Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amesema, kuanzishwa kwa Kozi ya Uvuvi na uchakataji wa mazao ya uvuvi, katika Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) itasaidia kujiajiri na kuinua kipato.
Profesa Ndalichako ametoa kauli hiyo Mei 25, 2021 mkoani Dar es Salaam wakati alipokuwa akipokea msaada wa vifaa vya mafunzo ya uvuvi na uchakataji wa mazao ya samaki vilivyotolewa na Serikali ya China kwa ajili ya Chuo cha Veta, Wilaya ya Chato mkoani Geita.
Amesema, kuwepo kwa kozi hiyo kutawawezesha wananchi wa Chato, Kagera na mikoa ambayo wananchi wake wanategemea uvuvi kuinua kipato chao pamoja na kuipa fursa Serikali kuendeleza mafunzo hayo katika mikoa mingine.
“Kozi hii ni ya kwanza kuanzishwa nchini hapa katika vyuo vya kiada ambapo kwa mara ya kwanza VETA watatoa mafunzo haya katika Chuo cha Ufundi Stadi Veta wilaya ya Chato.
“Vifaa vilivyotolewa na Serikali ya Watu wa China ni pamoja na majokofu, mashine za kusindika samaki, kutengeneza soseji za samaki na boti ya uvuvi ambavyo thamani yake ni sh.milioni 350,”amesema.
Profesa Ndalichako amesema, Serikali ya China imekuwa ikitoa msaada mbalimbali ikiwemo ambao ni mwendelezo wa urafiki na undugu siku nyingi.
Aidha, ameutaka Uongozi wa Chuo cha VETA kuendeleza mafunzo hayo katika kuwawezesha kuinua kipato na uchumi kwa ujumla.
Vilevile Profesa Ndalichako ameutaka uongozi wa VETA ukavitunze vifaa hivyo ili vitumike kikamilifu na kusaidia wanafunzi ambao watakuwa wataalamu mahiri katika nyanja ya uvuvi na uchakataji wa vifaa vya uvuvi.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Dkt. Pancras Bujulu alisema, vifaa hivyo ni matokeo ya ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa China mara baada ya kuja nchini na kufika katika chuo na kuahidi kukisaidia ili kiweze kukua kitaaluma.
Naye Balozi wa China nchini Tanzania, Wang ke amesema msaada huo wa vifaa ni mwendelezo wa ushirikiano wa China na Tanzania. Amesema, kila taifa linategemea elimu ili kuzalisha watu watu wenye weledi wa kutosha katika fani mbalimbali na kusaidia taifa kukua kiuchumi.
Amesema kuwa, Serikali ya China inajionea fahari kuendelea kuisaidia Tanzania na ili kuhakikisha watu wake wanaendelea na kupata kizazi kilichoendelea chenye manufaa makubwa.
Leonard Akwilapo ambaye ni Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi alisema, ukizingatia uhaba wa vifaa uliokuwepo, vifaa hivyo vitasaidia kuendeleza chuo na wanafunzi kuweza kupata elimu yenye viwango vyakutosha.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakaniÂ
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best