December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NBC ,TIRA yashirikiana kutumia akaunti ya dhamana katika benki

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) wameanzisha ushirikiano na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kuhakikisha Kampuni za bima zinatumia akaunti ya dhamana katika benki ili kuepusha changamoto ya kampuni hizo kutumia fedha bila ruhusa ya Kamishna wa Bima.

Akizungumza katika hafla hiyo jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania(TIRA) Dkt. Baghayo Saqware akifungua mafunzo ya akaunti ya dhamana kati ya TIRA na NBC ambayo yalilenga kuwajengea uwezo wadau wa bima.

“Awali kulikuwa na changamoto ndogo ambapo kampuni za bima zilikuwa na kiwango cha fedha katika Benki ya Tanzania (BoT) lakini kiwango hicho huwekwa kwenye hati fungani na zinapoiva zinarudi katika akaunti ya kampuni ya bima hivyo tukawa tunapata changamoto ya baadhi ya kampuni hizi kutumia fedha hizo bila ruhusa ya Kamishna wa Bima,“amesema Dkt.Saqware.

Amesema ili kuondoa changamoto hiyo wameanzisha akaunti ya dhamana ambayo wanaipa masharti na benki hivyo NBC imetimiza masharti hayo ya kufungua akaunti hiyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Benki ya NBC, Theobald Sabi amesema wamefanikiwa kutimiza matakwa ya masharti yaliyowekwa na TIRA hivyo itawezesha watu wa bima kulindwa.

Amesema kuwa wanategemea kuwapa wateja wao huduma nzuri kupitia mfumo wa kieletroniki ambapo Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania itakuwa inafuatilia mwenendo huo.

“Sisi NBC ni benki ambayo imekuwepo kwa miongo mitano hivyo tunayo furaha kutoa mafunzo haya kwa wadau wa bima,tumejipanga vyema katika kutoa ushauri wa uwekezaji kupitia idara yetu ya hazina na masoko ya mitaji hivyo nitoe wito kwa kampuni za bima nchini kuzingatia taratibu zilizowekwa,”amesema Sabi.

Naye Mkurugenzi wa Usimamizi wa TIRA Abubakar Ndwata amesema chimbuko la akaunti hiyo ya dhamana ya bima ni kanuni ya bima ya mwaka 2009 inayozitaka kampuni za bima kuweka amana za usalama angalau 50% ya kiwango cha chini cha mtaji halisi wa kampuni husika ya bima.

Ndwata amesema TIRA kwa kushirikiana na Chama cha Makampuni ya Bima Tanzania (ATI), walikubaliana kuandaa muongozo wa uwekezaji wa usimamizi wa ukwasi ambao pia ulielekeza uanzishwaji wa akaunti ya dhamana ya akiba kupitia benki za biashara ili kuondokana na tatizo la changamoto ya kimtaji au kushindwa kulipa fidia za madai ya wateja wake.