Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Mbunge Mteule wa Viti Maalumu Kundi la wanawake wenye Ulemavu Ummy Nderiananga amemtaja Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan kama Mtu mwenye Utu, Upendo na mwenye Kujali makundi mbalimbali ya Jamii, akimshukuru kwa kutoa zaidi ya Shilingi Bilioni mbili na Milioni mia moja hamsini na tisa kusaidia Vyama vya wenye ulemavu nchini Tanzania.
Nderiananga ameeleza hayo leo Oktoba Mosi, 2025 wakati wa Mkutano wa Kampeni za Dkt. Samia Moshi Mjini Mkoani Kilimanjaro kwenye Viwanja vya Mashujaa, akieleza kwamba Vyama hivyo vya wenye ulemavu kwa mara ya kwanza vimekuwa vikipokea ruzuku kutoka kwenye serikali ya awamu ya sita ya Dkt. Samia yenye kufikia shilingi Milioni mia nne na nane suala ambalo limefanikisha kuinua Vyama vya watu wenye Ulemavu nchini.
Amemshukuru Dkt. Samia pia kwa ujenzi wa Mabweni yaliyoongeza idadi ya wanafunzi wenye ulemavu kupata elimu ikiwemo bweni la zaidi ya Shilingi Milioni themanini lililojengwa Mkoani Kilimanjaro pamoja na uanzishwaji wa programu maalumu ya kumfuata mtoto mwenye ulemavu nyumbani na kumsomesha ( Home Schooling), jumla ya wanafunzi 691 wakiwa wanufaika wa programu hiyo.

Katika salamu zake wakati wa Mkutano huo wa Kampeni za Dkt. Samia, Nderiananga pia amemtaja Dkt. Samia kama Kiongozi aliyefanikisha watu wenye walemavu wa ngozi kuweza kuondokana na ugonjwa wa saratani kwa kutoa Milioni sitini kwa awamu ya kwanza na kuwezesha watu wenye ulemavu huo wa ngozi kuweza kupata mafuta kwa awamu ya kwanza kwaajili ya kusaidia matunzo ya ngozi.

More Stories
Wanawake washauriwa kuchangamkia fursa za uchumi
Aida:Wanawake wakipata haki zote itapunguza migogoro
LGTI wanawake waadhimisha siku yao Ngorongoro