Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline, Pwani.
SERIKALI inasimamia na kuratibu shughuli za kuzuia na kukabiliana na majanga yakiwemo yale yanayovuka mipaka ya Nchi kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Menejimenti ya Maafa ya mwaka 2004 na Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na 6 ya Mwaka 2022, Sambamba na kanuni zake za mwaka 2022 kupitia Idara ya Menejimenti ya Maafa inayotekeleza majukumu yake chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Akizungumza leo Julai 23,2024 kabla ya kuzindua Nyaraka za Usimamizi wa Maafa Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga amesema moja ya majukumu ya Idara ya Menejimenti ya Maafa kupitia Sheria ya Usimamizi wa Maafa namba 6 ya Mwaka 2022 ni kutayarisha, kuhuisha na kuratibu utekelezaji wa sera, mipango, sheria, kanuni, mikakati na taratibu za utendaji kwenye shughuli zote zinazohusiana na usimamizi wa maafa Tanzania Bara.
Aidha Ummy amesema kazi ya uandaaji wa mpango wa kujiandaa na kukabiliana na maafa na Mkakati wa Kupunguza Viatarishi vya Maafa kwa Wilaya ya Kibiti ni muendelezo wa utekelezaji wa jukumu hilo la msingi la Ofisi ya Waziri Mkuu ambalo limelenga kuimarisha usimamizi na uratibu wa Maafa katika ngazi za Mikoa na Wilaya.
“Kama mnavyofahamu katika kipindi cha mwezi Januari hadi Mei, 2024 mvua kubwa zilizonyesha katika maeneo mbalimbali Nchini na kusababisha Maafa ya Mafuriko katika maeneo mengi ikiwemo Mkoa wa Pwani Mafuriko haya yalisababisha madhara mbalimbali ikiwemo vifo, majeruhi, uharibifu wa mali, miundombinu na mazingira,”amesema Naibu Ummy
Aliongezea kuwa kufuatia hali hiyo Serikali kwa kushirikiana na wadau ilichukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuratibu upatikanaji wa misaada ya kibinadamu kwa waathirika, kuimarisha huduma za Afya, kutoa huduma ya Afya ya akili na msaada wa kisaikolojia na kijamii, kuratibu na kutekeleza operesheni ya utafutaji na uokoaji, kutafuta, kukusanya na kugawa misaada ya kibinadamu na kurejesha miundombinu iliyoathirika.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Ummy ametoa wito kwa wahusika kuhakikisha nyaraha hizo zilizoandaliwa ziwe ni chachu ya kuongeza ushirikishwaji wa jamii na wadau Pia, kujenga uelewa wa jamii kuhusu masuala ya usimamizi wa maafa, kuimarisha mfumo wa utoaji tahadhari ya awali, kujenga uwezo wa kuzuia, kupunguza madhara na kujiandaa na maafa na kujenga uwezo wa kukabiliana na maafa.
“Suala la kuzuia na kukabiliana na majanga ni mtambuka ambalo linahitaji nguvu za pamoja katika kulishughulikia hivyo, hapa leo suala hili, linajidhihirisha wazi kwa kuona washiriki walioko hapa kutoka katika idara mbalimbali, taasisi za Serikali za Wilaya ya Kibiti na taasisi zisizo za kiserikali hawa wote ni wadau muhimu sana katika kushughulikia usimamizi wa maafa hapa wilayani Kibiti.”Alisema Naibu Waziri Ummy
Kwa upande wake Mkurugenzi Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Brigedia Jenerali Hosea Ndagala amesema Ofisi kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) ilianza utekelezaji wa kazi hii kwa Kutoa Mafunzo ya kujengea uwezo Kamati Elekezi na Kamati ya Wataalamu ya Usimamizi wa Maafa kwa Wilaya ya Rufiji na Kibiti ambayo yalifanyika kwa njia ya nadharia na vitendo kwa muda wa siku kumi (10) ikiwa ni siku tano (5) kwa Wilaya ya Rufiji na siku tano (5) kwa Wilaya ya Kibiti.
Mafunzo hayo yalilenga kuimarisha zaidi kamati za usimamizi wa maafa kwa kufahamu majukumu yao kisheria, mfumo wa usimamizi wa maafa nchini pamoja na utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maafa kwa vipindi tofauti ikiwa ni kabla, wakati na baada ya maafa kutokea kwa kufuata mzingo wa usimamizi wa maafa.
“Uandaaji wa nyaraka hizi umezingatia ushirikishwaji wa jamii, wataalamu wa Halmashauri na Taasisi za kiserikali katika zoezi la ukusanyaji wa taarifa za msingi. Hali kadhalika kamati za usimamizi wa maafa zilipata wasaa wa kupitia na kuthibitisha nyaraka hizi na kujiridhisha kuwa zinaendana na mazingira ya Wilaya ya Kibiti na zitafaa kuwa muongozo wakati wa utekelezaji. Hakika ushirikiano ulikuwa mzuri ambapo mchakato wa uandaaji ulianza tarehe 24 Juni, 2024 hadi leo unapoenda kuzindua rasmi nyaraka hizi,”amesema Brigedia Jenerali Ndagala
Hata hivyo Brigedia Jenerali amewashukuru wadau wa maendeleo amabao ni Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa ufadhili ambao umechangia jitihada za Serikali katika kutekeleza kazi hii pamoja na uongozi Wilaya ya Kibiti, Kamati Elekezi ya Usimamizi wa Maafa chini ya Mhe, Mkuu wa Wilaya na Kamati ya Wataalam ya Usimamizi wa Maafa.
“Kwa niaba ya Serikali, naomba kutoa shukurani zangu za dhati kwa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa ufadhili ambao umewezesha kuchangia jitihada za Serikali katika kuandaa Mpango wa Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa pamoja na Mkakati wa Kupunguza Vihatarishi vya Maafa kwa Wilaya ya Kibiti Sambamba na hilo, niwashukuru wataalamu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu na Mtaalamu Mwelekezi toka DarMAERT kwa kufanikisha mchakato wa kitaalamu katika kutoa mafunzo na maandalizi ya nyaraka hizi,”amesema Brigedia Jenerali Ndagala
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakaniÂ
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best