January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NCAA yaadhimisha siku ya wanyamapori kwa kupanda miti 11,700 vijiji vinavyozunguka hifadhi

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro katika kuadhimisha siku ya Wanyamapori duniani imepanda miti 8000 kwa kushirikiana na Wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari pamoja na Wananchi wanaozunguka eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kwa lengo la kuimarisha mazingira na shoroba za Wanyama.

Kaimu kamishna Msaidizi Mwandamizi wa NCAA anayesimamia Idara ya Wanyamapori na Utafiti Bi. Vicktoria Shayo amebainisha kuwa NCAA imeamua kuadhimisha siku hiyo kwa kupanda miti katika shule Pamoja na shoroba za Wanyama ili kuimarisha ikolojia na kutunza mazingira maeneo mbalimbali pembezoni mwa hifadhi.

“Tulifanya utafiti na kuona kwamba Shoroba hasa inayopita kijiji cha Upper Kitete inahitaji kuimarisha uoto wake wa asili, miti iliyoko pembezoni iliathirika miaka ya nyuma kutokana na shughuli za kibinadamu, tunapanda miti ili kuimarisha uoto wake mapito ya Wanyamapori”

Bi. Vicktoria Shayo ameongeza kuwa sambamba na upandaji miti kwenye maeneo ya Shoroba NCAA Imetumia fursa ya wiki ya maadhimisho ya siku ya wanyamapori kwa kutoa elimu kwenye shule zinazonguka Hifadhi ya Ngorongoro upande wa wilaya ya Karatu na kugawa miti ya aina mbalimbali kwenye shule na wananchi kuipanda ili kuimarisha uoto wa asili na kutunza mazingira.

Mtaalam wa Misitu kutoka NCAA Bw. Naman N. Naman amebanisha kuwa katika maadhimisho ya siku ya wanyamapori duniani ambayo kilele chake ni leo tarehe 3/3/2022 Wataalam wa NCAA wametoa elimu ya upandaji miti na utunzaji mazingira katika shule za Sekondari 4 na shule za Msingi 2, amezitaja shule za Sekondari kuwa ni Awet, Slahhamo, Upper Kitete, Qurus, Shule za msingi ni Korido na Bonde la Faru ambazo zote ziko katika Wilayani Karatu.

“Elimu inalenga kutoa hamasa kwa wananchi kutunza mazingira, kupanda miti na kuitunza lakini pia kuepuka ukataji wa miti hasa maeneo ya pembezoni mwa Hifadhi na mapitio ya Wanyama” alifafanua Bw Naman.

Afisa Uhifadhi mkuu ikolojia wa NCAA Bi Flora Assey ameeleza kuwa eneo la Hifadhi ya Ngorongoro linazungukwa na shoroba tano (5) ambazo ni Upper kitete selela hadi manyara, Shoroba ya laja Eyasi hadi Manyara, Shoroba yaa Manyara Ranch, Shoroba ya Kakesio Maswa hadi yaeda Chini, Makoromba ziwa eyasi hadi Maswa na Shoroba ya loliondo hadi Serengeti.,

NCAA kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imekuwa na utamaduni wa kila mwaka kuzipitia, kupanda miti na kutoa elimu kwa Wananchi ili wasizivamie na kutunza mazingira ya maeneo hayo kwa faida ya kizazi cha sasa naa baadae.