November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ndaki: Tutengeneze uhitaji wa maziwa kwanza

Na Omary Mtamike, TimesMajira Online

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki ameiagiza Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) kushirikiana na chama cha Wasindikaji wa Maziwa (TAMPA) kutengeneza uhitaji wa maziwa kwa wananchi badala ya kuendelea kutumia nguvu kubwa sana kwenye kusisitiza uzalishaji na usindikaji wa bidhaa hiyo.

Ndaki amesema hayo jana kwenye mkutano wa Chama cha Wasindikaji wa Maziwa nchini (TAMPA) uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) jijini Dar es Salaam ambapo amezitaka pande hizo kuhakikisha zinapata suluhu ya changamoto ya kiwango kidogo cha matumizi ya bidhaa hiyo nchini.

“Hebu jiulizeni tu kwa mfano maziwa yakakosekana siku nzima hapa Tanzania kuna watu wataandamana kama ilivyo kwa bidhaa nyingine? Kwa sababu inawezekana tunatumia nguvu kubwa kusisitiza uzalishaji na usindikaji wakati hakuna uhitaji wa bidhaa hiyo hapa kwetu” alisisitiza Ndaki.

Ndaki alisema kuwa nia ya Serikali ni kuhakikisha bidhaa hiyo inawasaidia wafugaji na wasindikaji waliopo hapa nchini kwa kuanza na soko la ndani hivyo ni lazima Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi wahakikishe linakuwa la uhakika.

“Katika kuhakikisha tunawalinda Wasindikaji na Wazalishaji wa maziwa wa ndani, Sisi kama Serikali tutaendelea kutoza kiasi cha shilingi 2000 kwa kila pakiti ya Maziwa yanayoingia kutoka nje na hatuwezi kuiondoa kabisa labda tuipunguze kidogo kama tutalazimika kufanya hivyo” ameongeza Ndaki.

Kuhusu wingi wa Tozo zilizopo kwenye mnyororo wa thamani wa maziwa yanayozalishwa na kusindikwa hapa nchini, Waziri Ndaki amesema kuwa Serikali itaendelea kuondoa tozo kwenye bidhaa mbalimbali zinazotumika kwenye shughuli za uzalishaji na usindikaji wa maziwa hapa nchini.

“Nimesikia malalamiko hapa kuwa yale malori yanayotumika kusafirishia maziwa yanatozwa utitiri wa kodi mbalimbali ambazo kwa kiasi kikubwa zinawakwamisha kufanya shughuli zenu hivyo na hili tutaenda kuangalia namna ya kuliweka sawa ili lisiwe kikwazo kwenu” amesisitiza Ndaki.

Kwa upande wake Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini (TDB) Dkt. George Msalya alikiri kuwa mchango wa tasnia ya Maziwa kwenye pato la Taifa bado upo chini ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika Mashariki.

“Mpaka sasa Tasnia yetu inakuwa kwa asilimia 2.3 na mchango wake kwenye pato la Taifa ni asilimia 2 kwa mujibu wa takwimu zilizopo wakati wenzetu Kenya wanachangia asilimia 5 na Uganda na Rwanda nao wanakuja kwa kasi kubwa hivyo tuna kazi kubwa ya kufanya” amesema Dkt. Msalya.

Naye mmoja wa wasindikaji wa Maziwa nchini kutoka Kiwanda cha Nronga kilichopo Siha Mkoani Kilimanjaro Bi Hellen Usiri amebainisha kuwa changamoto kubwa inayowakabili ni uwepo wa wauzaji maziwa wasio rasmi ambao hununua maziwa kwa mfugaji kwa bei kubwa ikilinganishwa na ile inayotolewa na viwanda vya kusindika bidhaa hiyo.

“Hawa wenzetu hawalipi kodi na hawana gharama yoyote ya uchakataji ndio maana wanauza kwa bei wanayotaka wao hivyo nashauri wafanyabiashara hao wa mitaani wajiunge kwenye vyama vya ushirika ili maziwa wanayouza yatoke kwenye vyama hivyo yakiwa salama kabisa tofauti na sasa ambapo maziwa mengi yanayouzwa mtaani si salama” amesisitiza Bi. Usiri.

Kikao cha leo ni mwanzo wa vikao vitakavyofanyika mara kwa mara kati ya Wizara, taasisi zake na wadau wake ili kupata ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zinazowakabili wadau hao.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (katikati) akisisitiza kuhusu tasnia ya maziwa kutathmini uhitaji wa bidhaa hiyo wakati wa Mkutano wa Chama cha Wasindikaji wa Maziwa nchini (TAMPA) uliofanyika leo (05.04.2022) makao makuu ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) jijini Dar-es-salaam.
Mkurugenzi Mradi Mkaazi kutoka Shirika la kimataifa la Heifer Bw. Mark Tsoxo akieleza mipango ya Shirika hilo katika kuendeleza tasnia ya Maziwa nchini wakati wa Mkutano wa Chama cha Wasindikaji wa Maziwa nchini (TAMPA) uliofanyika leo (05.04.2022) makao makuu ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) jijini Dar-es-salaam.
Katibu Mtendaji wa Chama cha Wasindikaji wa Maziwa nchini (TAMPA) Bw. Florent Nguma akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa chama hicho wakati wa Mkutano wa Chama cha Wasindikaji wa Maziwa nchini (TAMPA) uliofanyika leo (05.04.2022) makao makuu ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) jijini Dar-es-salaam.