Na Agnes Alcardo, Timesmajiraonline, Singida
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, ameahidi kumpatia baiskeli ya magurudumu matatu mlemavu wa ngozi, Yacobo David, ili kimsaidia katika shughuli zake mbalimbali za kila siku aweze kujikwambua kiuchumi.
Ahadi hiyo imetolewa jana na Katibu Mkuu huyo katika Mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la Majengo katika Wilaya ya Manyoni mkoani Singida.
Nchimbi yupo kwenye ziara inayolenga kutembelea mikoa mitano, kwa lengo la kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025.
Amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Kemirembe Lwota, kutafuta eneo litalojengwa ofisi za walemavu wa ngozi katika wilaya hiyo.
Pia Dkt. Nchimbi amesema, bado Serikali inaendelea kutekeleza Ilani ya CCM, ikiwa pamoja na ukamilishwaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo mradi wa maji, kituo kidogo cha kupooza umeme ili wananchi waweze kuondokana na kero ya kukosekana kwa umeme.
Aidha ziara hiyo, Dkt. Nchimbi amewataka wananchi kuwa na umoja na kutokubali kugawanywa na kusema kuwa Taifa imara hujengwa na wananchi imara, walio na umoja na ushirikiano kwa Serikali yao.
“Katika mambo ambayo naomba niwasihi leo ni kuhusu suala la umoja, tusikubali leo aje mtu kutugawanya wakati sisi ni wamoja na kufanya hivyo atakuwa ameturudisha nyuma, tutambue kuwa umoja na mshikamano ni kwa maslahi ya Watanzania na Taifa, kwani Tanzania ni nchi yenye upendo na haibagui wananchi wake kwa rangi, dini wala kabila”, alisema Dkt. Nchimbi.
Sambamba na hayo, pia amemtaka Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Martha Mlata, kutoa kipaumbele kwa walemavu pindi wanapogombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama.
” Ilani yetu ya chama kati ya mambo yaliyoahinishwa ni pamoja na kutoa vipaumbele kwa watu wenye ulemavu, hivyo nikuombee ndugu Mwenyekiti kutekeleza hili hata katika chaguzi mbalimbali ili watu hawa waweze kupatiwa nafasi mbalimbali pindi wanapogembea nafasi mbalimbali za uongozi,” amesema Dkt. Nchimbi.
Kwa upande wake Katibu w NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, Amos Makalla, amesema malengo ya ziara hizo zinazofanywa na CCM ni pamoja na kukutana na wananchi katika maeneo mbalimbali kusikiliza changamoto zao na kukagua utekelezwaji wa miradi.
Naye Mwenyeki wa CCM Mkoa wa Singida, Martha Mlata, amesema hali ya kisiasa mkoani humo ipo shwari na miradi mablimbali ya maendeleo inaendelea kutekelezwa.
More Stories
Waziri Mkuu: Tumieni matokeo ya tafiti za kisayansi katika utekelezaji wa mipango ya kitaifa
Zaidi ya wananchi 32,000 Vijiji vya Wilaya za Morogoro na Mvomero kuanza kupata mawasiliano
Wafanyabiashara waomba elimu ya namna watakavyorejea soko kuu