Na Mwandishi Wetu ,Berlin Ujerumani

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu Mheshimiwa Ummy Nderiananga ameongoza ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaoshiriki Mkutano wa Tatu wa Kimataifa wa Watu wenye Ulemavu unaofanyika jijini Berlin, Ujerumani tarehe 2 hadi 3 April,2025.
Mkutano huo umeandaliwa na Shirikisho la Kimataifa wa Watu Wenye Ulemavu (IDA), Serikali ya Ujerumani, na Serikali ya Jordan na kufunguliwa rasmi kwa pamoja na Kansela wa Ujerumani Mhe. Olaf Scholz na Mfalme Abdullah II wa Jordani.
Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa Mkutano huo Mhe. Scholz amesisitiza juu ya umuhimu wa kushirikiana kimataifa kukuza haki na ujumuishaji wa masuala ya Watu Wenye Ulemavu.
“Ushirikiano wa kimataifa ni nguzo muhimu katika kuhakikisha haki na ujumuishaji wa watu wenye ulemavu unatekelezwa kikamilifu duniani kote kwa kushirikiana, serikali, mashirika ya kimataifa, sekta binafsi, taasisi za elimu, mashirika ya kiraia, na Mashirika ya Watu Wenye Ulemavu tunaweza kuunda sera na mipango madhubuti inayohakikisha usawa wa fursa na ushiriki kamili wa watu wenye ulemavu katika jamii, “ alisisitiza.
Naye Mfalme Abdullah II wa Jordani akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo alisisitiza dhamira ya dhati ya kuendeleza haki na ujumuishaji wa watu wenye ulemavu.
Mfalme Abdullah II alitilia mkazo umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kuhakikisha fursa sawa na ushiriki kamili wa watu wenye ulemavu katika nyanja zote za jamii.
Mkutano huo unalenga kuhamasisha juhudi za kimataifa katika kufanikisha ujumuishaji wa watu wenye ulemavu duniani na kuwaleta pamoja wadau wa ngazi za juu kujadili na kushiriki maendeleo katika ujumuishaji wa watu wenye ulemavu, kutoka serikalini, mashirika ya kimataifa, sekta binafsi, taasisi za elimu ya juu, mashirika ya kiraia na mashirika ya watu wenye ulemavu kutoka nchi mbalimbali.
Mkutano wa Kimataifa wa Watu wenye Ulemavu (GDS) ni jukwaa la kipekee la kimataifa linaloangazia uboreshaji wa maisha ya watu wenye ulemavu, hususan kutoka Kusini mwa Dunia.
Mkutano huo ulianzishwa mwaka 2017 kwa lengo la kuwakutanisha wadau wa kimataifa, kikanda, na kitaifa wanaoshiriki malengo na maono ya maendeleo jumuishi kwa watu wenye ulemavu na hatua za kibinadamu.
Mkutano huu unalenga kuziba pengo kati ya nyanja mbili za ujumuishaji watu wenye ulemavu na ushirikiano wa maendeleo.
Mkutano wa Kimataifa wa Watu wenye Ulemavu hufanyika kila baada ya miaka mitatu ni jukwaa linalohusisha utetezi wa mara kwa mara na wadau wa maendeleo ya wenye ulemavu kimataifa pamoja na kuhamasisha vuguvugu la haki za watu wenye ulemavu na washirika wake duniani.
Mkutano huo pia unaangalia namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya nchi wanachama na Mashirika ya Watu Wenye Ulemavu (OPDs) kupitia mipango ya pamoja ya uandaaji wa mkutano.
More Stories
Waziri Mavunde azindua rasmi shughuli za uchimbaji madini Porcupine North -Chunya Mbeya
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,Baraza la Taifa la Ujenzi waingia makubaliano ya mashirikiano sekta ya ujenzi
Nderiananga aongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa tatu wa Kimataifa wa watu wenye ulemavu ujerumani