Samia apongezwa kuwezesha ujenzi ofisi kuu WMA