Na Agnes Alcardo,TimesmajiraOnline,Arusha
KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amesema Viongozi wa Chama na Serikali wasiosikiliza na kutatua kero za wananchi wao hawafai na kuwa katika nafasi hizo na chama hakita wafumbia macho.
Dkt.Nchimbi amesema hayo Juni 2, 2024, akihutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara ambao umefanyika katika kijiji cha Makuyuni wilaya ya Monduli, mkoani Arusha, ikiwa ni siku yake ya kwanza ya ziara mkoani humo akitokea Manyara.
Katika ziara hiyo akiwa ameambatana na Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, CPA. Amos Makalla pamoja na Katibu wa NEC, Mambo ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Rabia Abdallah Hamid
Dkt.Nchimbi amesema,lengo la CCM kuendelea kufanya ziara katika maeneo mbalimbali nchini ni pamoja na kuangalia uhai wa Chama, kukagua utekelezaji wa Ilani 2020/2025 na kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
“CCM ipo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wake, hivyo ni wajibu wetu sisi viongozi wa Chama na Serikali kusikiliza na kutatua kero za wananchi na si vinginevyo na kama kuna viongozi wasiyofanya hivyo basi hawafai kuwa viongozi,”amesema Nchimbi.
Sambamba na hayo, pia Dkt. Nchimbi alipata nafasi ya kuzindua mashina mawili ya wakeleketwa wa CCM na wajasiriamali, katika Kata ya Makuyuni Wilaya ya Monduli na shina lingine wilayani Arumeru na kutoa kadi nne za uanachama wa CCM kwa Wanachama wapya.
Aidha kwa upande wake Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, CPA.Amos Makalla, amewasisitiza wananchi wa Arusha kuendelea kukiamini chama cha CCM ili kiendelee kuwaletea maendeleo na kutowafuata wachache wanaopotosha.
“Nyie ni watanzania na CCM kipo kwa ajili ya watanzania hivyo ni vyema mkaacha kusikiliza habari za upotoshaji na badala yake muendelee kuunga mkono juhudi za chama ili tuweze kuleta maendeleo zaidi katika nchi yetu,”amesema Makalla.
More Stories
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi
Mbunge Ndingo:CCM imejidhatiti kuwaletea maendeleo wananchi