Na Mwandishi Wetu,Timesmajira
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius John Ndejembi, ameiagiza Wizara ya Nishati kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) kuandaa mpango mkakati utakaowawezesha vijana na kampuni za Kitanzania kunufaika na fursa za ajira, zabuni na uwekezaji katika miradi ya mafuta na gesi asilia nchini.
Makamu wa Rais ametoa maagizo hayo leo, Oktoba 28, 2026, wakati wa hafla ya utiaji saini wa leseni nne za utafutaji wa mafuta na gesi asilia katika vitalu vya Mnazi Bay North, West Songo Songo, Eyasi – Wembere na Lindi- Mtwara, iliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.
Makamu wa Rais amesema ni muhimu kuhakikisha Watanzania, hususan vijana na wanawake, wanapewa kipaumbele katika ajira, mafunzo, teknolojia na zabuni, huku kampuni za ndani zikiwezeshwa kushiriki kikamilifu katika mnyororo wa thamani wa sekta hiyo.
Aidha, ameitaka Wizara ya Nishati kuimarisha mifumo ya tathmini, ufuatiliaji na usimamizi wa leseni hizo, sambamba na kuhakikisha kunakuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha, uwajibikaji na ongezeko la mapato ya Serikali kupitia kodi, mrabaha na mgao wa faida.

Ameielekeza TPDC kushirikiana na wawekezaji wenye uwezo wa kifedha, ujuzi na teknolojia ili kuongeza tija katika shughuli za utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi asilia, huku akiwataka wadau kutanguliza uzalendo kwa Tafa, uadilifu, uchapa kazi na maslahi ya Taifa mbele.
Makamu wa Rais amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji, yanayozingatia uwazi, kutabirika kwa mifumo ya kisheria, ushindani wa haki na ulinzi wa maslahi ya Taifa.
Makamu wa Rais amesema, pamoja na lengo la kukuza pato la Taifa kufikia dola za Marekani trillioni 1 kama iliyoainishwa kwenye dira ya Taifa ya 2050. Matarajio mengine ya leseni hizo katika ugunduzi wa mafuta na gesi asilia ni ongezeko la mapato ya Serikali kupitia mrabaha, kodi na mgao wa faida.

Amesema uzalishaji wa umeme kwa kutumia gesi unatarajiwa kuchangia uzalishaji wa Megawati 70,000 (zitakazohitajika ifikapo 2050), na kukuza ujuzi, teknolojia, kuongeza ajira na kupanua fursa kwa kampuni za Tanzania zinazotoa huduma katika sekta hiyo.
Ametaka uwepo wa usimamizi madhubuti, nidhamu ya matumizi ya fedha na uwajibikaji. Ametoa rai kwa taasisi zote zinazohusika na uwekezaji huu kuhakikisha Watanzania, hususan wanawake na vijana wanapewa fursa za ajira, mafunzo, teknolojia na zabuni. Vilevile, ni muhimu kuimarisha ushiriki wa kampuni za Kitanzania katika mnyororo wa thamani wa mafuta na gesi.
Makamu wa Rais amesema lengo la Serikali ya Awamu ya Sita ni kuanzisha Kituo cha umahiri cha kuendeleza ujuzi unaohitajika katika sekta ya mafuta na gesi asilia ili kujenga rasilimali-watu yenye ujuzi na itakayowezesha kuleta ustawi wa Uchumi jumuishi na endelevu.

Awali, Waziri wa Nishati, Dkt. Juma Zuberi Homera, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza uwekezaji katika miradi ya kimkakati ya nishati, akisema hatua ya TPDC kukabidhiwa leseni na kumiliki vitalu vyake ni mafanikio makubwa katika kuimarisha uwezo wa Taifa wa kutafuta na kuendeleza rasilimali za mafuta na gesi.
Amesema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha gesi asilia inayoendelezwa inatumika katika shughuli mbalimbali, zikiwemo matumizi ya majumbani, usafiri, uzalishaji wa umeme na viwandani, huku wananchi na kampuni za ndani zikinufaika na uwekezaji huo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mhandisi Mussa Makame, amesema vitalu vinne vilivyohusika katika utiaji saini viko katika hatua mbalimbali za utekelezaji, ikiwemo ukusanyaji wa taarifa za mitetemo kwa ajili ya shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia.
Amesema shirika hilo litahakikisha wananchi wanashirikishwa kikamilifu, kampuni za ndani zinapewa kipaumbele kulingana na uwezo na utaalamu wao, pamoja na kutekeleza miradi ya uwajibikaji kwa jamii (CSR) ili uwekezaji huo uwe na manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi.



More Stories
Serikali yaimarisha utafutaji wa Mafuta,Gesi
SGA Cash in Transit yatajwa kuwa kampuni bora ya huduma
TTCL yatangaza kutoa ofa ya fiber mlangoni kwako