January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Nchimbi atoa maelekezo kwa Waziri Kairuki kushughulikia kero za wanyamapori Karagwe

Na Mwandishi wetu, Timesmajira

KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, amemuelekeza Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki kuifanyia kazi na kupata ufumbuzi wa changamoto ya wanyama waharibifu wanaovamia makazi ya watu, kuharibu mazao na kutishia uhai wa binadamu, Wilaya ya Karagwe.

Vile vile, Katibu Mkuu Balozi Dkt. Nchimbi amezielekeza mamlaka husika mkoani Kagera, kwa kushirikiana na wizara za kisekta husika, kushughulikia na kumaliza tatizo la matumizi ya ardhi, mipaka kati ya wananchi na Kampuni ya Ranchi za Taifa NARCO, wilayani Karagwe.

Balozi Nchimbi ametoa maelekezo hayo alipokua akizungumza na wananchi wa Karagwe, katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Kituo cha Mabasi cha Kayanga, wilayani Karagwe, mkoani Kagera, Agosti 8, 2024, akiwa katika siku ya tatu ya ziara yake ya siku sita mkoani humo, ambapo miongoni mwa kero za wananchi wa jimbo alizotaarifiwa, ni pamoja na uvamizi wa wanyama hao wakali katika vijiji vya Kata ya Kihanga (Kihanga, Kibwela na Mshabaiguru), ambako Tembo wanavamia mashamba ya wakulima, kuharibu mazao na kuhatarisha maisha wa wananchi katika maeneo husika.

Aidha, kutokana na kuwepo taarifa za mgogoro wa ardhi Kata ya Rugera, kati ya wananchi na Shirika la NARCO katika Kijiji cha Omukakajinja, alitoa maelekezo, kupitia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, kuziagiza mamlaka zinazohusika, zikiwemo za kisekta, kufanyia kazi masuala hayo na kumpatia taarifa za kumalizika kwa migogoro hiyo.

Balozi Dkt.Nchimbi ametaka changamoto hiyo ishughulikiwe haraka ikiwemo kutafuta namna ya kudhibiti wanyama waharibifu hasa Tembo lakini pia suala la mipaka ili ijulikane.

Katika hatua nyingine Balozi Dokta Nchimbi amemshukuru Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kwa kuusikia wito wa suala la Vitambulisho vya NIDA, na kumuagiza Naibu Waziri wa Mambo ya ndani afike Kagera kuungana na Katibu Mkuu kuwa sehemu ya msafara wa ziara hiyo, ili atolee ufafanuzi na kujibu malalamiko ya wananchi kuhusu jambo hilo.

Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Nchimbi yuko ziara ya siku sita, Mkoa wa Kagera, akiwa ameambatana na Issa Haji Usi Gavu, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) – Oganaizesheni, Amos Gabriel Makalla, Katibu wa NEC – Itikadi, Uenezi na Mafunzo na Rabia Abdalla Hamid, Katibu wa NEC – Siasa na Uhusiano wa Kimataifa.

Aidha, katika mkutano huo, aliyekuwa Katibu wa Wanawake wa Chama cha Chadema Wilaya ya Karagwe,Delphine Andrea, akiwa pamoja na wanachama wengine wengi, walikihama chama hicho na kujiunga na CCM, ambapo kadi zao zilipokelewa na Katibu Makuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi.