Na Omary Mtamike,TimesMajira online,Dodoma
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amewataka wafugaji nchini kuipokea na kuifanyia kazi teknolojia mpya ya uzalishaji wa malisho ya mifugo inayojulikana kama ‘Juncao’ pindi itakapotambulishwa kwao.
Waziri Ndaki amesema hayo juzi baada ya kuwasilishiwa taarifa ya namna teknolojia hiyo inavyofanya kazi ambapo amebainisha kuwa aina hiyo ya malisho itakuwa mkombozi kwa wafugaji waliopo hapa nchini hasa kutokana na utamaduni wao wa kuhama katika maeneo tofauti wakitafuta malisho.
Wafugaji ni lazima tukubali kubadilika hasa kutokana na ukweli kuwa kazi hiyo ina faida kubwa kwa hiyo lazima sasa tuingie gharama kidogo ili tuwe na wafugaji wazuri na tufanye ufugaji wenye tija” amesema Ndaki.
Waziri Ndaki ameongeza kuwa Wizara yake inakusudia kusambaza teknolojia hiyo kwa wafugaji wote kupitia kwa wataalam waliopo kwenye Halmashauri za Wilaya hivyo aliwaomba wafugaji kuchangamkia fursa hiyo pindi itakapowafikia ili waondokane na migogoro baina yao na watumiaji wengine wa ardhi.
“Tukubali kutenga maeneo ya kupanda majani haya kwa sababu ule utaratibu wa kufika sehemu na kuanza kulisha mifugo yako majani ambayo hukupanda wewe utafika mwisho wake muda si mrefu na ndio maana nasisitiza ni lazima tukubali kubadilika” amesisitiza Ndaki.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi,Abdallah Ulega amesema kuwa amefurahi kusikia kuwa teknolojia hiyo hata hapa Tanzania ilikuwepo isipokuwa hii ya sasa imeboreshwa kwa kuongezwa virutubisho vya protini hivyo ana imani kuwa itafanya vizuri zaidi kwa mifugo iliyopo hapa nchini.
“Uzuri ni kwamba tumejipanga na tutaanza na ranchi zetu ili mifugo iliyopo kwenye ranchi hizo iwe ni ya mfano kwa wafugaji wengine kwa hiyo Mhe. Waziri hili jambo ni kubwa na zuri na kwa maeneo yenye ardhi kame kama vile Maswa, Manyara, Shinyanga, Singida na Dodoma itatusaidia sana kuongeza uzalishaji kwenye maeneo hayo” ameongeza Ulega.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo),Prof. Elisante Ole Gabriel amemshukuru Waziri Ndaki kwa kukubali teknolojia hiyo ianze kutekelezwa hapa nchini ambapo alimuagiza Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) Dkt.Erick Komba kufanya utafiti wa namna ya kuboresha zaidi malisho hayo ili kuongeza tija zaidi ya teknolojia hiyo.
“Waziri Malisho ni siasa na siasa ni malisho,kwa hiyo nawaomba wewe na Naibu Waziri mkatusaidie kuisemea sana hii teknolojia kwenye majukwaa yenu ikiwa ni pamoja na kusisitiza Halmashauri zetu ziangalie namna ya kuwawezesha vijana, wazee na wenye ulemavu kujiingiza kwenye kilimo cha malisho haya kupitia ile asilimia 10 ya mikopo wanayopata” alisema Prof. Ole Gabriel.
Akielezea namna walivyojipanga kutumia teknolojia hiyo, Mkurugenzi wa idara ya uendelezaji wa maeneo ya malisho na rasilimali za vyakula vya mifugo Dkt. Asimwe Rwiguza amesema kuwa tayari wameshapeleka aina hiyo ya malisho katika shamba la malisho ya mifugo la Vikuge lililopo Mkoani Pwani na wanatarajia kupeleka mbegu nyingine za malisho hayo katika mashamba yaliyopo kituo cha Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) kilichopo Mpwapwa, Dodoma.
Awali akiwasilisha teknolojia ya malisho hayo, Mhadhiri mwandamizi na mtaalam wa teknolojia hiyo hapa nchini Dkt. Elly Ligate amesema kuwa mbali na kutumika kwa ajili ya malisho ya mifugo,majani hayo yakisagwa na kuwa kwenye mfumo wa chenga chenga (pellet) yanaweza kutumika kama chakula cha samaki.
Utambulisho wa teknolojia hiyo ya malisho muendelezo wa jitihada mbalimbali ambazo Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikizifanya ili kuhakikisha wafugaji wanapata malisho ya kutosha na kuondokana na migogoro baina yao na watumiaji wengine wa ardhi.
More Stories
CCM hakuna kulala, Nchimbi atua Tabora kwa ziara ya siku mbili
Kongamano la Uwekezaji na Biashara lafunguliwa Pwani
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi