December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ndege mpya yatua na maelekezo juu


*Dkt. Mpango aitaka ATCL kuimarisha ushindani kikanda, kimataifa, atoa maelekezo kwa Bodi, ndege za mafunzo urubani NIT zazinduliwa

Jackline Martin na Irene Clemence, TimesMajira Online

NDEGE mpya iliyonunuliwa na Serikali aina ya Boeing 737-9 Max yenye uwezo wa kubeba abiria 181 imetua nchini na kupokelewa na Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango, huku akilita Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kuimarisha ushindani wa kikanda na kimataifa.

Hafla ya kupokea ndege hiyo ilienda sambamba na uzinduzi wa ndege mbili za mafunzo ya marubani na wahandisi aina ya Cessa katika  Chuo cha Usafirisha Tanzania (NIT).

Akizungumza wakati wa mapokezi ya ndege hiyo, Dkt. Mpango ameitaka Wizara ya Uchukuzi pamoja na Bodi ya Wakurugenzi na Wafanyakazi wa ATCL kutimiza wajibu wao, kwa kusimamia vizuri utoaji wa huduma za usafiri wa anga ili kuimarisha ushindani kwa lengo la kuongeza mchango katika Pato la Taifa

Dkt. Mpango alitoa maelekezo hayo jana Jijini Dar es Salaam wakati wa mapokezi ya ndege.

Alisema bado kuna malalamiko ya wateja wa ATCL kuhusu huduma za usafiri, ikiwemo kuahirishwa safari au kusogeza mbele muda wa safari.

“Kuna kelele nyingi sana, hivyo baada ya kupokea ndege hii (Boeing 737-9Max) matarajio ya Watanzania ni kuwa ATCL itamaliza kabisa kero hiyo,” alisema Dkt. Mpango.

Pia aliitaka Wizara ya Uchukuzi kufuatilia kwa ukaribu ubora wa huduma zinazotolewa na ATCL na za ununuzi wa vyakula na viburudisho ndani ya ndege.

“ATCL ihakikishe anatoa kipaumbele kwa bidhaa zinazozalishwa  nchini, ambazo zimethibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ili kukuza kipato na ajira za wajasiriamali na wazalishaji wa Tanzania,” alisema Dkt. Mpango.

Aliiagiza Bodi ya ATCL kulisimamia vizuri shirika hilo, ili kulinda mtaji uliowekezwa na Serikali kwa niaba ya Watanzania

“Serikali haitavumilia uzembe wowote utakaojitokeza tena ndani ya ATCL, kama ilivyowahi kuwa ndani ya miaka ya nyuma,” alisisitiza Dkt. Mpango.

Mbali na hayo, alisema amepokea changamoto za gharama kubwa ya usafirishaji wa mizigo kwenda nje ya nchi katika viwanja vya Julius Nyerere, Kilimanjaro na Sheikh Abeid Aman Karume Zanzibar ikilinganishwa na viwanja vya ndege vya nchi jirani, lakini pia na gharama za kusafirisha mizigo kwa kutumia ndege za Mashirika mengine Duniani.

“Naielekeza Wizara ya Uchukuzi kwa pamoja na Wizara ya Fedha washirikiane na wenzao wa Zanzibar ili kuchambua na kubaini kiini cha changamoto hiyo na kupendekeza hatua zinazopaswa kuchuchukuliwa,” alisema Dkt. Mpango na kuongeza;

“Tazameni hizo tozo na kodi mbalimbali, mfanye uchambuzi wa uhakika ndani ya siku 14 kuanzia leo (jana) na mlete mapendekezo serikalini.”

Alisema Serikali imewekeza fedha nyingi kununua ndege hizo na kufanya maboresha ya viwanja vya ndege, lengo ni kuhakikisha shehena kubwa ya mizigo inapatikana kuongeza mapato.

Kuhusu ndege za wanafunzi wa marubani, Dkt. Mpango aliuelekeza uongozi NIT na pia marubani wakufunzi na marubani wanafunzi watunze ndege hizo ili ziweze kudumu na kuendelea kufundishia marubani wengi zaidi.

Mbali na hayo, Dkt. Mpango alimuelekeza wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa kuangalia chuo NIT kibajeti kuanzia mwaka ujao wa fedha ili maombi ya ununuzi wa ndege nyingine mbili za marubani zenye  injini mbili yaweze kufanyiwa kazi haraka iwezekanavyo.