Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
KAMPENI za Uchaguzi Mkuu wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), ambao unatarajiwa kufanyika siku ya Ijumaa wiki hii zinaendelea kupamba moto kwa ambapo wagombea wanaendelea kunadi sera wakitaka kufanya mabadiliko kwenye taasisi hiyo.
Mmoja wa wagombea wa nafasi hiyo, Sweetbert Nkuba, alisema mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam kuwa anataka nafasi hiyo ili akapambane na mawakili ambao hawana sifa ya kufanyakazi hiyo.
TLS ni taasisi muhimu inayochangia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha mfumo wa sheria na haki nchini Tanzania na kwa mwaka huu wagombea wa nafasi ya urais kwenye uchaguzi huo wa mwaka huu watakuwa sita, Boniface Mwabukusi, Emmanuel Muga, Ibrahim Bendera, Paul Kaunda, Revocatus Kuuli na Sweetbert Nkuba.
Nkuba alisema anauzoefu wa muda mrefu wa uongozi katika ngazi mbalimbali na kuomba achaguliwe kwenye nafasi hiyo ili afanikishe vipaumbele vitano ikiwemo kuwaunganisha wanachama wa TLS na kuhakikisha maslahi ya kiuchumi ya wanachana wa chama hicho yanazingatiwa.
“Nikichaguliwa nitahakikisha wanachama wote wa TLS wanakuwa na bima ya afya, bima ya maisha, nitaaanzisha kituo cha malezi kwa wanachama wanaochipukia, kuimarisha uhusiano baina ya wanachama wa TLS, Serikali, mahakama na jamii kwa ujumla,” alisema Nkuba
Mgombea mwingine Wakili Paul Kaunda amejinadi kuwa yeye si mgeni kwenye uongozi kwani amefanyakazi kwa miaka 10 katika maeneo mbalimbali ya sheria hasa sheria za jina na madai na ni mdau mkubwa sana kwenye mapinduzi ya nne ya viwanda yaani akili bandia (AI).
Alisema kwamba yeye pia siyo mgeni wa kuongoza taasisi kama TLS kwani 2019 -2020 alipata bahati ya kutumika kama Mjumbe wa Baraza la Uongozi na Mjumbe wa Kamati ya Sheria na Katiba ya TLS kwa miaka mitano.
“Nimedhamiria kuleta heshima kwa TLS na nyote ni mashahidi kwamba heshima ya chama hiki imeshuka sana kwa hiyo nitakwenda kurejesha heshima hasa sisi mawakili tunapowawakilisha wateja wetu wakiwa polisi, magereza na mahakamani,” alisema
Naye Ibrahim Bendera alisema amefanyakazi ya uwakili kwa miaka 18 upande wa Tanzania Bara na miaka 19 kwa upande wa Zanzibar hivyo amejipima na kuona anatosha kuongoza chama hicho hasa wakati huu ambapo Rais wa chama hicho ataongoza kwa miaka mitatu badala ya mwaka mmoja.
“Zamani Rais alikuwa anahudumu kwa mwaka mmoja sasa kwa mwaka mmoja siyo rahisi kuleta mabadiliko kwa hiyo baada ya mabadiliko na kuweka ukomo wa miaka mitatu nimeona nitapata nafasi ya kulieleza Baraza la Uongozi maoni yangu na mpango mkakati wa TLS unaisha mwaka huu kwa hiyo nitaweka msukumo wa kutengeneza mpya,” alisema
Alisema kwa mwaka TLS yenye wanachama 12,000 inapata wastani wa bilioni 1.2 na inalipa mishahara inayofikia shilingi milioni 80 kwa mwezi hivyo akichaguliwa atahakikisha anapunguza gharama za matumizi na kuwawekea mazingira mazuri mawakili vijana waweze kupata uzoefu.
Revocatus Kuuli yeye alisema yeye amekuwa wakili kwa miaka 13 Tanzania Bara na wakili Zanzibar kwa miaka minne na kwamba katika mawakili 13 waliosajiliwa na Mahakama ya Arika iliyoko mkoani Arusha yeye ni miongoni mwao.
Alisema anafanyakazi pia kwenye Mahakama ya Umoja wa Mataifa ya IRMCT yenye Makao yake Makuu Geneva Uswis na Arusha Tanzania na kwamba ametumikia nafasi mbalimbali serikali na ngazi yake ya mwisho serikalini alikuwa ofisa Wizara ya Katiba na Sheria.
Naye Wakili Emmanuel Muga alisema amekuwa wakili kwa miaka 12 hivyo amejipima na kuona kuwa anaweza kumudu majukumu ya kuwasimamia mawakili wenzake kama atachaguliwa kushika nafasi hiyo kwenye uchaguzi ujao.
Alisema amekuwa mwenyekiti wa TLS mkoa wa Dar es Salaam kwa kipindi cha miaka miwili akianzia 2019 mpaka 2021 na kwamba fursa hiyo ndiyo ilimpa nafasi ya kuwafahamu mawakili na mahitaji yao na nini kifanyike ili chama hicho kiweze kutimiza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria.
“Nikiwa mwenyekiti wa TLS Mkoa wa Dar es Salaam nilifanikiwa kuunda kamati nane na zilileta mageuzi makubwa sana tunayoyaona kwa Chapter ya chama chetu hapa Dar es Salaam kwa hiyo mafanikio haya ndiyo yamenifanya nione ninaweza kuongoza chama hiki kwa ubora,” alisema
Boniface Mwabukuzi alisema anataka nafasi hiyo ili kuleta mageuzi ambayo kwa muda mrefu yameshindikana ikiwemo kupambana na mafisadi kwenye chama hicho na nje ya chama.
Alisema TLS kwa muda mrefu imeshindwa kutimiza wajibu wake wa kusaidia wanachama kutokana na watu wanaochaguliwa kuiogopa serikali hali ambayo iliwafanya washindwe kusimamia misingi ya kuanzishwa kwa TLS.
More Stories
SACP Katabazi: Elimu ya usafirishaji wa kemikali bado ni muhimu kwa watanzania
REA yajitosa kwenye nishati safi ya kupikia
Maghorofa Kariakoo mikononi mwa Tume