Na Hadija Bagasha, Timesmajira Online Tanga
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),Balozi Dkt.Emmanuel Nchimbi ameitaka serikali kuhakikisha viwanda vilivyopo nchini havionekani kama mapambo badala yake viwe viwanda vyenye uwezo wa kushiriki kujenga uchumi wa nchi.
Dkt Emanuel Nchimbi amesema uwepo wa viwanda vingi nchini utawezesha upatikanaji wa ajira za kutosha kwa wananchi ikiwemo kupunguza gharama za usafirishaji kutoka nje ya nchi ambazo ni kubwa.
Huku akitoa wito kwa watanzania wenye nguvu za kuwekeza waige mfano wa wengine ambao tayari wameshafanya jambo hilo kwa kujenga viwanda vidogo na vikubwa ambavyo vimewezesha upatikanaji wa ajira na hivyo kuchangia maendeleo na hatimaye kuongeza fedha za kigeni .
Balozi Nchimbi ameyasema hayo Juni 8,2024 wakati akifungua kiwanda cha Tanga Cable Industry Limited cha jijini Tanga wakati wa ziara yake mkoani humo ambapo amesema kwamba anafarijika kuona wazawa wanachukua hatua ya kuanzisha viwanda.
Amesema katika kujenga viwanda vidogo na vikubwa itasaidia kuimarisha uchumi wa nchi huku akieleza kwamba chama hicho kitaendelea kusimamia Sera yake ya kuhakikisha kwamba sekta binafasi inafanyiwa mazingira ya uwezeshaji kwa lengo la kuchochea maendeleo endelevu yaweze kupatikana kwa urahisi na kasi ya ukuaji wa uchumi wa nchi iwe kubwa zaidi kuliko ilivyo sasa.
Aidha amesema kwamba uwepo wa viwanda vya kutosha nchini utasaidia kuwa na uwezo wa kuuza zaidi kuliko wanavyonunua ili kujipatia fedha za kigeni za kutosha na kujenga uchumi wa nchi.
Amesema kwa sababu ipo changamoto ya uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi ambapo wangependa ifika mahala wajitegemea kwenye uzalishaji bidhaa wao wenyewe pamoja na kuwa na viwanda vya kutosha.
Hata hivyo ametoa wito kwa taasisi za Serikali na sekta binafsi kuona jitihada zinazofanywa na wafanyabishara wazawa zisipotee bure kwa kadri inavyowezekana watumie bidhaa za ndani na hasa wakijiridhisha kwenye ubora wake.
“CCM tutaendelea kusisitiza mara kwa mara tunahitaji viwanda vya ndani na sio kwa ajili ya mapambo bali ni kwa ajili ya kujenga uchumi wa nchi,”amesema Dkt.Nchimbi.
Mkurugenzi wa kiwanda cha Tanga Cable Industry Limited Murtaza Dossaji amesema kwamba uwekezaji uliofanywa kwenye kiwanda hicho ni wa zaidi ya bilioni 1 za kitanzania na wanawafanya kazi zaidi ya 50.
Amesema lengo la uwekezaji huo ni kuboresha sekta ya nishati ya umeme nchini huku wakimshukuru Rais Samia kwa kuwezesha wazawa kwa kutoa mazingira rafiki kwenye sekta ya viwanda.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga Rajabu Abdurhaman amesema kwamba wao wanaridhika kwa asilimia zaidi ya 100 namna Rais Samia anavyoitekeleza ilani ya CCM 2020/2025 kwa kasi kubwa ikiwemo suala la zima la uwekezaji wa viwanda.
Amesema kwa Mkoa wa Tanga jambo hilo linafanyika kwa kasi kubwa na mwenye macho aambiwi tazama pamoja na changamoto ya viwanda vingi vilivyofunguliwa na vikafungwa lakini kwa namna serikali ilivyokuwa macho kwa Mkoa huo wameamua kufanya jambo kubwa la kuwaita wale wote waliokuwa na viwanda hivyo wakavifunga na kuwataka wavifungue ili wananchi wapate ajira na serikali ipate kodi.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba