January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ndayiragije: Maandalizi bora yatatubeba AFCON

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

KOCHA mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Etienne Ndayiragije amesema kuwa ikiwa timu hiyo itapata muda mrefu wa kufanya maandalizi mazuri zaidi basi huenda wakafanya vizuri katika mechi zao mbili zilizobaki katika mashindano ya kutafuta tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON 2021) zitakazofanyika nchini Cameroon.

Baada ya sare ya goli 1-1 dhidi ya timu ya Taifa ya Tunisia waliyopata katika mchezo wa juzi wa marudiano uliochezwa kwenye uwanja wa Mkapa, sasa timu hiyo itakuwa na kibarua kingine katika mchezo wa ugenini namba 124 dhidi ya Equatorial Quinea huku wakimaliza nyumbani na Libya katika mchezo namba 147.

Licha ya sare hiyo lakini bado kuna matumaini makubwa ya kurudi tena katika fainali hizo ikiwa tu watapambana na kupata pointi katika ambazo zitawasogeza juu katika msimamo wa Kundi J.

Hadi sasa katika kundi hilo, vinara Tunisia ambao wamefikisha pointi 10 wameshajihakikishia akiungana na Senegal, Cameroon, Algeria na Mali ambazo tayari zimeshafuzu kucheza fainali hizo huku Equatorial Guinea wakiwa nafasi ya pili wakiwa na pointi sita huku kazi kubwa zaidi ikiwa kwa Tanzania ambao wanashika nafasi ya tatu wakiwa na pointi nne Libya ambao wanashika mkia kwenye kundi hilo.

Kocha Ndayiragije amesema, katika mchezo dhidi ya Tunisia wachezaji wake wameonesha kuwa wana uwezo wa kufanya kitu na kitu pekee wanachokihitaji ili kufika wanapopataka ni muda wa maandalizi zaidi.

Kilichowawezesha wapinzani wao kuwa bora ni kujiandaa kwa muda mrefu hivyo hata Tanzania ikiwekeza nguvu zaidi katika maandalizi ya Timu ya Taifa kama inavyofanyika kwa klabu kubwa hapa nchini basi ingekuwa mbali.

Pia bado ana imani kubwa kuwa kikosi hicho kinaweza kufanya makubwa katika michezo miwili iliyobaki na kupata nafasi ya kusonga mbele katika mashindano hayo.

“Nina imani kuwa tukiweka nguvu katika maandalizi basi tunaweza kufanya kitu katika mashindano haya kwani bado tuna nafasi ya kufanya vizuri na kusonga mbele hivyo kikubwa ni kufanikisha hilo ili kuweza kufikia malengo yetu,” amesema kocha huyo.

Hata hivyo kocha huyo amesema kuwa, kabla ya kucheza mechi hizo kutakuwa na michuano ya CHAN itakayoanza Januari hivyo ikiwa yatatumika vizuri kama sehemu ya maandalizi basi kazi haitakuwa kubwa pale watakapoungana na wachezaji wanaocheza nje ya nchi.